Mahabusu wa Gereza Kuu la Mkoa wa Arusha, jana walizua tafrani katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini hapa, baada ya kuvua nguo na kugoma kushuka kwenye basi wakipinga kitendo cha watuhumiwa wawili wa dawa za kulevya kuachiwa kinyemela.
Watuhumiwa wanaolalamikiwa ambao mashtaka yao yalibadilishwa mara mbili ili wapewe dhamana ni Dharam Patel (26) na Nivan Patel (20) wanaodaiwa kukamatwa na kete 173 za heroini na misokoto 300 ya bangi, Aprili mwaka huu.
Mahabusu hao walikuwa wakipaza sauti kupinga madaraja kati ya wenye nacho na wasio nacho kwa wengine kuachiwa na wengine kubaki ndani kwa kisingizo cha ‘upelelezi haujakamilika’.
Huku wakipaza sauti zao kwa nguvu, mahabusu hao wa kesi za mihadarati ikiwamo mirungi na bangi, wizi wa kutumia silaha na mauaji, walisema wamekaa mahabusu kwa zaidi ya miaka miwili, lakini hawajawahi hata kusomewa maelezo ya awali na kuendelea kuteseka gerezani.
Sauti ilisikika kutoka ndani ya basi: “Wenzetu hata mwezi haujaisha wanafutiwa kesi, jamani sisi tumekosa nini? Tunataka haki itendeke kwa wote.”
Mahabusu hao walionekana wakiwa wamesimama ndani ya basi hilo bila nguo, huku umati wa watu waliofika mahakamani hapo ukitazama.
Baada ya kuona umati wa watu unazidi kuongezeka kuwashangaa mahabusu hao, askari wa magereza waliondoa basi hilo eneo la Mahakama.
Kuachiwa watuhumiwa
Taarifa za kuachiwa kwa watuhumiwa hao wa dawa za kulevya waliokuwa na kesi mbele ya Hakimu Mkazi Arusha, Mwakuga Gwanta zilidaiwa kuwa zilitokana na Ofisi ya DPP Arusha, kubadilisha hati ya mashtaka.
Ilidaiwa kuwa badala ya kudaiwa kuwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya, iliandikwa kuwa walikutwa na dawa hizo mashtaka ambayo yana dhamana.
Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema jana kuwa ofisi yake haina taarifa za watuhumiwa hao kupewa dhamana lakini alisema kulikuwa na jaribio hilo.
Alisema kwa mujibu wa sheria, mtu ambaye anakamatwa na dawa za kulevya zenye thamani chini ya Sh10 milioni anaweza kupewa dhamana, lakini kiwango kikiwa zaidi ya hapo, hapati dhamana.
“Baada ya kubainika kuna njama za mashtaka kubadilishwa, tulipinga kwa kuwa kosa lipo wazi kwamba walikuwa wakisafirisha dawa hizo, sidhani kama wamepewa dhamana... sidhani kama inawezekana ila tunafuatilia kwa karibu tukio hili,” alisema Nzowa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema kazi ya polisi ilikuwa ni kukamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani tu.
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Wilibard Mashauri alisema hahusiki katika malalamiko hayo kwa kuwa si mpelelezi wa kesi.
“Lakini hawa mahabusu wanalalamikia kuachiwa kwa wale watuhumiwa wenye kesi ya dawa za kulevya, kesi ambayo haipo kwangu wala sijui wameachiwa kwa kifungu gani na inategemea na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DP) amewaachia kwa kifungu gani,” alisema.