Mwandikishaji wa Daftari la Wapiga Kura (katikati) akisoma jina la mwananchi aliyehitajika kwenda kujiandikisha.
Mwananchi aliyekwenda kujiandikisha (kulia) akipigwa picha na kamera maalum kwa ajili ya kupata kitambulisho eneo la Sinza- Mori, Dar. 

Wananchi waliojitokeza nje ya geti la Shule ya Msingi Sinza-Maalum kwa ajili ya kuanza kujiandikisha huku ndani wananchi walioandikishwa majina yao jana wakipatiwa huduma ya kuandikishwa. 

Mwananchi aliyekwenda kujiandikisha (kulia) akiweka vidole kwenye mashine ya kuchukua alama za vidole eneo la Mlimani City, Dar. 

Mama mmoja, mkazi wa Sinza A akisaidiwa na mwandikishaji jinsi ya kukaa ili aweze kupigwa picha kwa ajili ya kitambulisho cha kupigia kura. 

Wananchi wakiwa katika foleni kusubiria kujiandikisha maeneo ya Mlimani City, Dar.
IKIWA sasa ni siku ya tatu tangu zoezi la uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura uanze kwa teknolojia ya Biometric Voters Regitration (BVR), hali imezidi tete baada ya wakazi wa Dar kupata usumbufu wa kuamka asubuhi na mapema kwenda kujiandikisha na kurudi bila mafanikio.
Mapema hii leo mwandishi wetu amefanikiwa kutembelea baadhi ya vituo kama vya Sinza, Shule ya Msingi Mapambano, Mwenge, Kijitonyama pamoja na maeneo ya Mlimani City Dar na kushuhudia umati mkubwa ukiwa kwenye foleni kwa ajili ya kujiandikisha.
Katika baadhi ya vituo hivyo, zoezi lilionekana likiendelea vizuri huku baadhi ya maeneo yakiwa na changamoto za wananchi kulalamikia ubovu ‘Solar power’ zinazotumika katika mitambo ya uandikishaji kuwa jua linapopungua na mitambo husimama kutokufanya kazi.
Kituo Cha Kijitonyama-Mpakani B, maeneo ya Mori wananchi wengi wamelalamikia foleni kuwa ndefu na zoezi kwenda taratibu, huku wakilalamikia suala la kuandikishwa majina kisha kupatiwa vitambulisho siku inayofuata.
“Tunaomba waandikishaji wa BVR wasilaze majina kwa kuwa inasababisha msongamano na vurugu kwa wananchi wanaojitokeza siku inayofuata tena wakiwa wameamka alfajiri kushinda vituoni hapo,” alisema Amina Suleiman, mkazi wa Sinza-Mori jijini Dar.
Aidha, kwa upande wa waandikishaji nao wamelalamikia wananchi kwa kutozingatia taarifa zinazotelewa juu ya changamoto za kwenda kujiandikisha wakiwa wamejipaka mafuta mikononi hatua inayosababisha mashine kutofanya kazi vizuri.
Waandikishaji hao pia wamezungumzia suala la wananchi kutokuwa wavumilivu katika changamoto hizo wanazokutana nazo pindi wanapokwenda kujiandikisha, hasa pale wanapotumia lugha za kuudhi na kuwataka kuwa wavumilivu