Showing posts with label KITAIFA. Show all posts
Showing posts with label KITAIFA. Show all posts

Sunday, June 19, 2016

Makachero Watumwa Mwanza na Arusha Kuchunguza Mauaji ya dada wa bilionea Msuya

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam limetuma timu ya maofisa wake kwenda mikoa ya Arusha na Mwanza kufanya upelelezi wa mauaji ya dada wa bilionea Erasto Msuya, Aneth Msuya.

Hadi sasa jeshi hilo limewakamata watu wanne kwa tuhuma za mauaji hayo, akiwamo mumewe Aneth, mfanyakazi wao wa ndani na hawara wa mfanyakazi huyo.

Kamanda Sirro hakumtaja mtuhumiwa wa nne aliyekamatwa kwa tuhuma za mauaji hayo yaliyogusa hisia za watu.

Aneth aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojuliana Mei 26 mwaka huu, nyumbani kwake Kibada Kigamboni jijini Dar es Salaam, ambao inadaiwa hawakuchukua kitu chochote ndani na kutoweka.

Sirro alisema alituma maofisa hao kwenda Mwanza na Arusha kufanya upelelezi wa mauaji ya Aneth ili kubaini chanzo chake.

Hata hivyo, hakutaka kufafanua zaidi sababu za kutuma timu hiyo kwenye mikoa hiyo wakati mauaji hayo yalifanyika jijini Dar es Salaam.

“Jeshi la polisi bado tunafuatilia, kwa sasa tumeshatuma maofisa wetu wameenda katika mkoa wa Mwanza na Arusha ili kufanya upelelezi zaidi,”alisema Sirro.

Alisema jeshi hilo linaendelea kuwahoji watuhumiwa wanaowashikilia ili kubaini chanzo cha mauaji hayo, hivyo upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.

Bilionea Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi zaidi ya 12 na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi kandokando ya barabara eneo la Mojohoroni wilayani Hai Mkoa wa Kilimanjaro.

Februari 10, mawakili wanaosimamia kesi ya bilionea huyo, Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emmanuel Safari na John Lundu, waliiambia mahakama kuwa Serikali inakusudia kuita mashahidi 50 kuthibitisha mashtaka na kuwasilisha vielelezo 40, ikiwamo bunduki iliyotumika katika mauaji hayo.

Mawakili hao walidai mipango ya kumuua bilionea Msuya ilianza Julai 26, mwaka 2013 jijini Arusha, ikiwahusisha washtakiwa hao baada ya kuahidiwa wangelipwa Sh5 milioni kila mmoja.

Makonda Kupiga Marufuku Uvutaji Sigara Hadharani

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema waendesha bodaboda na abiria wasiovaa helmet watakamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kutaka kujiua.

Makonda aliyemwakilisha Makamu wa Rais kwenye futari iliyoandaliwa na Benki ya NMB kwa wateja na wadau wake juzi, alisema abiria na wapanda vyombo hivyo wanatakiwa kuvaa helmet.

Alisema kupanda pikipiki bila usalama ni kwamba abiria anadhamiria kujiua, kwa sababu akipata ajali ni rahisi kupoteza maisha kwa kupiga kichwa chini.

“Nimeshawasiliana na kamati yangu ya usalama barabarani mkoa, hili nitalisimamia kikamilifu lazima wote wawe na helmet na wakikamatwa wote watashtakiwa,” alisema.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kupanda bodaboda bila kuvaa kofia hiyo, ni sawa na mtu anayechukua vidonge na kunywa na pombe kali, ambayo matokeo yake ni kifo.

Makonda alisema kazi hiyo ataifanya kipindi hiki cha Mfungo wa Ramadhani ili apate thawabu ikiwamo kuruhusu maduka makubwa kufanya kazi hadi usiku wa manane.

Alisema hiyo itasaidia wanaofanya kazi wakirudi nyumbani wanafuturu baadaye wanaswali Tarawehe, hivyo wanaweza kwenda kufanya manunuzi usiku.

Alisema kitakachofanyika ni kuimarisha usalama wa raia kupitia kamati yake ya ulinzi na usalama ya mkoa.

Pia, alisema atatangaza kupiga marufuku uvutaji sigara hadharani zaidi kwenye mikusanyiko na kupambana na vijana na watu wanaojihusisha na uvutaji wa shisha (bangi).

“Mtu asiyevuta sigara, anakerwa sana na moshi ndiye anayeathirika zaidi, nitatangaza rasmi hivi karibuni marufuku ya kuvuta sigara, sasa watu watafute kwa kuvutia… nitatangaza na hatua za kuchukua,” alisema.

Makonda alitumia nafasi hiyo kuwataka NMB kuchangia madawati, kwa shule za msingi na sekondari katika mkoa wake.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker alisema utamaduni wa kufuturu pamoja hasa katika Afrika unadumisha amani, umoja na upendo miongoni mwa Waislamu na watu wengine, hivyo wao wanauendeleza.

