Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amezima hoja ya Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) aliyeomba suala la kupanda bei ya sukari lijadiliwe bungeni.
Wakati hayo yakitokea wananchi wa Mkoa wa Mbeya wameviomba vyombo vya dola kupekua malori yanayotokea Malawi, kwa madai yanabeba sukari ya magendo na kuingiza nchini.
Akitumia kifungu cha Kanuni za Bunge cha 47(1, 2, 3), mbunge huyo alisema bungeni mjini hapa jana, kuwa suala hilo ni muhimu kwa Watanzania hivyo ni vyema likajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
Alisema tangu itangazwe utaratibu wa kusitisha sukari kuingizwa nchini kutoka nje, bidhaa hiyo imekuwa adimu na bei yake imekuwa inapanda kila siku na kusababisha maisha ya wananchi kuzidi kuwa magumu.
Hata hivyo, kabla hajamalizia kuzungumza, Dk Ackson alimkatiza Bashe, akisema suala hilo lilishafanyiwa kazi Alhamisi wiki iliyopita, wakati wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
“Mtakumbuka Waziri Mkuu Alhamisi ya wiki iliyopita, alitoa maelezo na akatoa maelekezo kuwa sukari itaruhusiwa kuingizwa nchini kwa kiasi ambacho alitaja,”alisema.
Alisema pamoja na udharura wake kwasababu ilishatolewa maelekezo, wabunge wasubiri yale maagizo ya Waziri Mkuu kuuliza kama sukari imeingia ama haijaingia na kama hajaingia lini inaingia.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu akijibu hoja iliyoibuliwa bungeni hapo inayohusu pia bei ya sukari, Waziri Mkuu alisema serikali imeruhusu kiasi kidogo cha sukari kuingizwa nchini ili kupunguza tatizo la upungufu wa bidhaa hiyo.
Kwa mujibu wa Majaliwa, Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani 300,000 za sukari kwa mwaka wakati nchi inahitaji tani 420,000 hivyo kuwepo na upungufu wa tani 120,000.
Aidha, mapema mwezi uliopita, serikali ilitangaza kuwa bei elekezi ya sukari itakuwa Sh 1,800 kwa kilo, lakini hali katika maeneo mbalimbali nchini ni tofauti, kwani bidhaa hiyo muhimu inauzwa kwa bei ya juu.
Katika maeneo mbalimbali ukiwamo Mkoa wa Dar es Salaam, sukari inauzwa kuanzia Sh 2,200 hadi Sh 2,500 kwa kilo.
Baadhi ya wafanyabiashara nchini wameamua kufanya njama za kuficha bidhaa hiyo ili kuonekana kuwa kuna uhaba ili waruhusiwe kuagiza kutoka nje, jambo ambalo limekwishakataliwa na Rais John Magufuli.
Wiki iliyopita, mkoani Singida, wananchi walisaidia kukamatwa kwa mifuko 655 ya sukari sawa na tani 24.3, na kutiwa nguvuni wafanyabiashara wawili pia wakihusishwa na bidhaa hiyo ambayo ilifichwa stoo.
Waliokamatwa ni Mohamed Alute Ally (44) mfanyabiashara wa Unyankindi aliyekutwa na mifuko 335 ya kilo 25 kila mmoja na Yusufu Suleiman (39) mfanyabiashara wa Minga aliyepatikana na mifuko 320 ya kilo 50.
Taarifa ya kukamatwa kwa sukari hiyo na wafanyabiashara hao ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, Saidi Amanzi.
Taarifa zilieleza kuwa mfuko mmoja wa sukari ambao huuzwa kwa Sh 92,650 sasa unauzwa kati ya Sh 115,000 na Sh 120,000 huku kilo moja ikiuzwa kati ya Sh 2,400 na 2,800 kwa kilo kinyume cha bei elekezi ya Sh 1,800.
Kutoka Mbeya, wananchi jijini hapa wamevitaka vyombo vya dola kuyapekua malori yanayotokea nchi jirani ya Malawi, kwa kile walichodai yanabeba sukari ya magendo na kuingiza nchini.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao, walisema hivi karibuni kuna malori manane ya kampuni moja yalibeba shehena ya sukari yakitokea Malawi na yaliegesha kwenye moja ya kituo cha mafuta cha Uyole kwa lengo la kutafuta wateja.
Mkazi mwingine wa Mtaa wa Soweto, Hamphrey Lyoto alisema suala la uingizwaji wa sukari, linafanywa mchana ambapo malori yanapeleka sukari kwenye nyumba ya mfanyabiashara mmoja eneo hilo aliyejiwekea kiwanda cha kuweka sukari kwenye mifuko ya kilo moja moja na nusu kilo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Emmanuel Lukula alipoulizwa juu la suala hilo, alisema hafahamu lolote kwa kuwa ameanza kazi hivi karibuni, lakini aliahidi kulifutalia.