Huo unakuwa mchezo wa pili mfululizo timu hiyo kufungwa, baada ya awali kulala 1-0 mbele ya Swaziland Jumatatu na sasa itakamilisha ratiba Ijumaa kwa kumenyana na Lesotho kabla ya kurejea nyumbani.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Duncan Lengani wa Malawi aliyesaidiwa na Arsenio Chadreque Marengula wa Msumbiji na Isaskar Boois wa Namibia, Madagascar walikwenda kupumzika wakiwa wanaongoza mabao 2-0.
Mshambuliaji wa Tanzania, John Bocco akimtoka beki wa Madagascar |
Ibrahim Hajib wa Tanzania akitafuta maarifa ya kumtoka wachezaji wa Madagascar |
Madagascar walipata bao lao la kwanza dakika ya 13, mfungaji Rakotoharimalala Martin Njiva aliyemalizia krosi ya Randriamanjaka Rinho Michel kutoka upande wa kushoto.
Randriamanjaka Rinho Michel mwenyewe akapasua ukuta wa Taifa Stars baada ya pasi ya Njakanirina Tobisoa aliyemtoka Oscar Joshua na kwenda kumtungua kipa Deo Munishi ‘Dida’.
Stars ilizidiwa kabisa uwezo na Madagascar kipindi cha kwanza na washambuliaji Juma Luizio na John Bocco hawakuwa na madhara mbele ya ukuta wa wapinzani wao hao.
Hakuna shambulizi la maana Taifa Stars walifanya kipindi hicho, wakati Dida pamoja na kutunguliwa mara mbili, lakini aliokoa mashuti kadhaa ya hatari.
Kipindi cha pili, kocha Mart Nooij alianza na mabadiliko, akimpumzisha Mrisho Ngassa na kumuingiza Simon Msuva ambaye dakika ya Dk 52 alikaribia kufunga.
Mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Msuva alipokea pasi nzuri ya Said Hamisi Ndemla na kujaribu kumfunga kipa Randrianasolo Jean Dieu Gonne ambaye mpira ulimpita, lakini akawahi kugeuka na kuokoa kwa mguu.
Kocha Mholanzi, Nooij akafanya mabadiliko mengine dakika ya 55, akimtoa Ndemla na kumuingiza Shomary Kapombe.
Kuanzia dakika ya 65, Taifa Stars walianza kucheza kwa kujihami kuhofia kufungwa mabao zaidi, huku wakifanya mashambulizi ya kushitukiza.
Nooij alimtoa Juma Luizio na kumuingiza Ibrahim Hajib dakika ya 65 na kidogo mchezaji huyo akishirikiana na Msuva waliisumbua ngiome ya Madagascar.
Razanakotho Dina alitajwa mchezaji bora wa mechi baada ya mchezo huo.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Erasto Nyoni, Oscar Joshua, Salim Mbonde, Aggrey Morris, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla/Shomary Kapombe dk55, John Bocco, Juma Luizio/Ibrahim Hajib dk65 na Mrisho Ngassa/Simon Msuva dk46.
Madagascar; Randrianasolo Jean Dieu Gonne, Njakanirina Tobisoa, Fenolahy Zenith, Andianomenjanahary Francois, Rabeson Fetraniaina Michael, Raveloarisona Ardino, Razanakoto Dina, Sarivahy Vombola Nonoh, Rakotoharimalala Martin Njiva, Andriamanalina Lantoniaina na Randriamanjaka Rinho Michel.