Baada ya TCRA Kuzima Simu Feki, Wafanyabiashara Wamepata Soko Jipya la Simu Hizo


Moja ya habari iliyoripotiwa ni hii kutoka gazeti la Mwananchi, yenye kichwa cha habari ‘simu bandia zapata soko Msumbiji, Congo’.

Gazeti hilo limeripoti kuwa Siku mbili baada ya mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzima simu feki, wafanyabiashara wa simu hizo wamepata soko jipya katika nchi za Msumbiji na Congo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hilo, baadhi ya vijana waliokutwa wakizunguka madukani kuzikusanya, walisema wanazinunua na kuzisafirisha kwenda huko kwa ajili ya kuziuza kwa watumiaji. Walisema katika nchi hizo kuna soko kwa sababu zinakamata mawasiliano kama kawaida.

Gazeti hilo limemnukuu Lawrence Kyondo ambapo amesema wanazinunua kwa bei ya makubaliano na kwenda kuziuza katika soko la nje……….>>>’hatujaanza hii biashara leo, siku nyingi isipokuwa wenye maduka walikuwa bado wagumu kuziuza wakidhani hazitazimwa’

Magazeti ya Leo Jumapili ya June 19



Lowassa Atoboa Siri Ya Ujio wa TB Joshua Nchini.....Asema Aliitwa na CCM Kumshawishi Akubali Matokeo ya Uchaguzi Mkuu


Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa amesema hakuridhika na matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, na kwa kulijua hilo, ‘watawala’ walimleta rafiki yake kutoka Nigeria, TB Joshua ili amshawishi akubali matokeo. 

Lowassa alisema baada ya TB Joshua, muhubiri na kiongozi wa Synagogie Church of All Nations, kukaa naye pamoja na viongozi wengine wa Chadema na kumueleza jinsi ‘walivyoporwa’ ushindi, kiongozi huyo wa kidini alichukia na kusitisha azma yake ya kuhudhuria sherehe za kumuapisha Rais John Magufuli.

TB Joshua aliwasili nchini Novemba 3, siku mbili kabla ya kuapishwa kwa Magufuli kuwa Rais, na alienda Ikulu na baadaye nyumbani kwa Lowassa ambaye alitumia muda mwingi wa ziara yake pamoja naye. 

“Walimuita rafiki yangu TB Joshua, wakaenda wakampokea. Alipokelewa na Rais Magufuli, akapelekwa Ikulu akazungumza na Kikwete,” alisema Lowassa. 

“Baadaye akawaambia wamlete kwangu. Kweli akaja nyumbani kwangu, tukazungumza naye. Sitaki kusema mengi sana niliyomwambia, lakini moja, nilimwambia ukikubali yale matokeo ndugu yangu, heshima yako itashuka hapa nchini na duniani kwa ujumla,”alisema. 

Lowassa alisema hayo jana alipokuwa akizungumza katika mahafali ya Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Wafuasi wa Chadema (Chaso) katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam. 

Alisema ni kutokana na msimamo na mazungumzo waliyofanya na TB Joshua ndio yaliyosababisha kiongozi huyo wa kidini maarufu barani Afrika kutohudhuria sherehe hizo za kuapishwa zilizofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

Katika hotuba yake, Lowassa alimpongeza Rais Magufuli kwa jitihada anazozichukua za kujaribu kufufua uchumi wa nchi, lakini akasema hakubaliani na mbinu anazotumia. 

Alisema anafurahia kumsikia Rais Magufuli akiihubiri nchi ya viwanda, lakini hana imani na lugha anazotumia.

“Rafiki zangu nawasikia na nafurahi sana wanasema wanataka kujenga nchi ya viwanda. Natamani nchi hiyo, lakini lugha hiyo sina imani nayo sana,” alisema. 

Alisema haziamini lugha hizo kwa kuwa ni vitu visivyowezekana kutokana na ukweli kuwa viwanda vilivyopo haviwezi kufufuka na kuondoa tatizo la ajira lililopo nchini. 

“Wanasema watafufua viwanda, lakini viwanda vilivyopo vili kuwa analojia sasa hivi mambo yote ni ‘digital’. Hicho kiwanda kitafufuliwaje maana hata madukani spea zake hazipo labda zitengenezwe upya,”alisema. 

Alisema tatizo lililopo kwa sasa nchini ni la ajira na kwamba hata kaulimbiu yao kwenye kampeni ilikuwa ajira kwa kutambua kuwa wapo vijana wengi waliomaliza vyuo, hawana ajira na kwamba eneo kubwa litakaloweza kuwaajiri ni sekta ya kilimo. 

Lowassa, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, alisema anakubaliana na kauli iliyotolewa na Jenerali Ulimwengu aliyoitoa hivi karibuni kuwa Rais Magufuli ameturudisha nyuma miaka 50, akiponda uamuzi wa Serikali kuzuia matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja. 

