Showing posts with label SIASA. Show all posts
Showing posts with label SIASA. Show all posts

Sunday, June 19, 2016

Lowassa Atoboa Siri Ya Ujio wa TB Joshua Nchini.....Asema Aliitwa na CCM Kumshawishi Akubali Matokeo ya Uchaguzi Mkuu


Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa amesema hakuridhika na matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, na kwa kulijua hilo, ‘watawala’ walimleta rafiki yake kutoka Nigeria, TB Joshua ili amshawishi akubali matokeo. 

Lowassa alisema baada ya TB Joshua, muhubiri na kiongozi wa Synagogie Church of All Nations, kukaa naye pamoja na viongozi wengine wa Chadema na kumueleza jinsi ‘walivyoporwa’ ushindi, kiongozi huyo wa kidini alichukia na kusitisha azma yake ya kuhudhuria sherehe za kumuapisha Rais John Magufuli.

TB Joshua aliwasili nchini Novemba 3, siku mbili kabla ya kuapishwa kwa Magufuli kuwa Rais, na alienda Ikulu na baadaye nyumbani kwa Lowassa ambaye alitumia muda mwingi wa ziara yake pamoja naye. 

“Walimuita rafiki yangu TB Joshua, wakaenda wakampokea. Alipokelewa na Rais Magufuli, akapelekwa Ikulu akazungumza na Kikwete,” alisema Lowassa. 

“Baadaye akawaambia wamlete kwangu. Kweli akaja nyumbani kwangu, tukazungumza naye. Sitaki kusema mengi sana niliyomwambia, lakini moja, nilimwambia ukikubali yale matokeo ndugu yangu, heshima yako itashuka hapa nchini na duniani kwa ujumla,”alisema. 

Lowassa alisema hayo jana alipokuwa akizungumza katika mahafali ya Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Wafuasi wa Chadema (Chaso) katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam. 

Alisema ni kutokana na msimamo na mazungumzo waliyofanya na TB Joshua ndio yaliyosababisha kiongozi huyo wa kidini maarufu barani Afrika kutohudhuria sherehe hizo za kuapishwa zilizofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

Katika hotuba yake, Lowassa alimpongeza Rais Magufuli kwa jitihada anazozichukua za kujaribu kufufua uchumi wa nchi, lakini akasema hakubaliani na mbinu anazotumia. 

Alisema anafurahia kumsikia Rais Magufuli akiihubiri nchi ya viwanda, lakini hana imani na lugha anazotumia.

“Rafiki zangu nawasikia na nafurahi sana wanasema wanataka kujenga nchi ya viwanda. Natamani nchi hiyo, lakini lugha hiyo sina imani nayo sana,” alisema. 

Alisema haziamini lugha hizo kwa kuwa ni vitu visivyowezekana kutokana na ukweli kuwa viwanda vilivyopo haviwezi kufufuka na kuondoa tatizo la ajira lililopo nchini. 

“Wanasema watafufua viwanda, lakini viwanda vilivyopo vili kuwa analojia sasa hivi mambo yote ni ‘digital’. Hicho kiwanda kitafufuliwaje maana hata madukani spea zake hazipo labda zitengenezwe upya,”alisema. 

Alisema tatizo lililopo kwa sasa nchini ni la ajira na kwamba hata kaulimbiu yao kwenye kampeni ilikuwa ajira kwa kutambua kuwa wapo vijana wengi waliomaliza vyuo, hawana ajira na kwamba eneo kubwa litakaloweza kuwaajiri ni sekta ya kilimo. 

Lowassa, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, alisema anakubaliana na kauli iliyotolewa na Jenerali Ulimwengu aliyoitoa hivi karibuni kuwa Rais Magufuli ameturudisha nyuma miaka 50, akiponda uamuzi wa Serikali kuzuia matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja. 

“Uamuzi ule si mzuri na una matatizo makubwa kwa kuwa ni kuwanyima wananchi haki yao muhimu ya kuwasikiliza wawakilishi wao,” alisema.

Akizungumzia elimu, Lowassa alisema wakati Chadema na Ukawa waliposema watatoa elimu bure kuanzia chekechea mpaka chuo kikuu walikuwa wamejipanga, lakini Serikali imebeba sera hiyo bila kujiandaa.

Aliwapongeza vijana kwa kuwa kiini cha mabadiliko na kusema mpaka sasa akikutana na watoto wadogo wanamsalimia kwa kumwambia “Mabadiliko Lowassa”. 

Alisema vijana walifanya kampeni nzuri na kumwezesha kupata kura nyingi zilizowapa ushindi, lakini wakanyimwa ushindi. 

“Tulishinda vizuri sana lakini hata hizo walizotupa, zinatosha kuwaambia kuwa tuliwapa kazi ya kutosha. Nyie mnajua, wao wanajua na mimi najua,” alisema. 

