Showing posts with label BUNGENI. Show all posts
Showing posts with label BUNGENI. Show all posts

Thursday, May 5, 2016

Wabunge Wagomea Utaratibu wa Kujisajili Mara Mbili....Wadai wao ni Watu wazima na Sio Wanafunzi


Wabunge wameitaka Ofisi ya Bunge iwaondolee mara moja utaratibu wa kusaini kwa kutumia vidole mara mbili kwa siku kwa kuwa wao si wanafunzi.

Hoja hiyo iliwasilishwa kwa njia ya mwongozo na kuungwa mkono na wabunge wote isipokuwa mawaziri na Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) mjini Dodoma jana.

Katika Mwongozo wake, mbunge huyo alisema kitendo cha kutakiwa kusaini mara mbili kwa siku ni kero kwa wabunge na uonevu kwa kuwa hata Bunge limekuwa likitumia muda wa mapumziko wa wabunge kwa kazi za Bunge.

“Mheshimiwa Naibu Spika wewe mwenyewe muda mfupi umetangaza matangazo mbalimbali yanayotaka baadhi ya wajumbe wa kamati wakutane baada ya saa saba mchana, tunafanya kazi nje ya mapumziko yetu, haya haina tatizo... “...tatizo langu ni kitendo cha wabunge kutakiwa kusaini mara mbili kwa siku asubuhi na jioni, wakati mwingine tunatoka hapa saa saba, wabunge tunashughulikia mambo mpaka saa 12, mbunge anatumia muda wake wa mapumziko na ule wa kuhudhuria kikao cha jioni,” alisema Haji.

Alisema inasikitisha kuona mbunge anatolewa kwenye kazi za kujenga taifa ili aje tu asaini kwa kidole tena mara ya pili.

Alisema jambo hilo linawatatiza wabunge kwa kuwa wanajiona kama wanachukuliwa kama wanafunzi kwa kufuatiliwa kwani hata kwenye benki wafanyakazi hawasaini na kufuatiliwa kama ilivyo kwa wabunge hao.

Alifafanua kuwa kabla ya kuomba Mwongozo huo, alifanya utafiti kwenye benki mbalimbali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambao nao wana utaratibu kama huo wa Bunge lakini hakuna mahali wanapotakiwa kusaini kwa vidole mara mbili.

“Kutokana na uzito wa jambo hili naomba kutoa hoja wabunge mniunge mkono mpango huu ukome,” alisema na wabunge takribani wote walisimama ishara ya kumuunga mkono na kumpigia makofi na vigelegele.

Kwa upande wake, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema kutokana na namna wabunge hao walivyopokea suala hilo, pamoja na kwamba kikanuni jambo hilo halikutakiwa kuombewa mwongozo bado litaangaliwa.

“Hata hivyo, nifafanue kuwa kusaini mara mbili lengo lake si kuwafanya wabunge wanafunzi, ila lengo ni kutaka kujua nani wapo humu ndani (bungeni),” alisema Dk Ackson.

Naibu Spika Azima Mjadala Bungeni wa Kupanda Kwa Sukari

Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amezima hoja ya Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) aliyeomba suala la kupanda bei ya sukari lijadiliwe bungeni.

Wakati hayo yakitokea wananchi wa Mkoa wa Mbeya wameviomba vyombo vya dola kupekua malori yanayotokea Malawi, kwa madai yanabeba sukari ya magendo na kuingiza nchini.

Akitumia kifungu cha Kanuni za Bunge cha 47(1, 2, 3), mbunge huyo alisema bungeni mjini hapa jana, kuwa suala hilo ni muhimu kwa Watanzania hivyo ni vyema likajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.

Alisema tangu itangazwe utaratibu wa kusitisha sukari kuingizwa nchini kutoka nje, bidhaa hiyo imekuwa adimu na bei yake imekuwa inapanda kila siku na kusababisha maisha ya wananchi kuzidi kuwa magumu.

Hata hivyo, kabla hajamalizia kuzungumza, Dk Ackson alimkatiza Bashe, akisema suala hilo lilishafanyiwa kazi Alhamisi wiki iliyopita, wakati wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

“Mtakumbuka Waziri Mkuu Alhamisi ya wiki iliyopita, alitoa maelezo na akatoa maelekezo kuwa sukari itaruhusiwa kuingizwa nchini kwa kiasi ambacho alitaja,”alisema.

Alisema pamoja na udharura wake kwasababu ilishatolewa maelekezo, wabunge wasubiri yale maagizo ya Waziri Mkuu kuuliza kama sukari imeingia ama haijaingia na kama hajaingia lini inaingia.

