Friday, January 2, 2015

ROSE MHANDO; KIMYA KINAMAANISHA NDIYO?

NADHANI kati ya waimbaji wenye kufanya vizuri zaidi katika muziki wa Injili nchini, huwezi kumweka kando Rose Mhando ambaye amefanya kazi nyingi zilizompatia umaarufu mkubwa katika ukanda wote wa Afrika Mashariki.
Licha ya kutoa albamu zake mwenyewe, lakini pia ameimba kwa kushirikishwa na waimbaji wengine wengi maarufu katika eneo hili na hivyo kumfanya wakati f’lani awe ndiye msanii wa muziki huo anayelipwa zaidi kuliko wote.
Katika tamasha la tuzo za Injili lililofanyika mwaka 2004, alishinda tuzo tatu, Mtunzi Bora, Muimbaji Bora na Albamu Bora ya mwaka. Ana kazi nyingi nzuri, lakini baadhi yake ni albamu ya Kitimutimu, Uwe Macho na Jipange Sawasawa.
Hivi sasa anakimbiza na wimbo wake mpya, unaotamba sana wa Facebook. Ukimsikiliza kwa makini anavyotambaa kwenye mistari ya wimbo huo, huna sababu ya kutomtaja kama nyota halisi wa muziki huo.
Mara kwa mara, amekuwa akidai kuwa uimbaji wake wa nyimbo za Injili unatokana na maono aliyoyapata kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ndiyo maana aliamua kuondoka katika dini ya Kiislamu aliyokuwa awali na kuhamia Ukristo.
Kwa tafsiri ya wengi, waimbaji wa muziki wa Injili ni sawa na watumishi wengine wa Mungu, wakiwemo Mapadre, Maaskofu, Masheikh wanaozunguka duniani kusambaza upendo na amani. Kwa maana hiyo, wengi wangetaraji kuwa watu hao ni wenye kutenda mambo ya kumpendeza Mwenyezi na kwa vyovyote, ni mifano bora.
Lakini simulizi zinazosikika kuhusu Rose Mhando zinasikitisha sana, hasa kutokana na ukimya wake wa kuzizungumzia tuhuma zinazomkabili. Ukiacha maisha yake binafsi (sitaki kuzungumzia kuhusu ujauzito wake), kinachovuma zaidi hivi sasa ni tabia yake ya kuchukua fedha za watu kwa ajili ya shoo, halafu baadaye hatokei.
Imeshatokea mara nyingi kwa watu kutoa malalamiko ya aina moja kumhusu, baadhi wanadai anaposhindwa kutokea baada ya kuwa ameshachukua malipo ya awali, huwa hata hatoi taarifa za kuomba udhuru ili waliomwalika wajue namna ya kuweka mbadala au hata kubadili matangazo yao.
Pengine ni kwa vile haya ni matamasha ya Injili ambayo wahudhuriaji wake pia nao huwa ni wachamungu, lakini kama yangekuwa yale majukwaa ya Bongo Fleva, watu wanaweza kuuana, kwa kumtangaza msanii ambaye siku ya siku hatokei jukwaani.
Ingekuwa ni suala la siku moja, watu wangeweza kuelewa labda limetokea kwa bahati mbaya, lakini mfululizo wa matukio hayo unaonyesha ni jinsi gani hii imekuwa tabia yake ya sasa. Watu wanazungumza mengi kuhusu kinachotokea, ambacho kinahusisha na kuacha kwake kutokea kwenye shughuli mbalimbali.
Kitu cha ajabu ni kuwa pamoja na tuhuma hizo kusemwa katika vyombo mbalimbali vya habari, yeye mwenyewe amekuwa kimya kuzungumzia, kitu kinachoweza kuwapa ishara watu kuwa kinachozungumzwa juu yake ni kweli, ndiyo maana anakosa cha kujibu.
Nasema hivi kwa sababu huenda ni njama zinazosukwa dhidi yake ili kumwondolea uaminifu miongoni mwa mapromota, hasa kama tunavyojua kuwa muziki huo nao hivi sasa umeondoka katika kuwa kazi ya Mungu, na sasa ni biashara kubwa.
Vinginevyo, Rose anahitaji kubadilika ili kuirejesha taswira yake halisi katika muziki huu, ambao yeye ameshiriki kwa kiasi kikubwa katika kuutangaza na hata kuitambulisha nchi yetu kimataifa.
Ni jambo la ajabu Mtumishi wa Mungu kuonekana tapeli na hata neno hili linapozidi kupata umaarufu, halionekani kumshtua yeye mwenyewe.