Lubuva aondolewe 
Alisema licha ya kumuheshimu mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, anapaswa kutimuliwa kwa kushindwa kuisimamia vyema tume hiyo. 

“Tume ya Uchaguzi inapaswa iondoke. It must go na ndio maana nasema iko haja ya kuanza upya kudai Katiba mpya haraka iwezekanavyo,” alisema Lowassa. 

“Kama yupo mtu yeyote anayechukia matokeo ya uchaguzi uliopita, suluhisho lake ni kuwa na tume huru ya Uchaguzi itakayotokana na Katiba mpya. Tusipohangaika na Katiba mpya tutarudi palepale.”

Alirudia kauli yake kuwa baada ya uchaguzi kulikuwa na waliomtaka atangaze “kuingia barabarani”, lakini aliwakatalia. 

“Tutakuwa tunakwenda Ikulu kwa kufagia barabarani kwa damu za watu. No, tutakwenda Ikulu bila damu za watu wakati wowote na Mungu atatusaidia. Nawaambia wale wote ambao hawakuridhika, mnajua nguvu ya umma lakini msiitumie kuwaumiza watu,” alisema. 

Aliwataka viongozi wote wa Chadema kujali maslahi ya wanyonge kwa kuepuka kufanya kazi kwa mazoea. 

Meya wa Jiji la Dar es Salaam ambaye ni diwani wa Chadema, Charles Mwita aliwataka wanafunzi kufanya kazi ya kukijenga chama kwani mabadiliko ya kweli yataletwa na vijana. 

Muasisi wa Chaso, Pamela Maasaio aliwataka vijana wa Chadema kuachana na siasa za kwenye mitandao na badala yake waende mitaani kupiga kelele na kuweka mikakati ya pamoja.

Katibu Mkuu wa Chadema Akwea Pipa Kujinoa Kisiasa Ujerumani


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji anatarajia kuhudhuria kongamano la kujadili sauti za wananchi kupitia Bunge katika maendeleo na Taifa litakalofanyika Ujerumani, Juni 20 hadi 25.

Msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene alisema jana kuwa, kongamano hilo litajadili mikakati ya kampeni na kushinda uchaguzi, hususan kwenye mazingira yenye changamoto mbalimbali za kisiasa huku pia wakijifunza umuhimu na nafasi ya Serikali za mitaa katika maendeleo ya wananchi.

“Katibu Mkuu Dk Mashinji pamoja na washiriki wengine watajadili kwa kina na kubadilishana uzoefu wa ushindani wa siasa kutoka maeneo mbalimbali, huku pia wakijifunza umuhimu wa kutumia teknolojia ya mawasiliano kupambana na changamoto za kisiasa, hasa katika nchi zinazoendelea,” alisema Makene.

Mada nyingine katika kongamano hilo zitahusu mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, kuwasaidia vijana kutambua umuhimu wa siasa na kushiriki.

Mbali na Dk Mashinji washiriki wengine watatoka nchi za Ufaransa, India, Ujerumani, Ghana, Ufilipino, Mexico, Mongolia, Argentina, Ukraine, Poland, Bolivia, Cambodia, Syria, Tunisia, Uganda, Kurdistan, Venezuela, Hoduras na Ugiriki.

Monday, June 13, 2016

Zitto Kabwe Aibuka Baada ya Kupotea kwa Siku Mbili.....Kasemaje??? BOFYA Hapa

Baada ya taarifa za kutoweka, Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameibuka leo na kusema yuko salama wa afya huku akilaani mbinu za Jeshi la Polisi kutaka kumkamata kwa siri bila kufuata utaratibu unaotakiwa.

Tangu Jumamosi usiku, vyombo mbalimbali vya habari viliripoti Zitto kutofahamika alikokuwa baada ya simu zake zote kutopatikana huku viongozi wa chama hicho wakihofia kukamatwa na polisi baada ya kubaini njia za uviziaji wa kumkamata nyumbani
kwake.