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu akijibu hoja iliyoibuliwa bungeni hapo inayohusu pia bei ya sukari, Waziri Mkuu alisema serikali imeruhusu kiasi kidogo cha sukari kuingizwa nchini ili kupunguza tatizo la upungufu wa bidhaa hiyo.

Kwa mujibu wa Majaliwa, Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani 300,000 za sukari kwa mwaka wakati nchi inahitaji tani 420,000 hivyo kuwepo na upungufu wa tani 120,000.

Aidha, mapema mwezi uliopita, serikali ilitangaza kuwa bei elekezi ya sukari itakuwa Sh 1,800 kwa kilo, lakini hali katika maeneo mbalimbali nchini ni tofauti, kwani bidhaa hiyo muhimu inauzwa kwa bei ya juu.

Katika maeneo mbalimbali ukiwamo Mkoa wa Dar es Salaam, sukari inauzwa kuanzia Sh 2,200 hadi Sh 2,500 kwa kilo.

Baadhi ya wafanyabiashara nchini wameamua kufanya njama za kuficha bidhaa hiyo ili kuonekana kuwa kuna uhaba ili waruhusiwe kuagiza kutoka nje, jambo ambalo limekwishakataliwa na Rais John Magufuli.

Wiki iliyopita, mkoani Singida, wananchi walisaidia kukamatwa kwa mifuko 655 ya sukari sawa na tani 24.3, na kutiwa nguvuni wafanyabiashara wawili pia wakihusishwa na bidhaa hiyo ambayo ilifichwa stoo.

Waliokamatwa ni Mohamed Alute Ally (44) mfanyabiashara wa Unyankindi aliyekutwa na mifuko 335 ya kilo 25 kila mmoja na Yusufu Suleiman (39) mfanyabiashara wa Minga aliyepatikana na mifuko 320 ya kilo 50.

Taarifa ya kukamatwa kwa sukari hiyo na wafanyabiashara hao ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, Saidi Amanzi.

Taarifa zilieleza kuwa mfuko mmoja wa sukari ambao huuzwa kwa Sh 92,650 sasa unauzwa kati ya Sh 115,000 na Sh 120,000 huku kilo moja ikiuzwa kati ya Sh 2,400 na 2,800 kwa kilo kinyume cha bei elekezi ya Sh 1,800.

Kutoka Mbeya, wananchi jijini hapa wamevitaka vyombo vya dola kuyapekua malori yanayotokea nchi jirani ya Malawi, kwa kile walichodai yanabeba sukari ya magendo na kuingiza nchini.

Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao, walisema hivi karibuni kuna malori manane ya kampuni moja  yalibeba shehena ya sukari yakitokea Malawi na yaliegesha kwenye moja ya kituo cha mafuta cha Uyole kwa lengo la kutafuta wateja.

Mkazi mwingine wa Mtaa wa Soweto, Hamphrey Lyoto alisema suala la uingizwaji wa sukari, linafanywa mchana ambapo malori yanapeleka sukari kwenye nyumba ya mfanyabiashara mmoja eneo hilo aliyejiwekea kiwanda cha kuweka sukari kwenye mifuko ya kilo moja moja na nusu kilo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Emmanuel Lukula alipoulizwa juu la suala hilo, alisema hafahamu lolote kwa kuwa ameanza kazi hivi karibuni, lakini aliahidi kulifutalia.

Wanaodai bunge kuonyeshwa live watakiwa kuomba kwa utulivu

Katibu Mkuu wa National Reconstruction Alliance (NRA), Hassan Kisabya Almas amewataka  Watanzania wanaoomba Bunge  la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuonyeshwa  kupitia matangazo ya moja kwa moja (Live) kuomba  kwa utaratibu bila kuharibu amani ya Tanzania.

Aidha Katibu Mkuu wa Chama hicho, amesema  kwamba   amani iliyoko ni hazina kubwa ambayo nchi nyingine inatamani kuwa nayo.

Almas aliyasema hayo jana alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO).

“Leo hii tupo tunaopigania kutaka kuona Bunge Live, lakini yote haya ni kwa kuwa Tanzania amani tunayo, sidhani kama nchi kama Afghastan siku watakayoamua kuonyesha Bunge Live kwa mwaka mzima, kwa saa 24 kama wataweza kukaa kuangalia Bunge hilo, hivyo basi wale wanaotaka hayo, kwanza tudumishe amani  yetu,” alisema Almas.