“Uamuzi ule si mzuri na una matatizo makubwa kwa kuwa ni kuwanyima wananchi haki yao muhimu ya kuwasikiliza wawakilishi wao,” alisema.

Akizungumzia elimu, Lowassa alisema wakati Chadema na Ukawa waliposema watatoa elimu bure kuanzia chekechea mpaka chuo kikuu walikuwa wamejipanga, lakini Serikali imebeba sera hiyo bila kujiandaa.

Aliwapongeza vijana kwa kuwa kiini cha mabadiliko na kusema mpaka sasa akikutana na watoto wadogo wanamsalimia kwa kumwambia “Mabadiliko Lowassa”. 

Alisema vijana walifanya kampeni nzuri na kumwezesha kupata kura nyingi zilizowapa ushindi, lakini wakanyimwa ushindi. 

“Tulishinda vizuri sana lakini hata hizo walizotupa, zinatosha kuwaambia kuwa tuliwapa kazi ya kutosha. Nyie mnajua, wao wanajua na mimi najua,” alisema. 

Lubuva aondolewe 
Alisema licha ya kumuheshimu mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, anapaswa kutimuliwa kwa kushindwa kuisimamia vyema tume hiyo. 

“Tume ya Uchaguzi inapaswa iondoke. It must go na ndio maana nasema iko haja ya kuanza upya kudai Katiba mpya haraka iwezekanavyo,” alisema Lowassa. 

“Kama yupo mtu yeyote anayechukia matokeo ya uchaguzi uliopita, suluhisho lake ni kuwa na tume huru ya Uchaguzi itakayotokana na Katiba mpya. Tusipohangaika na Katiba mpya tutarudi palepale.”

Alirudia kauli yake kuwa baada ya uchaguzi kulikuwa na waliomtaka atangaze “kuingia barabarani”, lakini aliwakatalia. 

“Tutakuwa tunakwenda Ikulu kwa kufagia barabarani kwa damu za watu. No, tutakwenda Ikulu bila damu za watu wakati wowote na Mungu atatusaidia. Nawaambia wale wote ambao hawakuridhika, mnajua nguvu ya umma lakini msiitumie kuwaumiza watu,” alisema. 

Aliwataka viongozi wote wa Chadema kujali maslahi ya wanyonge kwa kuepuka kufanya kazi kwa mazoea. 

Meya wa Jiji la Dar es Salaam ambaye ni diwani wa Chadema, Charles Mwita aliwataka wanafunzi kufanya kazi ya kukijenga chama kwani mabadiliko ya kweli yataletwa na vijana. 

Muasisi wa Chaso, Pamela Maasaio aliwataka vijana wa Chadema kuachana na siasa za kwenye mitandao na badala yake waende mitaani kupiga kelele na kuweka mikakati ya pamoja.

Aliyelawiti Watoto Wawili Akijifanya Polisi Ahukumiwa Kifungo cha Miaka 60 Jela

MAHAKAMA ya Wilaya ya Bunda, mkoani Mara imemhukumu, Ally Mpemba au Ustadhi (32), Mkazi wa Mtaa wa Bunda Stoo mjini Bunda kifungo cha miaka 60 jela baada ya kupatikana na hatia ya kubaka watoto wawili kwa zamu akijifanya polisi.

Adhabu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya Bunda, Said Kasonso, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo pasipo kuacha shaka yoyote.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Hamuza Mdogwa, kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo mnamo Januari 17 mwaka huu, majira ya saa 8:30 mchana, katika kijiji cha Kitaramanka wilayani hapa.

Alisema kuwa mshtakiwa huyo aliwakuta watoto hao wakiwa katika eneo hilo na akawatisha kuwakamata akidai kuwa yeye ni askari Polisi na kwamba wamefanya kosa hivyo atawachukua maelezo yao na baadaye awapeleke kituoni.

Aliongeza kuwa mshtakiwa huyo alitoa Sh 200 na kumpatia mtoto mmoja aende akanunue daftari la kuandikia maelezo yao, na baada ya mtoto huyo kwenda ndipo alipombaka aliyebaki na kisha kumwambia adhabu yake imekwisha sasa aende nyumbani.

Alisema kuwa baada ya yule aliyetumwa daftari kurudi, Mpemba alimbaka pia na kumuamuru arudi nyumbani adhabu yake imekwisha na kwamba watoto hao baada ya kufanyiwa unyama huo walikwenda kutoa taarifa nyumbani kwa wazazi wao.

Aidha alisema kuwa Ofisa Mtendaji wa kata hiyo kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho walimkamata mshtakiwa huyo na kumfikisha Polisi.

Kabla ya adhabu kutolewa mshtakiwa huyo alipewa fursa ya kujitetea na akaiomba Mahakama hiyo impunguzie adhabu.