"Ilikuwa Jumamosi , walikuja nyumbani kwangu wakiwa na magari matatu ila hawakufanikiwa, siwezi kukamatwa kwa `terms' zao ila nitakuwa tayari kukamatwa kwa `terms' zetu na wala siyo kuviziana, kama nina makosa kwa nini wanivizie," amesema Zitto Kabwe na kuongeza;

''Watu wetu wa Usalama wa Chama walihakikisha kwamba sitakamatwa ili niweze leo kupata fursa kuzungumza na watanzania kupitia nyie wana habari
 

''Hatufahamu Watawala wanaogopa nini mpaka kuzuia mikutano ya wanasiasa
 

''Nasikia Jana Walimkamata Mwenyekiti Mbowe wa Chadema Huko Mwanza kisa eti kawasalimia wananchi, huu ni uvunjwaji na ukiukwaji mkubwa wa utawala wa kidemokrasia

''Tunalaani tabia za Kidikteta za Rais Magufuli .Magufuli ameanza na vyama vya siasa kuonyesha Udikteta wake, nawahakikishia akimalizana na Vyama vya siasa atahamia kwenu Wanahabari, Tumkatalie
 

''Ndio maana Magufuli Ziara yake ya Kwanza alifanya Rwanda, tumegundua kuwa alikwenda kujifunza namna ya Kudhibiti Demokrasia na Kuongoza Kidikteta
 

''Hauwezi kupambana na Ufisadi kama haumpi nguvu ya Kiutendaji wa CAG. Kwa hali Hii anayokwenda Magufuli ajiandae kuwa rais wa term moja kwa sababu watanzania hawataweza kuvumilia kutawaliwa, kuminywa na kuburuzwa .

''CCM wamdhibiti Magufuli, na wasipomdhibiti sisi na Watanzania Tutamdhibiti
 

''Hatutakaa Kimya hata kama atatufunga, akimfunga Zitto watazaliwa wakina Zitto wengine, na kwenye hili hatutakaa Kimya, tutasimama kidete mpaka nchi irudi kwenye misingi''
 

''IGP ameagizwa na Magufuli anikamate, lakini hawezi kunikamata bila kufuata utaratibu, hawawezi kunikamata kwa kunivizia, viongozi hatukamatwi kwa kuviziwa viziwa, tumewaonyesha kwamba Polisi wanaweza kutukamata kwa kufuata terms zetu na sio zao
 
''Karibuni kesho saa tisa kwenye Kongamano letu, Hatuwezi kuacha kufanya siasa, lazima tuendelee kufanya siasa, mmehudhuria mikutano yetu hamjaona hata sisimizi amekanyagwa
 

''Wanasema Bajeti imeongezeka kwa 32% ukweli ni kwamba Bajeti imeshuka kwa maana Dola imeporomoka''

Audio: Gwajima afyatuka tena, amshauri Magufuli aihame CCM....Adai amenasa njama Mbaya


Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye anafahamika kwa kutoa kauli ‘tata’, amefyatuka tena akimshauri Rais John Magufuli kuihama CCM endapo kile alichokiita ‘njama alizozibaini’ ndani ya chama hicho zitaletwa mezani.

Gwajima ambaye amekiri kuwa katika kampeni alikuwa hamkubali Dk. Magufuli kutokana na kutokuwa na imani na CCM, amesema amemkubali  sana baada ya kuanza kazi ya urais kutokana na hatua ambazo amekuwa akizichukua ndani ya muda mfupi.

Akizungumza katika ibada ya Jumapili kanisani kwake, Gwajima ameeleza kuwa amebaini njama za baadhi ya wanachama wa CCM ambao ‘dili’ zao mbalimbali ikiwa ni pamoja na ‘flow meter’ ya mafuta yaingiayo nchini na makontena yaliyokamatwa yalikuwa yanawahusu, wameanza kampeni ya chinichini nchi nzima kutaka Rais Magufuli asipewe uenyekiti wa chama hicho.

Amesema kuwa watu hao wanazunguka nchi nzima kuwashawishi wanachama wa CCM kuridhia hoja ya kutenga uenyekiti wa chama na urais, ili kumnyima nafasi hiyo Rais Magufuli ambaye utendaji wake umewabana bila kujali ni wa chama chake.

Hivyo, amemshauri Rais Magufuli kuwa endapo itatokea hilo, akihame chama hicho na kuendelea na kazi yake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mengine, msikilize mwenyewe hapo chini:


Freeman Mbowe na Viongozi Wengine wa Chadema Wakamatwa.....Alipo Zitto Kabwe Bado ni Utata

Wakati Polisi ikimshikilia kwa saa mbili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mkoani Mwanza, jeshi hilo limefuta kongamano la kujadili Bajeti ya Serikali lililoandaliwa na ACT Wazalendo jijini Dar es Salaam huku kiongozi wake, Zitto Kabwe akisakwa.

Jeshi hilo lilizuia mkutano wa hadhara wa Chadema uliokuwa ufanyike wiki iliyopita mjini Kahama ambako lilitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanachama na wafuasi wa chama hicho, katika kile kilichoelezwa kulikuwa na dalili za uvunjifu wa amani.

Jeshi hilo pia lilizuia msafara wa viongozi wa chama hicho kuingia katika ofisi zake za Shinyanga walipokuwa wakielekea Mwanza.

Taarifa iliyotolewa jana na msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene ilieleza kuwa mbali na Mbowe, jeshi hilo pia lilikuwa linawashikilia Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi na Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita.