Almas alieleza kuwa, amani ya Tanzania ni zaidi ya dhahabu ambayo Tanzania inajivunia hivyo ni lazima Watanzania kuitunza na kuithamini amani ambayo ipo kwa sasa na kuacha kuchochea mambo ambayo yanaweza kuleta machafuko katika nchi na amani ambayo leo haithaminiwi ikaja kukumbukwa siku moja.

Pia, alisema yeye ni mmojawapo wa watu wanaopenda kuona Bunge Live lakini jambo hilo halishadadii kama inavyofanywa na watu wengine kwani anajua kwa kufanya hivyo anaweza kuhatarisha Amani ya Tanzania na hata hilo Bunge halitaweza kuliona tena kutokana na kutokuwa na Amani ndani ya nchi.

Vilevile, amewataka waandishi wa habari kuandika yale yaliyo mazuri ya nchi kuliko mabaya machache ili kuzidi kuitangaza Tanzania vyema kimataifa, kwani sio uzalendo kuona mambo yote mabaya yanakuwa ukurasa wa kwanza, bali kwanza yarekebishwe kwakuwa ni makosa yanayoweza kurekebishwa. Kalamu za waandishi wa habari ni chachu ya amani na maendeleo ya Taifa la Tanzania.

Sunday, May 1, 2016

Serikali Yaiagiza Mamlaka Ya Bandari Na TRA Kubaini Chanzo Cha Kupungua Kwa Shehena Ya Kontena Zinazoingia Nchini


SERIKALI imeziagiza Mamlaka ya Bandari-TPA, na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kufanya uchambuzi wa kina ili kubaini sababu za kupungua kwa shehena ya kontena zinazoingia nchini kupitia Bandari ya Dar es salaam kwenda nchi jirani.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dokta Philip Mpango, ameliambia Bunge mjini Dodoma, jana tarehe 30, Machi, 2016 kwamba taarifa zilizopo zinaonesha kwamba uingiaji wa mizigo inayopelekwa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, Malawi na Zambia kupitia bandari hiyo, umeshuka.

Alisema katika kipindi cha mwezi Oktoba mwaka jana na Machi mwaka huu kontena zilizopelekwa nchini Congo zilishuka kutoka 5,529 hadi 4,092, wakati yale yaliyokuwa yakipelekwa nchini Malawi yalishuka kutoka kontena 337 hadi 265, huku yale ya Zambia yakishuka kutoka 6,859 hadi kufikia 4,448.

Hata hivyo, Dokta Mpango aliwahakikishia waheshimiwa wabunge kwamba kushuka kwa kiwango cha kontena ziendazo nchi jirani kupitia  Bandari ya Dar es salaam, hakujaathiri malengo ya ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Alisema sababu mojawapo ya kushuka kwa idadi ya kontena zinazopitia bandari ya Dar es slaam zinachangiwa na kuporomoka kwa uchumi wa China ambao umeathiri nchi mbalimbali duniani ikiwemo  Tanzania.

"Lakini naziagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania-TPA na Mamlaka ya Mapato-TRA, zichambue mwenendo huo ikilinganishwa  na nchi nyingine" alisisitiza Dokta Mpango.

Alilieleza Bunge pia kwamba, Tanzania haitozi kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kontena zinazosafirishwa kutoka bandari hiyo kwenda nchi jirani hivyo hiyo haiwezi kuwa sababu ya kuzikwaza nchi jirani kutumia bandari ya Dar es salaam

Wabunge wa CCM Wakataa Bunge Kuonyeshwa LIVE.......Wapinzani Waamua Kujirekodi Kwa Simu Zao


Wabunge wa CCM jana waliibuka kidedea walipowazidi wenzao wa upinzani kwa kura za sauti “Siyooooo” kuikataa hoja ya kutaka matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja ‘live’ na televisheni. 

Hiyo ilitokea jana wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti ya Ofisi ya Rais (Tamisemi na Utumishi na Utawala Bora) na kuzua mvutano mkali uliosababisha bajeti hiyo ipitishwe kwa utaratibu wa wabunge kutohoji kitu chochote (guillotine).

Wakati hoja yao hiyo ikipingwa kila kona, tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti, wabunge hao wa upinzani sasa wamebuni mbinu mpya ya kujirekodi wenyewe wakati wakichangia mijadala mbalimbali bungeni na kurusha sauti zao kwenye mitandao ya kijamii na kupeleka sauti hizo kwenye redio zilizopo katika maeneo ya majimbo yao.

Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Salehe ndiye aliyeibua hoja hiyo akitaka kushika mshahara wa waziri kwa maelezo kuwa kuzuia Bunge kurushwa ‘live’ ni kinyume na utawala bora na haki ya kupata habari.

Hoja hiyo iliungwa mkono na  Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, Masoud Abdalla Salim (Mtambale-CUF), Rose Kamili (Viti Maalumu -Chadema), Ester Matiko (Tarime Mjini – Chadema) na Mussa Mbarouk (Tanga Mjini - CUF).

Wabunge wa CCM waliopewa nafasi na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kuchangia hoja hiyo ni Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini), Kangi Lugola (Mwibara), Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) pamoja na Waziri Ofisi ya Rais - Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki.

Ilivyokuwa  Bungeni
 Baada ya Salehe kutaka ufafanuzi wa kina huku akisisitiza kuwa uamuzi huo unakiuka Katiba ya nchi na haki ya kupata habari, Kairuki alisema kwa mujibu wa Ibara ya 18 na 100 ya Katiba zinazozungumzia uhuru wa kupata habari, uamuzi huo ni sahihi na hakuna mwananchi aliyenyimwa taarifa.

Maelezo hayo yalipingwa na Salehe, safari hii akifafanua kuwa matangazo ya Bunge yanarekodiwa kwa saa saba na kurushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) kwa saa moja tu, huku wabunge wa upinzani wakiondolewa na kuonyeshwa wa CCM pekee.

Alitaka vyombo vya habari vya elektroniki kuruhusiwa kurekodi shughuli za Bunge na kurusha maudhui wanayoyataka, badala ya kupewa video na studio ya Bunge ambayo huondoa michango na hoja za wapinzani.

Mchungaji Msigwa, Masoud Abdallah, Kamili, Matiko waliungana na Salehe na kusisitiza kuwa nchi nyingi barani Afrika zinarusha ‘live’ matangazo ya Bunge huku wakihoji sababu za TBC kurusha moja kwa moja harusi na kushindwa kuonyesha shughuli za Bunge.

Mbarouk alikwenda mbali akitaka Bunge kuanza shughuli zake usiku ili kuendana na utetezi wa Waziri wa Habari, Nape Nnauye kuwa usiku wananchi wengi wanakuwa majumbani mwao hivyo wanapata nafasi nzuri ya kufuatilia Bunge.

Matiko: Juzi Rais John Magufuli kazindua Daraja la Kigamboni, TBC ilikata matangazo ya Bunge ili kuonyesha uzinduzi huo. Yaani ya kwenu mnataka yaonyeshwe ila haya ya Bunge yasionekane. Mnakiuka demokrasia.

Ghasia: Demokrasia siyo Bunge kuonyeshwa ‘live’. Wakulima na wafugaji hawawezi kuona Bunge asubuhi ndiyo maana yanarushwa usiku. 

Serukamba: Mbona wabunge wa Chadema wanaonyeshwa katika matangazo ya TBC. Hoja kwamba maagizo ya Serikali hayatawafikia watendaji si kweli.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju alisema wapinzani hawajiamini na hawaaminiki huku akiwataka wasome ibara ya 100 ya Katiba; “Bunge kuonyeshwa au kutoonyeshwa hakuongezi kitu jimboni. Wanaozungumza ni wabunge siyo televisheni.”

Akihitimisha hoja, Kairuki alipinga maelezo ya Salehe na kutoa mfano wa nchi ambazo matangazo ya Bunge hayarushwi moja kwa moja.

Kutokana na mvutano huo Chenge aliwahoji wabunge wanaoafiki hoja ya Salehe waseme “ndiyooo”, wapinzani pekee wakasema ndiyoo, aliposema wasioafiki waseme siyo, wabunge wa CCM kutokana na wingi waliitikia kwa sauti kubwa siyoooo, na Chenge akasema anadhani wasioafiki wameshinda. 

Wapinzani  Waamua Kujirekodi kwa simu
Kwa zaidi ya mara tano,wabunge wa upinzani wameshuhudiwa wakijirekodi ndani ya ukumbi wa Bunge kwa kutumia simu zao za mkononi, wanapotoka nje huulizana kama wameshatumia video na sauti hizo katika mitandao ya kijamii.

Juzi, Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara baada ya kumaliza kuchangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais (Tamisemi na Utawala Bora) alirusha sauti yake katika mitandao ya kijamii na kusema hiyo ni moja ya njia ya kuwafanya wananchi wajue kinachoendelea bungeni.