Hata hivyo mwendesha mashitaka huyo aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa huyo kwa sababu makosa aliyofanya ni ya kinyama na ya udhalilishaji mkubwa kwa watoto hao wenye umri wa miaka 16 kila mmoja.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Kasonso, alisema kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na kwamba kwa kosa la kwanza la kubaka mtoto wa kwanza ataenda jela miaka miaka 30 na la pili pia atatumikia kifungo cha miaka 30 jela na adhabu zote zinakwenda kwa pamoja hivyo atatumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye nia na tabia kama hiyo.

Katibu Mkuu wa Chadema Akwea Pipa Kujinoa Kisiasa Ujerumani


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji anatarajia kuhudhuria kongamano la kujadili sauti za wananchi kupitia Bunge katika maendeleo na Taifa litakalofanyika Ujerumani, Juni 20 hadi 25.

Msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene alisema jana kuwa, kongamano hilo litajadili mikakati ya kampeni na kushinda uchaguzi, hususan kwenye mazingira yenye changamoto mbalimbali za kisiasa huku pia wakijifunza umuhimu na nafasi ya Serikali za mitaa katika maendeleo ya wananchi.

“Katibu Mkuu Dk Mashinji pamoja na washiriki wengine watajadili kwa kina na kubadilishana uzoefu wa ushindani wa siasa kutoka maeneo mbalimbali, huku pia wakijifunza umuhimu wa kutumia teknolojia ya mawasiliano kupambana na changamoto za kisiasa, hasa katika nchi zinazoendelea,” alisema Makene.

Mada nyingine katika kongamano hilo zitahusu mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, kuwasaidia vijana kutambua umuhimu wa siasa na kushiriki.

Mbali na Dk Mashinji washiriki wengine watatoka nchi za Ufaransa, India, Ujerumani, Ghana, Ufilipino, Mexico, Mongolia, Argentina, Ukraine, Poland, Bolivia, Cambodia, Syria, Tunisia, Uganda, Kurdistan, Venezuela, Hoduras na Ugiriki.

Monday, June 13, 2016

VIDEO: Jionee wizi mpya wa mpesa na tigo pesa, jamaa kaibiwa 720,000


http://mobilemarketingmagazine.com/wp-content/uploads/2015/08/M-Pesa-Mobile-Money-User-Tanzania-Africa.jpgUtapeli umekua mwingi sana hapa mjini, watu wengi wanatapeliwa kila siku. Kutapeliwa ni kutapeliwa tu haijalishi ujanja utakaotumika ni wa sasa au wa zamani. Ila siku za karibuni kumetokea aina mpya ya utapeli ambao wahathirika wakubwa ni watu wanaotoa huduma za Mpesa na Tigo Pesa.

Kama utakavyoona katika video hii ni ngumu sana kugundua kama umeshatapeliwa mpaka baada ya mdaya mda upite. Kwa mfano huyu jamaa aliyetapeliwa hapa kaibiwa 723,000 na matapeli hao. Hebu tazama video hii na wewe usije ukaibiwa kama huyu.