Wengine ni Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka na viongozi wengine na wanachama wa chama hicho waliokuwa wanashikiliwa katika kituo cha Polisi Nyakato, jijini Mwanza.

Makene alisema tangu asubuhi ya jana, Mbowe na viongozi wenzake walikuwa wakizunguka katika maeneo kadhaa ya jijini Mwanza kuwasalimia wananchi katika ‘vijiwe’ mbalimbali kabla hawajakamatwa.

Alisema, “Hadi sasa (saa 11 jioni) hakuna maelezo ya kushikiliwa kwao.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alithibitisha kukamatwa kwa viongozi hao na kubainisha kuwa waliachiwa bila kufunguliwa kesi yoyote.

“Walikutwa Igoma Sokoni wakizungumza na wananchi. Mikutano ya namna hii imezuiwa. Wamefungua kesi mahakamani, hivyo hakuna haja ya kufanya tofauti mpaka itakapohukumiwa,” alisema Msangi.

Alifafanua kuwa jeshi hilo halina uhasama wowote na Chadema au chama kingine chochote na "hatuwezi kukiingilia kinapofanya mikutano yake ya ndani au hotelini. Kilichozuiwa ni mikutano ya hadhara.”

Wakati Msangi akisema hayo, kongamano la ACT Wazalendo ambalo lilitakiwa lifanyike jana kuanzia saa 7:00 mchana kwenye Ukumbi wa Jengo la LAPF; Millennium Towers, Kijitonyama lilizuiwa na polisi.

Tangu mapema asubuhi, askari polisi walitanda katika eneo la ukumbi huo kuzuia kongomano hilo.

Ukumbini hapo, waandaaji walisema hakuna anayeruhusiwa kuingia kwani wamepewa maelezo ya kuufunga baada ya tukio lililoandaliwa kuahirishwa.

Zaidi ya viti 210 vilikuwa vimepangwa kwa ajili ya kongamano hilo na mmoja wa viongozi wa ukumbi huo alionekana akiondoa mabango yaliyokuwa yanautambulisha mkutano huo wa ACT.

Viongozi watatu wa ukumbi huo walikataa kueleza kinagaubaga juu ya sakata hilo, lakini taarifa za jumla zilisema mkutano umezuiwa.

Mmoja wa watumishi wa ukumbi huo, alisema: “Tuliandaa kila kitu, ila shughuli imeahirishwa. Ukumbi unatakiwa kufungwa. Hautatumika kwa leo.”

Ilipofika saa 5:00 asubuhi, Msemaji wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis alisema chama kinafanya mkutano wa dharura kwenye ofisi zake za makao makuu na baadaye kingezungumza na waandishi wa habari.

Saa 8:00 mchana, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mghwira akiwa na viongozi wenzake, isipokuwa Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe alikuwa mbele ya kamera za wanahabari akifafanua kilichotokea kwa wanachama, wafuasi wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla.

Alisema ilipotimu saa 4:00 asubuhi walipewa taarifa na mwenye ukumbi kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni limemjulisha kuwa chama hicho hakina kibali cha kuendesha kongamano hilo na kwamba kisiruhusiwe kufanya hivyo.

“Huku ni kufifisha demokrasia. Wapigania haki za kiraia wasimame imara na vyama vya upinzani katika kuilinda,” alisema Mghwira.

Wakati kongamano hilo likizuiwa, kuna taarifa za kukanganya juu ya alipo Zitto baada ya kudaiwa alikuwa anasakwa na polisi tangu juzi.

Taarifa hizo zinakuja siku chache baada ya kiongozi huyo kuitwa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam na kuhojiwa juu ya kauli alizozitoa kwenye mkutano wa hadhara zinazokosoa utendaji wa Serikali na kupinga matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.

Baadaye jioni, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Msafiri Mtemelwaalitoa taarifa kuwa Zitto ametoweka na hajulikani alipo. Hiyo ilikuwa ni baada ya askari kanzu kumtafuta kwa muda kwa saa kadhaa.

“Zitto amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu. Askari wanalinda nyumbani kwake tangu jana (juzi) usiku. Hivi sasa ametoweka, hatujui alipo. Lolote litakalompata, Jeshi la Polisi litajibu,” alisema Mtemelwa.

Awali, Mghwira alipoulizwa imekuwaje kuhusu Zitto alijibu kuwa mkutano ulikuwa wa dharura ndiyo maana viongozi wote hawakuwapo.

Tuesday, June 7, 2016

Taarifa ya Ofisi ya Spika kuthibitisha kupokea hoja ya kumeondoa madarakani Naibu Spika

Ofisi ya Spika imepokea taarifa ya kusudio la kuleta Bungeni Hoja ya kumwondoa madarakani Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb) iliyowasilishwa na Mbunge wa Simanjiro Mhe. Mhe. James Kinyasi Millya siku ya Jumatano tarehe 1 Juni, 2016.