Thursday, April 28, 2016

Wabunge MABUBU Kubanwa Bungeni......Ni Wale Wanaoshiriki Vikao vya Bunge Lakini Hawachangii Chochote


Kiti cha Spika wa Bunge kimesema ipo haja ya kufanya marekebisho ya Sheria pamoja na Kanuni ili kila mbunge apate posho kulingana na kazi aliyofanya bungeni, badala ya utaratibu wa sasa wa kuangalia mahudhurio pekee. 

Aidha, kimewataka wabunge kubadilika na kuacha tabia ya kuchukua posho za vikao vya Bunge bila kuzitolea jasho.

Kauli hiyo imekuja kutokana na Mwongozo ulioombwa Aprili 25, mwaka huu na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) ambaye alikitaka kiti cha Spika kutoa Mwongozo kuhusu usahihi wa wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kulipwa posho na mishahara wakati hawashiriki na kutimiza wajibu wao wa kuchangia kwenye mjadala wa Bunge la Bajeti linaloendelea katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la 11.

Bashe alisema mbunge huyo alitumia Kanuni ya 68(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge akiomba Mwongozo wa Spika kutokana na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuamua kutoshiriki mjadala unaoendelea bungeni, lakini wabunge hao wanasaini na kulipwa mishahara na posho.

Hivyo akaomba Mwongozo endapo ni haki kwa wabunge hao kupokea posho wakati hawashiriki wala kutimiza wajibu wao wa kisheria. 

Katika kujenga hoja hiyo, Bashe alitumia Ibara ya 63(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania isemayo, “Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti.”

Aidha, Bashe alitumia Ibara ya 73 ya Katiba ya Tanzania kufafanua kuhusu malipo ya mshahara, posho na malipo mengine kwa wabunge. 

Akitoa Mwongozo wa Spika, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Ibara ya 73 imeainisha masharti ya kazi ya wabunge.

Alisema mbunge anastahili kulipwa mshahara kwa kila mwezi, na kufafanua kuwa mbunge anapohudhuria vikao bungeni na kamati atalipwa posho ya vikao kwa kiwango kitakachowekwa na Serikali na Kanuni za Bunge. 

Alisema malipo ya mshahara ni suala la Kikatiba na Sheria hulipwa kwa mbunge kutokana na kazi yake ya ubunge.

Hivyo malipo ya posho kwa wabunge yanatokana na mahudhurio yao bungeni na siyo kwa kuchangia kama ambavyo wengi wao wanapenda iwe hivyo. 

“Kimsingi kuhudhuria bungeni pekee siyo njia inayopendeza kwa kuwa mbunge anapofika bungeni anatarajiwa atekeleze majukumu yake yalivyoainishwa katika Ibara ya 63.

“…Tabia hii ya kutochangia mijadala na kuzunguka zunguka bungeni haikubaliki na haitakiwi kuendelea, kila mbunge atekeleze wajibu wake na sio anahudhuria ili alipwe posho,” alisema Dk Ackson.

Wakati huo huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai amefanya mabadiliko katika Kamati mbalimbali za Bunge, kwa kubadilisha wabunge 16 wa Kamati za Awali kwenda nyingine. 

Aidha, Spika amewapangia Kamati wabunge wapya wanne, walioapishwa mwanzoni mwa Mkutano huu wa Bunge, ambao ni Shamsi Vuai Nahodha, Rita Kabati, Oliver Semuguruka na Lucy Owenya.

Friday, February 12, 2016

Hawa Ndo Wabunge 15 ‘Visu’

site_197_Swahili_329474
Sifael Paul na Brighton Masalu
Upande wa pili! Bunge la 11 liliahirishwa Ijumaa iliyopita ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli aliwahutubia wabunge huku Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akihitimisha hotuba kwa kuliahirisha rasmi bunge hilo hadi Januari 26, mwakani.
Hata hivyo, hiyo siyo hoja wala gumzo kuu la bunge hilo ambalo linajumuisha wabunge wengi wapya kutoka vyama mbalimbali, lakini ‘pointi’ kubwa ni jinsi wabunge 15 wanawake ambao walilitikisa bunge hilo kutokana na urembo wao na kuzua gumzo kubwa.
Wabunge hao warembo a.k.a visu ambao umri wao bado ni ‘asubuhi’, walikuwa kivutio machoni mwa baadhi ya wabunge hususan vijana ambao ‘walivunjika’ shingo juu ya wawakilishi hao.
Jiji letu linakupa orodha ya wabunge hao warembo ambapo waliojulikana kwa kukimbiza kama akina Halima Mdee wametakiwa kukaa chonjo. Hata hivyo, wabunge warembo wa kike ni wengi, lakini wafuatao ndiyo ‘shida’ kuanzia maumbo na sura zao.
magige
CATHERINE MAGIGE (CCM)