Nimekuletea List Za Biashara Mbalimbali..Kamata Moja Ujikomboe

1. Kununua Mashine za kukoroga zege na kukodisha.
2. Kununua Mashine za kukata vyuma na kuzikodisha.
3. Kutengeneza na kuuza tofali
4. Ufundi, Website updating/Database: Katika Halmashauri, Manispaa, Mashule, Wizara, Wilaya na Makampuni mbalimbali.
5. Kuanzisha kituo cha redio na televisheni
6. Kufunga na kutengeneza vifaa mbalimbali vya electroniki na mawasiliano mfano; compyuta na vifaa vya compyuta na mawasiliano.
7. Kuuza software; mfano Antivirus, Operating Systems, Pastel, Tally, Myob, n.k
8. Kushona na kuuza nguo.
9. Kufungua Duka la kuuza nguo mpya; suit, socks, batiki, nguo za asili, Mashuka, Mashati, Suruali, 10. Ufugaji wa mifugo mbalimbali mfano Kondoo, Mbuzi, Ng’ombe, Kuku, Bata, na wengine.
11. Kufungua stationery, kuuza (supply) vitabu na vifaa mbalimbali ktk mashule na vyuo.
12. Kutoa ushauri mbalimbali wa Kitaalamu.
13. Kuuza viazi, mahindi, mihogo, kutengeneza popcorn na kuziuza.
14. Kusajili namba za simu na kuuza vocha
15. Kuwa na mradi wa Pikipiki zisizotumia mafuta na zinazotumia mafuta
16. Kilimo cha mazao mbalimbali kulingana na hali ya hewa ya sehemu husika.
17. Kuuza Mitumba
18. Kusimamia miradi mbalimbali
19. Kufungua duka la kuuza mitambo mbalimbali
20. Kufungua banda la chakula na chips
21. Kukodisha turubai viti na meza
22. Kufungua Supermarket
23. Kufungua Saluni
24. Kufungua Bucha
25. Video Shooting & Editing.
26. Kufungua Internet cafe 2
7. Duka la kuuza matunda
28. Kufungua duka la kuuza vifaa vya simu za mkononi na landline.
29. Kufungua duka la vifaa vya ujenzi; cement, vifaa vya umeme, duka la mabati
30. Kutengeneza michoro mbalimbali ya majumba na miradi ya ICT
31. Kuchapa vitabu, bronchures, n.k
32. Kuanzisha kampuni ya ujenzi (Building contractor)
33. Kuuza Vifaa vya umeme wa nishati ya jua (solar) ,battery, inverter na vifaa vingine vya solar n.k 34. Kuuza maji kwa jumla na rejaleja.
35. Kutengeneza na kuuza Unga wa lishe bora.
36. Kukodisha Music
37. Kuanzisha Mradi wa Taxi
38. Kuanzisha mradi wa Daladala
39. Kuuza vifaa vya Kompyuta, laptops, converters, HDDs, Monitors, Softwares, CD Copiers na vifaa vingine.
40. Kununua magenerator na kukodisha
41. Kufungua kampuni ya kutoa huduma za simu
42. Kufungua kampuni ya kutoa huduma za internet (ISP)
43. Kuuza mabati na vigae
44. Kujenga apartments
45. Kufungua Kisima cha mafuta ya taa au mafuta ya aina zote
46. Kufungua Duka la samaki
47. Kufungua Duka la nafaka
48. Kufungua Shule za Awali, Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo.
49. Kujenga hostel
50. Kuuza vocha na ving’amuzi vya DStv, Zuku, Startimes, Easy TV, TNG, Digitech, Continental. 51. Kujenga mtambo wa kuzalisha umeme na kuuza katika viwanda na wananchi.
52. Ufundi simu
53. Kufungua Hospitali, Zahanati.
54. Maabara ya Macho, Meno
55. Kuchimba/Kuuza Madini
56. Kufungua ofisi ya kutoa huduma ya simu na fax
57. Kuuza miti na mbao
58. Kufungua Grocery
59. Kufungua studio ya kupiga na kusafisha picha
60. Kucharge simu/battery
61. Duka la TV na vifaa vingine
62. Kuanzisha biashara ya kuuza vyakula katika sherehe na tamasha mbalimbali (catering).
63. Banda la kupigisha simu
64. Kuuza na kushona Uniform za shule
65. Kuanzisha duka la kuuza vitu kwa jumla.
 66. Kufungua gereji za kutengeneza bajaji, pikipiki na magari
67. Kuuza vyuma, pembejeo, rake, jembe 68. Kuuza fanicha
69. Kufungua sehemu ya kuziba pancha za matairi ya magari na mitambo.
70. Kujenga nyumba za kulala wageni (hotel) 71. Kuagiza na kuuza vifaa vya aluminium.
72. Kuuza vioo
73. Kushona na kukodisha nguo za harusi
74. Kufungua yard kwa ajili ya kuosha magari
75. Kuuza mashine za kuchomelea (welding machine).
76. Kuuza vifaa vya kuvaa Site (boots, helmets etc)
77. Kununua mabasi kwa ajili ya kusafirisha wanafunzi
78. Kufungua studio ya kutengeneza vipindi vya redio na televisheni
79. Kuanzisha ofisi ya michezo ya televisheni (TV Games)
80. Kufungua benki 81. Kuwa na malori ya kubeba kokoto na mchanga
82. Kuuza vifaa mfano TV, CCTV Camera, n.k
83. Kuwa dalali wa vitu mbalimbali
84. Kuanzisha mradi wa kukodisha fork lift na winchi (crane)
85. Kuanzisha kiwanda cha kutengeneza viatu.
86. Kuanzisha viwanda mbalimbali
87. Duka la vifaa vya simu na gadgets mbalimbali zinazoendana na mawasiliano ya Vodacom, TTCL, AIRTEL, TIGO, ZANTEL, n.k.
88. Kujenga Ukumbi wa kukodisha kwa sherehe, mikutano mbalimbali
89. Kununua matrekta, mitambo ya ujenzi wa barabara na kukodisha
90. Kutengeneza antenna na kuuza
91. Kufungua mradi wa Machine za kusafisha, kutoboa na kuchana mbao
92. Kufungua mradi wa kuuza vifaa vya Umeme wa kutumia upepo
93. Biashara ya kuagiza magari
94. Kufanya biashara za Jukebox
95. Kukodisha matenki ya maji**
96. Kufungua duka la kuuza Asali
97. Kutengeneza Mikokoteni/ matoroli na kuikodisha
98. Kufungua Duka la vinyago, batiki
99. Kuanzisha huduma ya AIRTEL MONEY, MPESA, TIGOPESA, EZY PESA
100.Kuanzisha sehemu ya kufanyia mazoezi (Gym).
101. Kununua na kuuza vifaa vya kupima ardhi.
102. Kufungua duka la kuuza dawa (pharmacy).
103. Kufungua Kampuni ya Ulinzi
104. Kufungua kampuni ya "Clearing and fowarding"
105. Kuchezesha vikaragosi
106. Kuuza spea za bajaji, magari na pikipiki
107. Kuuza baiskeli
108. Kuuza magodoro
109. Kuuza vyombo mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya nyumbani mfano bakuli, sahani, vikombe, vijiko,
110. Kuuza marumaru (limestones)
111. Kuuza kokoto
112. Kuuza mchanga
113. Kufundisha Tuisheni
114. Biashara za bima
115. Kampuni ya kusafirisha abiria kwa njia ya anga (ndege)
116. Biashara za kitalii
117. Biashara za meli na maboti.
118. Kampuni ya kuchimba visima
119. Kufungua ofisi ya wakili/mawakili wa kujitegemea
120. Kuuza mkaa
121. Kutengeneza mashine za kutengeneza tofali
122. Kampuni ya kupima ardhi
123. Kampuni ya magazeti
124. Kuchapa (printing) magazeti
125. Kuuza magazeti
126. Kuchimba mafuta
127. Kiwanda cha kutengeneza mabati
128. Kiwanda cha kutengeneza fanicha
129. Kiwanda cha kutengeneza matairi
130. Kutengeneza vitanda vya chuma
131. Kununua nyumba katika Maghorofa (Apartments) na kuzikodisha.
132. Kukodisha makapeti
133. Kupamba maharusi na kumbi za harusi/sherehe.
134. Mashine ya kusaga na kukoboa nafaka.
135. Kazi ya ususi na kusafisha kucha.
136. Kuuza Gypsum
137. Malori ya kubeba mafuta na Mizigo
138. Duka la kuuza mboga za majani
139. Duka la kuuza maua.
140. Kampuni ya kuzoa takataka
141. Kampuni ya kuuza magari
142. Kuuza viwanja
143. Uvuvi
144. Kutengeneza na kuuza nguzo za kujengea fensi
145. Uchoraji wa mabango.
146. Duka la kuuza silaha
147. Ukumbi wa kuonesha mpira
148. Biashara ya mlm (network marketing)
149. Yadi kwa ajili ya kupaki magari
150. Mradi wa trekta za kukodisha kwa ajili ya kilimo
151.Kuendesha bodaboda,Taxi,Daladala,Carry
KAMA YOTE HAYA UMESHINDWA KUPATA LA KUFANYA, BASI TUENDELEE KUWA WAAJIRIWA WA SERIKALI NA TUSUBIRI KUSTAAFU TU.