Utaratibu huo ni wa Kikatiba na upo chini ya Ibara ya 85(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ambapo pia umeainishwa katika Kanuni ya 138 (1), ya kanuni za Kudumu za Bunge kuhusu utaratibu wa Kumwondoa Naibu Spika Madarakani.

Baada ya kupokea kusudio hilo, Kanuni za Bunge zinamtaka Spika kuiwasilisha hoja hiyo katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ifanyiwe kazi.

Kutokana na msingi huo wa kikanuni, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai (Mb) anakusudia kuliwasilisha swala hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kama Kanuni inavyoelekeza ambapo kamati hiyo itaangalia msingi wa hoja na endapo itaridhika, kanuni inaitaka Kamati kuwasilisha hoja hiyo Bungeni ili ijadiliwe.

Aidha, Kanuni ya 138 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, inamtaka Spika kukalia kiti wakati wa mjadala wa hoja ya kumwondoa Naibu Spika Madarakani.

Hivyo basi, suala lililowasilishwa na Mhe. James Kinyasi Millya kuhusu kusudio la kumwondoa Naibu Spika Madarakani, tayari limepokelewa na lipo katika Ofisi ya Spika kwa ajili ya utekelezaji wa masharti ya Kanuni.

Imetolewa na,
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Ofisi ya Bunge
DODOMA
6 Juni, 2016.

Wabunge wa Upinzani Wanaosusia Vikao vya Bunge Wataendelea Kulipwa Posho Zao


Udhaifu wa Kanuni za Bunge katika kufafanua mambo mbalimbali ya uendeshaji wa Bunge, umeelezwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuwa unatakiwa kurekebishwa ili kutoa nafasi ya Kiti cha Spika kutoa uamuzi dhidi ya vitendo visivyokubalika vinavyoendelea ndani ya Bunge.

Amesema hayo jana alipokuwa akitoa majibu wa muongozo alioombwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe na Mbunge Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM) kuhusu uhalali wa posho wanazolipwa wabunge wa Kambi ya Upinzani, ambao wamekuwa wakiingia bungeni kusaini posho na kwenda kupumzika.

Dk Tulia alisema tangu Mei 30, mwaka huu, wabunge hao wamekuwa wakiingia bungeni kusaini posho na kuondoka kwenda kupumzika, jambo lililosababisha Dk Mwakyembe kuomba muongozo kama malipo hayo ni haki kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya Katiba ya 23.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 23, ibara ndogo ya kwanza na ya pili; “Kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na kiasi na sifa za kazi wanayoifanya.Kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya haki.” 

Akitoa muongozo wake kama malipo hayo ya posho ni halali kwa mujibu wa Katiba au la, Naibu Spika alisema ametumia uamuzi wa Kiti cha Spika uliotolewa Aprili 27, 2016 kuhusu muongozo kama huo.

Alisema Kiti cha Spika katika muongozo huo wa Bashe, kilinukuu Katiba Ibara ya 73 inayosema, “Wabunge wote wa aina zote watashika madaraka yao kwa mujibu wa Katiba hii, na watalipwa mshahara, posho na malipo mengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.”

Mbali na malipo hayo kulindwa na Katiba, Dk Tulia alisema pia Sheria ya Uendeshaji wa Bunge Sura ya 15 na 19 Kanuni za Bunge zinaelezea kuwa mbunge anapohudhuria vikao vya Bunge, atalipwa posho.

Dk Tulia alisema vitendo vya kutohudhuria mjadala wa Bunge havikubaliki kwa kuwa havikidhi matakwa ya Katiba Ibara ya 23, lakini akasema pamoja na Kiti cha Spika kusisitiza kuwa kutohudhuria mjadala hakukubaliki, lakini kuna haja ya kubadili sheria ili mbunge alipwe baada ya kumaliza kazi.

Pia alisisitiza kuwa Kanuni za Bunge zinazotumika katika kuwalipa posho, hazijaeleza kwa uwazi maana ya neno mahudhurio, hivyo nazo zinahitaji marekebisho kudhibiti hali hiyo.

Baaada ya kutoa muongozo huo, Keissy alisimama na kuomba muongozo mwingine na alipopewa nafasi, aliomba utaratibu wa kutumia mashine za kielektroniki kusaini mahudhurio, ubadilishwe na badala yake urejeshwe ule wa zamani wa mbunge kusaini katika karatasi.