Rekodi ya urembo wake haijawahi kuvunjwa bungeni. Mara zote, tangu alipotinga bungeni mwaka 2010, amekuwa gumzo kubwa kwa uzuri wake, licha ya kushindanishwa na wabunge kadhaa, lakini bado ‘anatusua’ vilivyo.
Bonnah
Bonnah
BONNAH KALUWA (CCM)
Hii ni mara yake ya kwanza kuingia bungeni. Uzuri na urembo wake umeonekana gumzo bungeni tangu mwanzo hadi mwisho wa kikao hicho. Sura, umbo na macho yake vimekuwa kivutio kikubwa.
kairuki

kairuki
ANGELLA KAIRUKI (CCM)
Ukimwangalia vibaya, unaweza kusema ni shombeshombe. Urembo wa sura yake, umekuwa ukiwapa nyakati ngumu watu wengi, wakati mwingine kushindwa hata kung’amua kama ana asili ya Kiarabu au la! Kinachomuongezea sifa katika kilinge cha urembo ni umbo lake lililojengeka.
ESTER MATIKO
ESTER MATIKO (CHADEMA)
Achana na ukali wa hoja zake anapochangia mijadala. Hiki ni ‘kisu’ kikali kinachovutia bungeni. Umbo lake la ‘kitoto’, uzuri wa sura na macho ya mviringo, vinamfanya aonekane mrembo na mwenye uzuri wa kupindukia.
bukwimba
LOLESIA BUKWIMBA (CCM)
Tabasamu lake ndiyo limekuwa gumzo. Sura yenye uchangamfu imekuwa ikiteka macho ya watu wengi. Kamwe huwezi kuchoka kumtazama mwakilishi huyo. Mpole kama alivyo, lakini amekuwa ‘akikimbiza’ vilivyo mjengoni.
DK MARRY MWANJELWA (CCM)
Licha ya umri kuanza kumpigia honi lakini anawafunika wabunge wengi wenye umri mdogo. Urefu na figa nzuri, vinachangia kwa kiasi kikubwa kumweka kwenye orodha ya wabunge wa kike wanaotikisa kwa uzuri.
UMMY MWALIMU (CCM)
Hana makuu. Mpole na mwenye aibu wakati wote, lakini urembo wake unashereheshwa na umbo lake matata. Ana urembo wa haja unaoyapa macho kazi ya ziada kuitafuta kasoro yake.
CECILIA PARESSO (CHADEMA)
Urembo, uzuri wa umbo lake, urefu, unene wa wastani na sura nzuri vinatosha kumuingiza kwenye orodha hii.
shonza
JULIANA SHONZA (CCM)
Umbo lake ni la kawaida, lakini shughuli iko usoni. Achana na sehemu zingine za mwili, ukimtazama usoni tu utagundua ni kisu.
lucy
LUCY MAYENGA (CCM)
Ni mrembo wa umbo na sura. Hahitaji maneno mengi kumwelezea, lakini ukweli unabaki palepale kuwa ni miongoni mwa wabunge warembo walioupa shida Mji wa Dodoma.
Mboni-Mhita
MBONI MHITA (CCM)
Akiwa umbali kidogo kutoka mahali ulipo, unaweza kumchukulia kawaida! Shughuli ipo akikusogelea. Umbo na uzuri wake ni habari nyingine.
NEEMA MGAYA (CCM)
Rangi yake ya asili, ngozi laini, umbo namba nane na ucheshi wake, vinamtetea kuingia kwenye ulingo wa wabunge hawa warembo zaidi.
VICKY KAMATA (CCM)
Silaha kubwa aliyonayo ni midomo na macho! Geuza gazeti nyuma, mtazame tena Vicky, unaona? Si umbo, si sura, si macho, si mdomo, Vicky Kamata ni mrembo. Inatosha kusema hivyo tu.
JESCA KISHOA (CHADEMA)
Ni mrembo anayevutia kwenye viunga vya bungeni na inawezekana ndiyo maana aliyekuwa Mbunge wa NCCR-Mageuzi, David Kafulila aliamua kuchukua jumla na kumweka ndani.
bulaya
ESTER BULAYA (CHADEMA)
Kama unahitaji kumpongeza muumba kwa kazi njema, wewe mtazame Ester Bulaya, si mrefu, si mfupi, si mweusi wala si mweupe. Yuko kati kwa kati. Akitembea, kama ni barabarani, jihadhari na vyombo vingine vya usafiri.

