Sunday, June 19, 2016

Irene Uwoya na Skendo ya Kubakwa!

Untold story! Skendo ambayo haijawahi kuandikwa wala kusimuliwa popote inayomhusu mwigizaji ‘hot’ wa sinema za Kibongo, Irene Pancras Uwoya ‘Mama Krish’ ni juu ya madai ya kubakwa na mfanyabiashara maarufu wa Kihindi jijini Dar (jina linahifadhiwa kwa sasa), alipokuwa na umri wa miaka 18 ambapo kwa sasa ana umri wa miaka 28, Ijumaa limefukunyua na kuinyaka.

Chanzo chetu makini ambacho ni mtu wa karibu wa Uwoya kilichoomba hifadhi ya jina gazetini kilidai kuwa, tukio hilo limekuwa likimtesa Uwoya kwenye maisha yake kiasi kwamba kila akilikumbuka huwa anakosa amani.

KISIKIE CHANZO
“Irene (Uwoya) ana kitu ambacho kinamtesa sana na mara kadhaa amekuwa akiniambia kuwa, ipo siku atakitengenezea filamu, anazungukazunguka sana ila alimdokeza mtu kuwa aliwahi kunusurika kubakwa, labda mkijaribu kumdodosa anaweza kuwapa ukweli,” kilifunguka chanzo hicho na kuongeza:

“Chondechonde asijue tu kwamba mimi ndiye nimewaambia maana alisema skendo hiyo ikiandikwa magazetini na dunia ikajua kilichompata, anaweza akajifungia ndani mwaka mzima kwa aibu.”

UWOYA ANASEMAJE?
Baada ya kuinasa habari hiyo, Ijumaa lilifanya jitihada za makusudi za kumsaka mlimbwende huyo aliyeshiriki Shindano la Miss Tanzania 2006/07 na kushika nafasi ya tano ambapo baada ya kubanwa ipasavyo kwa kuwa alikuwa hataki kusikia habari hiyo, alikiri kunusa skendo hiyo ila akafafanua kuwa, si kweli kwamba alibakwa bali ilibaki ‘kiduchu’ kitendo hicho kikamilike.

“Nikiri tu kwamba ni tukio ambalo sijawahi kulisimulia popote lakini kwa kuwa umenibana, ngoja niseme kilichotokea ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema Uwoya na kuendelea:

“Sikumbuki ilikuwa mwaka gani ila ni kweli nilikuwa na kama miaka 18. Nilikuwa na tabia ya kwenda na wenzangu kwenye nyumba ya mfanyabiashara mmoja ambaye alikuwa jirani yetu, Mbezi- Beach (naomba nisimtaje) kuangalia muvi.

“Siku moja, tukiwa kwenye sebule ya tajiri huyo ambaye ana asili ya Kihindi aliyekuwa akiishi peke yake, aliniita chumbani kwake.

“Kwa kuwa tulikuwa tumezoeana sana, sikuwa na wasiwasi wala kudhani angeweza kunifanyia jambo baya. Hee! Ile kuingia ndani si akafunga mlango, wenzangu kule sebuleni hawakujua chochote. Alichokifanya ni kunilazimisha kufanya naye mapenzi kwa nguvu, akaanza kunivua nguo, nikaona hapa nimekwisha.

“Nilichokifanya nilipiga kelele huku nikipiga ule mlango ndipo wale wenzangu walipokuja na kutaka mlango ufunguliwe, jamaa alipoona kimenuka alifungua mlango akatoka nduki na kutokomea nje.”

TAARIFA YAFIKA KWA WAZAZI
Kufuatia tukio hilo, Uwoya alifikisha taarifa kwa wazazi wake ambapo baba yake, Mzee Pancras Uwoya alilivalia njuga na kumfungulia kesi mfanyabiashara huyo, kesi ambayo ilinguruma kwa muda mrefu.

“Ni tukio ambalo liliwashangaza wengi na sikumbuki hasa kilichoendelea ila ninachojua yule mfanyabiashara alitoa fedha nyingi kwa kitendo kile cha kunidhalilisha,” alifunguka Uwoya.

ANAFICHA KUBAKWA?
Alipobanwa juu ya madai kuwa alibakwa ila hataki watu wajue kuwa alifanyiwa kitendo hicho, Uwoya alisema: “Kwa kweli hakufanikisha azma yake, alilazimisha kunivua nguo kweli lakini hakufanikiwa baada ya mimi kupiga kelele.

KWA NINI AMEFUNGUKA LEO?
“Nimeamua kuliweka wazi kwa kuwa umenibana juu ya ishu hiyo na ili watu wajue kwamba sijawahi kukwaa skendo ya kubakwa ‘pasee’ ila nilinusurika kubakwa. Lakini pia nimefanya hivi ili kuwapa fundisho wasichana wengine kutomuamini kila mtu, kwani aliyetaka kunifanyia kitendo hicho ni mtu ambaye sikumdhania.”