Dk Tulia akijibu muongozo huo, alisema hata ukirejeshwa utaratibu huo, mbunge anaweza kusaini katika karatasi saa tano na kuondoka kwenda Dar es Salaam na kusisitiza kunahitajika marekebisho ya Kanuni za Bunge ili neno mahudhurio, lipewe ufafanuzi wa wazi.

Hata hivyo, aliahidi kuwasiliana na Katibu wa Bunge ili kuona utaratibu mzuri wa wabunge kusaini posho katika wakati wa sasa. 

Baada ya muongozo huo wa Naibu Spika, Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu alidai wao wataendelea kususia vikao vyote vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika kwa madai kuwa anatumia Kanuni za Bunge, kuwakandamiza.

Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni, Mbilinyi alisema wabunge wa Kambi ya Upinzani wanaposusa hawarudi nyumbani kupumzika, bali wanashinda katika maktaba ya Bunge kufanya kazi.

Mbilinyi alisema ni heri wabunge wa Kambi ya Upinzani wanaoshinda katika maktaba ya Bunge, kuliko wa CCM wanaohudhuria vikao hivyo.

Saturday, June 4, 2016

Kauli za Rais Magufuli Zawa Gumzo Nchini

Kauli mbalimbali zinazoendelea kutolewa na Rais John Magufuli, zimezua mjadala miongoni mwa wasomi nchini.

Kwa mfano, wanasema kauli ya kukosoa udahili wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na ile ya kuelekeza hatua za kuchukua dhidi ya watu wanaotumia kimakosa barabara za Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), inaashiria kuna tatizo kubwa la utendaji serikalini.

Walisema ni jambo lisiloingia akilini, wanafunzi wadahiliwe na kuanza masomo kisha baadaye wafukuzwe kwa maelezo kuwa Serikali haiwezi kulipia ada wanafunzi ‘vilaza’.

Akizungumzia kauli hizo jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse alisema hakuna sheria za usalama barabarani zinazotamka mtu akifanya kosa gari lake litolewe magurudumu.

Juzi wakati akiweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa maktaba ya kisasa ya UDSM, Rais Magufuli alisema mpango maalumu uliopitishwa na Serikali ya Awamu ya Nne wa wanafunzi kusoma diploma ya ualimu Udom, unajumuisha waliofeli.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim alihoji: “Rais amesema wanafunzi waliopo Udom ni vilaza ila waziri wa elimu (Profesa Joyce Ndalichako) alisema wanafunzi wanaosoma mafunzo hayo hakuna aliyepata daraja la nne. Sasa hapo nani mkweli.”

“Kupishana huku kwa kauli kunatupa mashaka na utendaji kazi wa baadhi ya viongozi serikalini."

Hamad alisema suala kama hilo lilipaswa kutolewa ufafanuzi na waziri husika na si Rais.

Alisema umefikia wakati wa kiongozi huyo mkuu wa nchi kubaini changamoto na kutoa maelekezo na si kuzungumzia kila kitu.

Friday, June 3, 2016

Watoto Mkoani Iringa Wapigwa Marufuku Kutembea Saa 12 jioni na Kuendelea

Serikali wilayani Iringa imetoa waraka unaozuia watoto wenye umri wa kuanzia miaka 14 kushuka chini, kutotembea usiku kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ulawiti na ubakaji.

Wiki moja iliyopita wananchi walimpiga hadi kumuua kijana aliyefahamika kwa jina moja la Emmanuel (25-30), baada ya kukutwa akimbaka mtoto mwenye umri wa miaka kumi, katika eneo la Mtwivila, Manispaa ya Iringa.

Pia, katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita matukio 36 ya ubakaji yameripotiwa kutokea manispaa hiyo huku watuhumiwa 17, wakitiwa mbaroni.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema hali ni mbaya hivyo kila mzazi na mlezi anapaswa kumlinda mtoto wake.

Kasesela alisema waraka huo unawataka wazazi na walezi kutowatuma watoto kuanzia saa 12.00 jioni.

“Ni marufuku mtoto kutumwa kuanzia saa 12, wazazi na walezi wanatakiwa kuwalinda na kuwatunza watoto wao kwa kuwahakikishia usalama,” alisema.

Waraka huo pia umezuia watoto kuzurura hovyo mitaani kwa kuwa wabakaji wamekuwa wakitumia mbinu nyingi ikiwamo kuwalaghai kwa pipi au kuwatuma.

“Ni marufuku watoto kuonekana baa au vilabu vya pombe za kienyeji, ikibainika wamiliki watachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema.

Alisema matatizo ya ubakaji na kuwalawiti watoto yamekuwa sugu na kwamba unahitaji ushirikiano baina ya polisi, wananchi na viongozi kupambana nayo.

“Nimeagiza polisi kuongeza doria na watuhumiwa wanaokamatwa kwa ubakaji, sheria ichukue mkondo wake ili kukomesha hali hii,” alisema.

