Sunday, June 19, 2016

Katibu Mkuu wa Chadema Akwea Pipa Kujinoa Kisiasa Ujerumani


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji anatarajia kuhudhuria kongamano la kujadili sauti za wananchi kupitia Bunge katika maendeleo na Taifa litakalofanyika Ujerumani, Juni 20 hadi 25.

Msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene alisema jana kuwa, kongamano hilo litajadili mikakati ya kampeni na kushinda uchaguzi, hususan kwenye mazingira yenye changamoto mbalimbali za kisiasa huku pia wakijifunza umuhimu na nafasi ya Serikali za mitaa katika maendeleo ya wananchi.

“Katibu Mkuu Dk Mashinji pamoja na washiriki wengine watajadili kwa kina na kubadilishana uzoefu wa ushindani wa siasa kutoka maeneo mbalimbali, huku pia wakijifunza umuhimu wa kutumia teknolojia ya mawasiliano kupambana na changamoto za kisiasa, hasa katika nchi zinazoendelea,” alisema Makene.

Mada nyingine katika kongamano hilo zitahusu mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, kuwasaidia vijana kutambua umuhimu wa siasa na kushiriki.

Mbali na Dk Mashinji washiriki wengine watatoka nchi za Ufaransa, India, Ujerumani, Ghana, Ufilipino, Mexico, Mongolia, Argentina, Ukraine, Poland, Bolivia, Cambodia, Syria, Tunisia, Uganda, Kurdistan, Venezuela, Hoduras na Ugiriki.