Zitto Kabwe Aibuka Baada ya Kupotea kwa Siku Mbili.....Kasemaje??? BOFYA Hapa

Baada ya taarifa za kutoweka, Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameibuka leo na kusema yuko salama wa afya huku akilaani mbinu za Jeshi la Polisi kutaka kumkamata kwa siri bila kufuata utaratibu unaotakiwa.

Tangu Jumamosi usiku, vyombo mbalimbali vya habari viliripoti Zitto kutofahamika alikokuwa baada ya simu zake zote kutopatikana huku viongozi wa chama hicho wakihofia kukamatwa na polisi baada ya kubaini njia za uviziaji wa kumkamata nyumbani
kwake.

"Ilikuwa Jumamosi , walikuja nyumbani kwangu wakiwa na magari matatu ila hawakufanikiwa, siwezi kukamatwa kwa `terms' zao ila nitakuwa tayari kukamatwa kwa `terms' zetu na wala siyo kuviziana, kama nina makosa kwa nini wanivizie," amesema Zitto Kabwe na kuongeza;

''Watu wetu wa Usalama wa Chama walihakikisha kwamba sitakamatwa ili niweze leo kupata fursa kuzungumza na watanzania kupitia nyie wana habari
 

''Hatufahamu Watawala wanaogopa nini mpaka kuzuia mikutano ya wanasiasa
 

''Nasikia Jana Walimkamata Mwenyekiti Mbowe wa Chadema Huko Mwanza kisa eti kawasalimia wananchi, huu ni uvunjwaji na ukiukwaji mkubwa wa utawala wa kidemokrasia

''Tunalaani tabia za Kidikteta za Rais Magufuli .Magufuli ameanza na vyama vya siasa kuonyesha Udikteta wake, nawahakikishia akimalizana na Vyama vya siasa atahamia kwenu Wanahabari, Tumkatalie
 

''Ndio maana Magufuli Ziara yake ya Kwanza alifanya Rwanda, tumegundua kuwa alikwenda kujifunza namna ya Kudhibiti Demokrasia na Kuongoza Kidikteta
 

''Hauwezi kupambana na Ufisadi kama haumpi nguvu ya Kiutendaji wa CAG. Kwa hali Hii anayokwenda Magufuli ajiandae kuwa rais wa term moja kwa sababu watanzania hawataweza kuvumilia kutawaliwa, kuminywa na kuburuzwa .