Aliwaomba viongozi wa dini kusaidia kutoa elimu kwa waumini wao juu ya kuwalinda watoto na kukemea ukatili huo ambao ni hatari ikiwa utaachwa kuendelea.

Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa, Joseph Lyata alisema imani za kishirikina zimechangia ubakaji na ulawiti kwa watoto kukithiri.

Alisema katika uchunguzi wao walibaini vikaratasi vilivyokuwa vikisambazwa mitaani vikishauri wanaume wanaotaka kufanikiwa kimaisha, wabake na kulawiti watoto wadogo kisha wajiunge na dini yao ya ‘freemason’.

“Mtaa wa Semtema ndiyo ulikuwa tishio na huko tuliokota vikaratasi vilivyokuwa vimeandikwa ukitaka kutajirika, jiunge na freemason pia ubake au kulawiti mtoto chini ya miaka 14,” alisema.

Lyata alisema sababu nyingine ni ulevi wa kupindukia na utumiaji wa dawa za kulevya kama bangi.

Alisema kukithiri kwa vitendo hivyo kumeifanya manispaa hiyo kutangaza jambo hilo kuwa ni janga ambalo lazima wapambane nalo kwa kuwasaka wabakaji.

Naibu meya aliwataka polisi kudhibiti vitendo hivyo vinginevyo watoto wataendelea kuteseka.

Alisema wapo watoto wanaofanyiwa ukatili huo majumbani na wengine mitaani. Alisema wameanza kuwatambua watoto wa mitaani na kuwarudisha makwao ili kuwanusuru kubakwa.

Watoto wasimulia 
Baadhi ya watoto walisema wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo na vijana waliopo mtaani, hasa nyakati za jioni.

 “Siku hiyo nilitumwa na mama dukani, wakati narudi kuna mtu akanipa hela nimnunulie mafuta ya taa nimpelekee kwake, nilipompelekea akanifanyia hivi,” alisema mtoto huyo.

Alisema mbakaji huyo alimtishia endapo atasema angemfanyia tena ukatili huo bila huruma.

“Nilimpa mama mafuta, nikaenda kulala nikilia sana niliogopa kumwambia, bahati aligundua kwa sababu sikuwa naweza kutembea na aliponikagua akakuta nimeumizwa,” alisema.

Mama wa mtoto huyo alisema mbali na kuumizwa mwanaye aliambukizwa magonjwa ya zinaa. Aliiomba Serikali kutowanyamazia wanaume wenye tabia ya kuwabaka watoto.

Mtoto mwingine wa kiume alisema kijana asiyemjua alimpatia pipi akijifanya rafiki yake, hali iliyomfanya waongozane hadi mlima wa Semtema, ambako alimlawiti.

Wananchi walia 
Kukithiri kwa vitendo hivyo kuliwafanya wananchi waandamane hadi kwa mkuu wa wilaya kuomba msaada. Wananchi hao walieleza kuwa kinachowatesa ni watuhumiwa kuachiwa huru na polisi na kurejea mtaani.

“Ndiyo maana tumeamua tutakayemkuta tunammaliza kwa sababu akienda polisi atarudi tu,” alisema Gerald Matibabu.

Wazazi hao walidai vitendo hivyo vimewachosha, na kwamba wapo watoto walioambukizwa magonjwa ya zinaa ikiwamo Ukimwi.

Mwenyekiti wa mtaa wa Semtema wenye wakazi 3,800, Reminus Ndale alisema mpaka sasa idadi ya watoto waliofanyiwa unyama huo kwenye mtaa wake ni wanne.

Alisema kwa kushirikiana na wananchi wameamua kuhakikisha watoto wao wanalindwa na kuwachukulia hatua kali watakaobainika kuwabaka.

Polisi wazungumza 
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, John Kauga alikiri kuwapo kwa vitendo vya ulawiti na ubakaji na kuwataka wananchi kutoa taarifa haraka vinapotokea.

“Kuna matukio mengi pia majumbani, wazazi wasifiche, watoe taarifa kwa polisi ili hatua kali za kisheria zichukuliwe,” alisema.

Aliwataka wananchi kupinga imani za kishirikina zinazowahamasisha kufanya ukatili kwa watoto kwa madai ya kutajirika.

Mwakyembe Ataka Mishahara na Posho za Wabunge wa UKAWA Zifutwe.........Keissy Awafananisha na Watumishi HEWA


WABUNGE wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambao wamekuwa wakiingia bungeni kusaini posho na kuondoka, wako hatarini kufutiwa posho kama wataendelea kususa vikao vya Bunge kama walivyotangaza.

