Katibu Mkuu wa National Reconstruction Alliance (NRA), Hassan Kisabya Almas amewataka Watanzania wanaoomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuonyeshwa kupitia matangazo ya moja kwa moja (Live) kuomba kwa utaratibu bila kuharibu amani ya Tanzania.
Aidha Katibu Mkuu wa Chama hicho, amesema kwamba amani iliyoko ni hazina kubwa ambayo nchi nyingine inatamani kuwa nayo.
Almas aliyasema hayo jana alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO).
“Leo hii tupo tunaopigania kutaka kuona Bunge Live, lakini yote haya ni kwa kuwa Tanzania amani tunayo, sidhani kama nchi kama Afghastan siku watakayoamua kuonyesha Bunge Live kwa mwaka mzima, kwa saa 24 kama wataweza kukaa kuangalia Bunge hilo, hivyo basi wale wanaotaka hayo, kwanza tudumishe amani yetu,” alisema Almas.
Almas alieleza kuwa, amani ya Tanzania ni zaidi ya dhahabu ambayo Tanzania inajivunia hivyo ni lazima Watanzania kuitunza na kuithamini amani ambayo ipo kwa sasa na kuacha kuchochea mambo ambayo yanaweza kuleta machafuko katika nchi na amani ambayo leo haithaminiwi ikaja kukumbukwa siku moja.
Pia, alisema yeye ni mmojawapo wa watu wanaopenda kuona Bunge Live lakini jambo hilo halishadadii kama inavyofanywa na watu wengine kwani anajua kwa kufanya hivyo anaweza kuhatarisha Amani ya Tanzania na hata hilo Bunge halitaweza kuliona tena kutokana na kutokuwa na Amani ndani ya nchi.
Vilevile, amewataka waandishi wa habari kuandika yale yaliyo mazuri ya nchi kuliko mabaya machache ili kuzidi kuitangaza Tanzania vyema kimataifa, kwani sio uzalendo kuona mambo yote mabaya yanakuwa ukurasa wa kwanza, bali kwanza yarekebishwe kwakuwa ni makosa yanayoweza kurekebishwa. Kalamu za waandishi wa habari ni chachu ya amani na maendeleo ya Taifa la Tanzania.