MAHAKAMA ya Wilaya ya Bunda, mkoani Mara imemhukumu, Ally Mpemba au Ustadhi (32), Mkazi wa Mtaa wa Bunda Stoo mjini Bunda kifungo cha miaka 60 jela baada ya kupatikana na hatia ya kubaka watoto wawili kwa zamu akijifanya polisi.
Adhabu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya Bunda, Said Kasonso, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo pasipo kuacha shaka yoyote.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Hamuza Mdogwa, kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo mnamo Januari 17 mwaka huu, majira ya saa 8:30 mchana, katika kijiji cha Kitaramanka wilayani hapa.
Alisema kuwa mshtakiwa huyo aliwakuta watoto hao wakiwa katika eneo hilo na akawatisha kuwakamata akidai kuwa yeye ni askari Polisi na kwamba wamefanya kosa hivyo atawachukua maelezo yao na baadaye awapeleke kituoni.
Aliongeza kuwa mshtakiwa huyo alitoa Sh 200 na kumpatia mtoto mmoja aende akanunue daftari la kuandikia maelezo yao, na baada ya mtoto huyo kwenda ndipo alipombaka aliyebaki na kisha kumwambia adhabu yake imekwisha sasa aende nyumbani.
Alisema kuwa baada ya yule aliyetumwa daftari kurudi, Mpemba alimbaka pia na kumuamuru arudi nyumbani adhabu yake imekwisha na kwamba watoto hao baada ya kufanyiwa unyama huo walikwenda kutoa taarifa nyumbani kwa wazazi wao.
Aidha alisema kuwa Ofisa Mtendaji wa kata hiyo kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho walimkamata mshtakiwa huyo na kumfikisha Polisi.
Kabla ya adhabu kutolewa mshtakiwa huyo alipewa fursa ya kujitetea na akaiomba Mahakama hiyo impunguzie adhabu.
Hata hivyo mwendesha mashitaka huyo aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa huyo kwa sababu makosa aliyofanya ni ya kinyama na ya udhalilishaji mkubwa kwa watoto hao wenye umri wa miaka 16 kila mmoja.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Kasonso, alisema kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na kwamba kwa kosa la kwanza la kubaka mtoto wa kwanza ataenda jela miaka miaka 30 na la pili pia atatumikia kifungo cha miaka 30 jela na adhabu zote zinakwenda kwa pamoja hivyo atatumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye nia na tabia kama hiyo.