Wednesday, February 3, 2016

HALIMA MDEE: HII BIASHARA YA KUFANYA RAIS ASHIKIKI WALA HATAJWI ‘IKOME’

Halima mdee
Mbunge wa Kawe jijini Dar es Salaam, Halima James Mdee, jana amezua mjadala bungeni baada ya kuweka wazi kuwa anakerwa na kitendo kinachotajwa na baadhi ya Wabunge kwamba Rais hatajwi wala haguswi na hoja.
Akichangia Bungeni jana, Mdee alidai wakati Rais Magufuli alipokuwa waziri wa Ujenzi walipanga kukarabati barabara ya kilometa 5004 lakini zikakarabatiwa 2700 pekee.
Wabunge wa CCM walicharuka wakimtaka Halima, kutotumia wala kumtaja Rais kwa Dhihaka kwa kuwa kanuni za Bunge haziruhusu.
“Kwa mujibu wa kanuni ya 64 fasili ya kwanza, Mbunge hatotumia kwa dhihaka jina la Rais katika mjadala, Mbunge anayeendelea anatumia jina la Rais kwa Dhihaka naomba aendelee bila kumtaja” Alisikika Mbunge mmoja wa chama cha Mapinduzi.
Mbunge huyo kijana wa CHADEMA, alijibu hoja hiyo kwa kusema jukumu la Bunge ni kuirekebisha Serikali hivyo yuko sawa kumtaja.
“Nasema hivi hii biashara ya kufanya rais ni mtu ambae hashikiki wala hatajwi wala haguswi iachwe, kwa sababu jukumu la Bunge ni kuirekebisha na kushauri Serikali” Alisema.

AUDIO: MNYUKANO WA HALIMA MDEE NA DK. MWAKYEMBE BUNGENI JANA FEBR 2 KUHUSU SAKATA LA MABEHEWA MABOVU

Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe na Mbunge wa jimbo la Kawe, Halima Mdee (Chadema), jana waliingia kwenye mvutano mkali huku wakitunishiana misuli ya sheria kuhusu kashfa ya ununuzi wa mabehewa 274 yanayodaiwa kuwa mabovu. Ununuzi huo uliofanywa wakati Dk. Mwakyembe alipokuwa Waziri wa Uchukuzi.

Mdee aliibua tena suala la kashfa ya ununuzi wa mabehewa hayo 274 akisisitiza kuwa ni mabovu, wakati alipopata nafasi ya kuchangia katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2011/- 2015/16 ambapo aligusia ahadi ya serikali ya kukarabati reli ya kati  ambayo alidai haijatekelezwa ipasavyo.

Dk. Mwakyembe alikanusha taarifa ya kuwepo kwa mabehewa mabovu kati ya mabehewa hayo 274 yaliyonunuliwa wakati akiwa Waziri wa Uchukuzi.

 “Leo nikimwambia Halima aniletee mabehewa ambayo hayafanyi kazi atashindwa kunionesha,” alisema  Mwakembe

Waziri huyo alieleza kuwa mkataba wa ununuzi wa mabehewa hayo ulitoa mwanya wa kufanya ukarabati au marekebisho katika bidhaa husika ndani ya muda fulani, kipengele kinachojulikana kama ‘defect liability period’. 

Hivyo, alitumia kipengele hicho kufanyia marekebisho mabehewa hayo ambayo alikiri hayakuwa mazuri yalipowasilishwa.

“Mabehewa yote yanafanya kazi kwa sababu yalipoletwa ni mimi mwenyewe nilisema kuna mabehewa ambayo sio mazuri. Nikaunda uchunguzi, kwa sababu tulikuwa na haki chini ya mkataba (defects liability period), ilikuwa ndani ya mwaka mmoja, wakaja wale walioutuuzia mabehewa wakayatengeneza. Sasa yako wapi hayo mabovu?” alieleza Mwakyembe.

Juzi, Mwakyembe alieleza kuwa yuko tayari kujiuzulu ubunge wake kama itabainika kuwa madai ya kashfa hiyo ni ya kweli.

 Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walitaka ripoti ya uchunguzi wa ununuzi wa mabehewa hayo iwasilishwe bungeni huku wakisisitiza kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria ya ununuzi iliyopelekea ununuzi wa mabehewa mabovu.

