Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema waendesha bodaboda na abiria wasiovaa helmet watakamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kutaka kujiua.
Makonda aliyemwakilisha Makamu wa Rais kwenye futari iliyoandaliwa na Benki ya NMB kwa wateja na wadau wake juzi, alisema abiria na wapanda vyombo hivyo wanatakiwa kuvaa helmet.
Alisema kupanda pikipiki bila usalama ni kwamba abiria anadhamiria kujiua, kwa sababu akipata ajali ni rahisi kupoteza maisha kwa kupiga kichwa chini.
“Nimeshawasiliana na kamati yangu ya usalama barabarani mkoa, hili nitalisimamia kikamilifu lazima wote wawe na helmet na wakikamatwa wote watashtakiwa,” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kupanda bodaboda bila kuvaa kofia hiyo, ni sawa na mtu anayechukua vidonge na kunywa na pombe kali, ambayo matokeo yake ni kifo.
Makonda alisema kazi hiyo ataifanya kipindi hiki cha Mfungo wa Ramadhani ili apate thawabu ikiwamo kuruhusu maduka makubwa kufanya kazi hadi usiku wa manane.
Alisema hiyo itasaidia wanaofanya kazi wakirudi nyumbani wanafuturu baadaye wanaswali Tarawehe, hivyo wanaweza kwenda kufanya manunuzi usiku.
Alisema kitakachofanyika ni kuimarisha usalama wa raia kupitia kamati yake ya ulinzi na usalama ya mkoa.
Pia, alisema atatangaza kupiga marufuku uvutaji sigara hadharani zaidi kwenye mikusanyiko na kupambana na vijana na watu wanaojihusisha na uvutaji wa shisha (bangi).
“Mtu asiyevuta sigara, anakerwa sana na moshi ndiye anayeathirika zaidi, nitatangaza rasmi hivi karibuni marufuku ya kuvuta sigara, sasa watu watafute kwa kuvutia… nitatangaza na hatua za kuchukua,” alisema.
Makonda alitumia nafasi hiyo kuwataka NMB kuchangia madawati, kwa shule za msingi na sekondari katika mkoa wake.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker alisema utamaduni wa kufuturu pamoja hasa katika Afrika unadumisha amani, umoja na upendo miongoni mwa Waislamu na watu wengine, hivyo wao wanauendeleza.