Ndoa ya Mwana FA haikuwa ya kifahari lakini ilikuwa bora, yenye furaha na iliyochangamka kuliko nyingi nilizowahi kuhudhuria, Ommy Dimpoz.
Akizungumza kwenye documentary yangu maalum niliyoipa jina ‘Bado Nipo Nipo ilivyogeuka kuwa historia kwa Mwana FA’, Ommy amedai kujifunza mengi kupitia ndoa ya swahiba wake huyo.
FA alifunga ndoa June 5, 2016 na mchumba wake wa miaka mingi ambaye tayari pamoja wana mtoto wa kike aitwaye Maleeka.
“Watu wengi wanaogopa kuoa kwasababu ya kufikiria gharama, naweza kusema kwamba ndoa ya Mwana FA haikuwa ndoa yenye mambo ya kifahari lakini ilikuwa moja ya ndoa nzuri kabisa nilizowahi kuhudhuria,” anasema Ommy.
“Haikuwa na mambo mengi kwa maana ya magharama, tumetoka msikitini tumeenda moja kwa moja nyumbani kwake. Baada ya hapo nyumbani kulikuwa tu na kasherehe kadogo tumekusanyika washkaji, kama house party. Ukiangalia kwasababu ilikuwa ndoa ya staa ikawa kubwa,” ameongeza.
Ommy pia amedai kuwa FA alikuwa amepanga kuifanya ndoa itakayohusisha watu wachache sana na ya faragha.
“Mwenyewe alitaka kwamba harusi iwe ni ya watu wasiozidi kumi,” anasema.
“Hakutaka watu watu wajue kabisa. Tulikubaliana kwamba hakutakuwa na picha hata moja. Kwahiyo mimi nilikuwa nahisi naenda kwenye harusi ambayo sitapost chochote. Lakini nafika msikitini naona watu wako busy wanairekodi Snapchat… nikaona hapa hamna siri na mimi nikaanza kurekodi hapo hapo nikaanza kuzirusha.”
“Baada ya hapo unajua tena ndoa jambo la heri, sio jambo la siri.”