===> Sikiliza Hapo Mnyukano ulivyokuwa Bungeni


Tuesday, February 2, 2016

AFANDE SELE AUNGANA NA MBUNGE JOSEPH MSUKUMA KUITAKA SERIKALI IHALALISHE MATUMIZI YA BHANGI


Msanii mkongwe wa hip hop nchini, Afande Sele amefunguka na kusema serikali ihalalishe matumizi ya bangi na si kukosoa juu ya hoja iliyotolewa na mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma.

Ikiwa imepita siku moja toka mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM), kusema haoni sababu ya serikali kuzuia bangi kuwa zao la biashara kwa maana haoni madhara yake huku akidai kwamba viroba vina madhara zaidi kuliko bangi, Afande Sele amefunguka na kusema serikali ihalalishe matumizi ya bangi na si kukosoa juu ya hoja hiyo ya Joseph Msukuma.

Afande Sele amedai kuwa kuna nchi ambazo tayari wao wamehalalisha matumizi ya bangi na kuthibitisha kuwa pombe ina madhara makubwa zaidi kuliko bangi.

"Legalize it, Don't criticize it. Korea Kaskazini, Marekani, Mexico Uruguay na mataifa mengine ya Ulaya yamethibitisha pombe ina madhara kuliko Cannabis Sativa" Amesema Afande Sele.

MKE WA KAFULILA AMLIPUA DR. MWAKYEMBE KUHUSU SAKATA LA MABEHEWA FEKI..MWAKYEMBE AKOMAA, ASEMA YUPO TAYARI KUJIUZULU IKITHIBITIKA

Sakata la ununuzi wa mabehewa kwa ajili ya Shirika la Reli Tanzania (TRL) yanayodaiwa kuwa mabovu liliibuka jana Bungeni na kumuinua Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi katika serikali ya awamu ya nne.

Waziri Mwakyembe alikanusha madai yaliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Jesca Kishoa kuwa ununuzi huo wa mabehewa mabovu uliisababishia sherikali hasara ya shilingi bilioni 238, huku akitaka ripoti ya ukaguzi wa ununuzi huo iwasilishwe bungeni.

Akitumia kanuni ya 63 (3) kuomba kutoa taarifa, Mwakyembe alikanusha kiwango cha fedha kilichotajwa na mbunge huyo wa viti maalum ambaye ni mke wa aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.

“Mbunge aliyesimama kabla, aliyejitambulisha kama mke wa Kafulila, ameeleza kwamba serikali ilitumia zaidi ya shilingi bilioni 238 na kuleta hasara kwa kununua mabehewa mabovu. Mheshimiwa Mwenyekiti nataka kukuthibitishia kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kwa kununua mabehewa 274 haijawahi kutumia zaidi ya shilingi bilioni 60,”alisema Mwakyembe.

Waziri huyo alienda mbali na kueleza kuwa endapo mbunge huyo atawasilisha uthibitisho wa kiwango hicho cha fedha kutumika kununua mabehewa hayo, atajiuzulu nafasi yake ya ubunge.

“Mimi naomba athibitishe hiyo shilingi bilioni 238. Na nitashukuru sana kama akileta hapa. Na akileta hiyo, mimi nitajiuzulu hata ubunge,”alisema Mwakyembe.

Baada ya kauli hiyo ya Mwakyembe, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee naye alisimama na kueleza kuwa Waziri huyo hakutumia kifungu sahihi kutoa taarifa kwa kuwa alipaswa kutumia kifungu cha 63 (4) kutoa ushahidi wa kukanusha kwake kwanza.

Naye Kishoa aliendelea kusisitiza kuwa Serikali inapaswa kuwasilisha bungeni hapo ripoti ya ukaguzi wa manunuzi ya mabehewa hayo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge, Dk. Mary Mwanjelwa alitoa siku tatu kwa mbunge huyo wa viti maalum kuwasilisha ushahidi kuhusu madai yake.

Thursday, January 28, 2016

Siasa Haina Adui wa Kudumu Kama Wengi Wanavyodhani.....Watazame Mbowe na Zitto Kabwe Wakicheka na Kufurahi Pamoja

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (kulia) akipeana mkono na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kabla ya kuanza kwa mkutano na waandishi wa habari wakipinga kitendo cha kutolewa kwa nguvu katika Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma jana. 

March 10 2015, Zitto Kabwe alivuliwa uanachama wa CHADEMA  kwa tuhuma za kukihujumu na kikisaliti chama hicho.

Hata hivyo, baada ya muda mfupi, Zitto alijiunga na chama cha ACT-Wazalendo na kuteuliwa kuwa kiongozi mkuu wa chama hicho huku mwenyekiti wake akiwa Anna Mghwira