''CCM wamdhibiti Magufuli, na wasipomdhibiti sisi na Watanzania Tutamdhibiti
 

''Hatutakaa Kimya hata kama atatufunga, akimfunga Zitto watazaliwa wakina Zitto wengine, na kwenye hili hatutakaa Kimya, tutasimama kidete mpaka nchi irudi kwenye misingi''
 

''IGP ameagizwa na Magufuli anikamate, lakini hawezi kunikamata bila kufuata utaratibu, hawawezi kunikamata kwa kunivizia, viongozi hatukamatwi kwa kuviziwa viziwa, tumewaonyesha kwamba Polisi wanaweza kutukamata kwa kufuata terms zetu na sio zao
 
''Karibuni kesho saa tisa kwenye Kongamano letu, Hatuwezi kuacha kufanya siasa, lazima tuendelee kufanya siasa, mmehudhuria mikutano yetu hamjaona hata sisimizi amekanyagwa
 

''Wanasema Bajeti imeongezeka kwa 32% ukweli ni kwamba Bajeti imeshuka kwa maana Dola imeporomoka''

Audio: Gwajima afyatuka tena, amshauri Magufuli aihame CCM....Adai amenasa njama Mbaya


Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye anafahamika kwa kutoa kauli ‘tata’, amefyatuka tena akimshauri Rais John Magufuli kuihama CCM endapo kile alichokiita ‘njama alizozibaini’ ndani ya chama hicho zitaletwa mezani.

Gwajima ambaye amekiri kuwa katika kampeni alikuwa hamkubali Dk. Magufuli kutokana na kutokuwa na imani na CCM, amesema amemkubali  sana baada ya kuanza kazi ya urais kutokana na hatua ambazo amekuwa akizichukua ndani ya muda mfupi.

Akizungumza katika ibada ya Jumapili kanisani kwake, Gwajima ameeleza kuwa amebaini njama za baadhi ya wanachama wa CCM ambao ‘dili’ zao mbalimbali ikiwa ni pamoja na ‘flow meter’ ya mafuta yaingiayo nchini na makontena yaliyokamatwa yalikuwa yanawahusu, wameanza kampeni ya chinichini nchi nzima kutaka Rais Magufuli asipewe uenyekiti wa chama hicho.

Amesema kuwa watu hao wanazunguka nchi nzima kuwashawishi wanachama wa CCM kuridhia hoja ya kutenga uenyekiti wa chama na urais, ili kumnyima nafasi hiyo Rais Magufuli ambaye utendaji wake umewabana bila kujali ni wa chama chake.

Hivyo, amemshauri Rais Magufuli kuwa endapo itatokea hilo, akihame chama hicho na kuendelea na kazi yake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mengine, msikilize mwenyewe hapo chini:


Freeman Mbowe na Viongozi Wengine wa Chadema Wakamatwa.....Alipo Zitto Kabwe Bado ni Utata

Wakati Polisi ikimshikilia kwa saa mbili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mkoani Mwanza, jeshi hilo limefuta kongamano la kujadili Bajeti ya Serikali lililoandaliwa na ACT Wazalendo jijini Dar es Salaam huku kiongozi wake, Zitto Kabwe akisakwa.

Jeshi hilo lilizuia mkutano wa hadhara wa Chadema uliokuwa ufanyike wiki iliyopita mjini Kahama ambako lilitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanachama na wafuasi wa chama hicho, katika kile kilichoelezwa kulikuwa na dalili za uvunjifu wa amani.

Jeshi hilo pia lilizuia msafara wa viongozi wa chama hicho kuingia katika ofisi zake za Shinyanga walipokuwa wakielekea Mwanza.

Taarifa iliyotolewa jana na msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene ilieleza kuwa mbali na Mbowe, jeshi hilo pia lilikuwa linawashikilia Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi na Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita.

Wengine ni Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka na viongozi wengine na wanachama wa chama hicho waliokuwa wanashikiliwa katika kituo cha Polisi Nyakato, jijini Mwanza.

Makene alisema tangu asubuhi ya jana, Mbowe na viongozi wenzake walikuwa wakizunguka katika maeneo kadhaa ya jijini Mwanza kuwasalimia wananchi katika ‘vijiwe’ mbalimbali kabla hawajakamatwa.

Alisema, “Hadi sasa (saa 11 jioni) hakuna maelezo ya kushikiliwa kwao.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alithibitisha kukamatwa kwa viongozi hao na kubainisha kuwa waliachiwa bila kufunguliwa kesi yoyote.

“Walikutwa Igoma Sokoni wakizungumza na wananchi. Mikutano ya namna hii imezuiwa. Wamefungua kesi mahakamani, hivyo hakuna haja ya kufanya tofauti mpaka itakapohukumiwa,” alisema Msangi.

Alifafanua kuwa jeshi hilo halina uhasama wowote na Chadema au chama kingine chochote na "hatuwezi kukiingilia kinapofanya mikutano yake ya ndani au hotelini. Kilichozuiwa ni mikutano ya hadhara.”