Hali hiyo inatokana na hoja zaidi ya mbili zilizowasilishwa kwa Spika wa Bunge kwa njia ya Mwongozo huku moja ikiwasilishwa na Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, zikikusudia kutaka Bunge kufuta posho za wabunge hao.

Akizungumza jana bungeni baada ya kuruhusiwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Dk Mwakyembe akitumia ibara za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na Kanuni za Kudumu za Bunge, alitaka uongozi wa Bunge kutazama upya kama wabunge hao wanastahili kulipwa posho.

Dk Mwakyembe, kwanza alitumia Ibara ya 26 ibara ndogo ya kwanza na ibara ndogo ya pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo aliinukuu; “Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano. Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi.”

Baada ya hapo alinukuu tena Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 23, ibara ndogo ya kwanza na ya pili; “Kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na kiasi na sifa za kazi wanayoifanya. Kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya haki.”

Kwa kuzingatia ibara hizo za Katiba, alisema kwa kutumia nafasi yake ya raia wa Tanzania na Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria, alihoji kama haki inatendeka, kulipa posho na stahiki wabunge ambao hawakuingia bungeni wala hawakuwa katika shughuli inayotambuliwa na Bunge, sawa na waliokuwa wakifanya kazi bungeni.

Alitaka Bunge lifafanue kwa kuzingatia ibara hizo za katiba kama ni haki kulipa wabunge hao wa Ukawa, wanaoingia bungeni na kusaini ili walipwe posho, kwa kubonyeza vitufe vya kielektroniki na kuingia bungeni kwa sekunde chache na kutoka kwenda kupumzika. 

Kuhusu wabunge waliosimamishwa kazi na Bunge, Dk Mwakyembe alihoji kama Bunge linazingatia Kanuni ya 75, ama la.

Kanuni hiyo inasema: “Mbunge aliyesimamishwa kazi atatoka katika Bunge na hataingia tena katika sehemu yoyote ya Ukumbi wa Bunge na maeneo ya Bunge kwa muda wote atakapokuwa amesimamishwa, na atalipwa nusu mshahara na nusu posho zinazoambatana na mshahara huo.”

Kabla ya Mwongozo wa Dk Mwakyembe, juzi usiku Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy (CCM) aliomba Mwongozo na aliporuhusiwa alimtaka Naibu Spika aeleze kama kitendo cha wabunge hao wa Upinzani kuingia na kukaa muda mfupi na kutoka bungeni, kinatofautiana na tatizo la wafanyakazi hewa ambao wanapigwa vita na serikali.

“Kweli Mheshimiwa Naibu Spika, serikali inawaona na wewe unawaona, hii si kuiibia serikali? Au na sisi tuanze?” Alihoji Keissy.

Mbali na Keissy, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) aliomba Mwongozo jana na kumtaka Naibu Spika kuzingatia Mwongozo wa Dk Mwakyembe na Keissy, akieleza kuwa kama si dharau kwa Bunge, kumsimamisha mtu kazi, halafu anaruhusiwa kuitisha mikutano ya kibunge jimboni.

Alimtaka Naibu Spika ambaye ni mwalimu wa sheria, akubali iletwe hoja ya kurekebisha Kanuni za Bunge ili adhabu inayotolewa kwa mbunge, imdhibiti asifanye shughuli zozote ikiwemo mikutano ya hadhara wakati wa adhabu.

Akipokea miongozo hiyo, Naibu Spika aliahidi kutolea uamuzi baadaye baada ya kufanya mashauriano huku suala la adhabu likirejeshwa kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Wabunge wa Ukawa kuanzia mwanzoni mwa wiki hii waliazimia kususa kuingia bungeni katika vipindi vyote vitakavyoongozwa na Naibu Spika, kwa madai kuwa anawaongoza kibabe kama wanafunzi na kuwa hajui uchungu wa kampeni katika majimbo.

Hata hivyo, juzi Dk Tulia  aliwataka Watanzania wasikubali kupotoshwa na Kambi Rasmi ya Upinzani, iliyoamua kususa vikao anavyoviongoza, kwa kuwa kama wanaona amekosea, kuna fursa ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake.

Kwa upande wao, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imewasilisha kwa Ofisi ya Spika wa Bunge kusudio la kumwondoa madarakani Naibu Spika wanayemtuhumu kwa mambo sita ikiwemo upendeleo, ubabe na kufanya kazi kwa maslahi ya Serikali, badala ya umma.

Kusudio hilo la maandishi lilipelekwa katika ofisi hiyo jana na kupokelewa na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah kwa niaba ya Spika, Job Ndugai ambaye hakuwepo ofisini wakati huo.

Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya (Chadema) ndiye aliyewasilisha kusudio hilo kwa niaba ya kambi hiyo ya upinzani na kuzungumza na wanahabari kuhusu hatua hiyo, katika mkutano na vyombo vya habari.