Wakati Msangi akisema hayo, kongamano la ACT Wazalendo ambalo lilitakiwa lifanyike jana kuanzia saa 7:00 mchana kwenye Ukumbi wa Jengo la LAPF; Millennium Towers, Kijitonyama lilizuiwa na polisi.

Tangu mapema asubuhi, askari polisi walitanda katika eneo la ukumbi huo kuzuia kongomano hilo.

Ukumbini hapo, waandaaji walisema hakuna anayeruhusiwa kuingia kwani wamepewa maelezo ya kuufunga baada ya tukio lililoandaliwa kuahirishwa.

Zaidi ya viti 210 vilikuwa vimepangwa kwa ajili ya kongamano hilo na mmoja wa viongozi wa ukumbi huo alionekana akiondoa mabango yaliyokuwa yanautambulisha mkutano huo wa ACT.

Viongozi watatu wa ukumbi huo walikataa kueleza kinagaubaga juu ya sakata hilo, lakini taarifa za jumla zilisema mkutano umezuiwa.

Mmoja wa watumishi wa ukumbi huo, alisema: “Tuliandaa kila kitu, ila shughuli imeahirishwa. Ukumbi unatakiwa kufungwa. Hautatumika kwa leo.”

Ilipofika saa 5:00 asubuhi, Msemaji wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis alisema chama kinafanya mkutano wa dharura kwenye ofisi zake za makao makuu na baadaye kingezungumza na waandishi wa habari.

Saa 8:00 mchana, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mghwira akiwa na viongozi wenzake, isipokuwa Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe alikuwa mbele ya kamera za wanahabari akifafanua kilichotokea kwa wanachama, wafuasi wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla.

Alisema ilipotimu saa 4:00 asubuhi walipewa taarifa na mwenye ukumbi kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni limemjulisha kuwa chama hicho hakina kibali cha kuendesha kongamano hilo na kwamba kisiruhusiwe kufanya hivyo.

“Huku ni kufifisha demokrasia. Wapigania haki za kiraia wasimame imara na vyama vya upinzani katika kuilinda,” alisema Mghwira.

Wakati kongamano hilo likizuiwa, kuna taarifa za kukanganya juu ya alipo Zitto baada ya kudaiwa alikuwa anasakwa na polisi tangu juzi.

Taarifa hizo zinakuja siku chache baada ya kiongozi huyo kuitwa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam na kuhojiwa juu ya kauli alizozitoa kwenye mkutano wa hadhara zinazokosoa utendaji wa Serikali na kupinga matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.

Baadaye jioni, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Msafiri Mtemelwaalitoa taarifa kuwa Zitto ametoweka na hajulikani alipo. Hiyo ilikuwa ni baada ya askari kanzu kumtafuta kwa muda kwa saa kadhaa.

“Zitto amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu. Askari wanalinda nyumbani kwake tangu jana (juzi) usiku. Hivi sasa ametoweka, hatujui alipo. Lolote litakalompata, Jeshi la Polisi litajibu,” alisema Mtemelwa.

Awali, Mghwira alipoulizwa imekuwaje kuhusu Zitto alijibu kuwa mkutano ulikuwa wa dharura ndiyo maana viongozi wote hawakuwapo.

Mwigulu Nchemba Aapishwa Rasmi Kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.......Atoa ONYO Kali kwa Wauza Dawa za Kulevya

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu Nchemba amewataka wafanyabiashara haramu ya kuuza madawa ya kulevya kuacha mara moja biashara hiyo badala yake watafute shughuli halali za kujiingizia kipato.

Waziri Nchemba ametoa agizo hilo mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliyemteua kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Mh.Charles Kitwanga ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Aidha Waziri Nchemba alisema kuwa atahakikisha anasimamia Ulinzi na Usalama wa Raia na Mali zao kwa kuziba mianya inayohatarisha amani na utulivu katika nchi.

Naye Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba amesema kuwa atahakikisha anashirikiana na wataalum wa sekta tatu zilizo katika Wizara yake ili kufanya mapinduzi katika maeneo hayo yaliyoajiri zaidi ya asiimia 80 ya Watanzania.

Pia Waziri Dkt. Tizeba alisema kuwa Wizara itahakikisha inashugahulikia changamoto zinazozokabili vyama vya ushirika ambavyo vimekuwa havifanyi vizuri katika miaka ya hivi karibuni.

Mawaziri walioapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu Nchemba aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi anayejaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya Rais kutengua uteuzi wa Mh. Charles Kitwanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akimkabidhi hati ya kiapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu Nchemba mara baada ya kumuapisha Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba akila kiapo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akisaini hati ya kiapo mara baada ya kumuapisha Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu Nchemba wakipongezana mara baada ya kuapishwa Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akimpongeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu Nchemba mara baada ya kumuapisha Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akimpongeza Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba mara baada ya kumuapisha Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu Nchemba.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba (kulia) na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu Nchemba mara baada ya kuwaapisha Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.