MAJANGA! Baada ya kuchomoka kwenye ule msala wa awali wa madawa ya kulevya, video queen matata Bongo, Agness Gerald ‘Masogange’ amejikuta akiteseka kwa ishu hiyo kwa mara nyingine.
Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia Risasi Jumamosi, Masogange alipatwa na msala huo mara baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar hivi karibuni akitokea nchini Afrika Kusini ‘Sauz’ ambapo alidakwa na polisi wa kitengo cha kudhibiti madawa ya kulevya nchini kilicho chini ya Godfrey Nzowa.
Akisimulia ishu hiyo, Masogange ambaye umaarufu wake mkubwa ulizaliwa katika video ya Wimbo wa Masogange wa Abednego Damian ‘Belle 9’, alisema alikamatwa na watu wa uhamiaji nchini baada ya kuhisiwa kuwa hati yake ya kusafiria ina matatizo.
“Walinikamata baada ya kuiona hati ilikuwa na ule msala wa awali lakini walinihoji na nikawapa majibu ambayo yaliwaridhisha, wakaniachia.
“Hii ishu inanitesa sana lakini nashukuru Mungu kwa kuwa nakamilisha taratibu za kuwa raia wa Afrika Kusini, nitaishi kule,” alisema Masogange alipobanwa na Risasi Jumamosi.
Juzi wakati gazeti hili likienda mitamboni, Masogange alikuwa kwenye Ubalozi wa Sauz nchini katika harakati za mwisho kukamilisha taratibu za kuwa na uraia wa Afrika Kusini ambako amesema ndiko atakapokuwa akiishi.
Julai 9, mwaka jana, Masogange alikamatwa na madawa ambayo yalihisiwa kuwa ni ya kulevya nchini Afrika Kusini, akashikiliwa na polisi kwa miezi kadhaa.
Septemba, mwaka jana Mahakama ya Kempton ya jijini Johannesburg, baada uchunguzi kukamilika na kubainika kuwa hayakuwa madawa ya kulevya bali ni kemikali zinazotengenezea madawa ya kulevya, Masogange alitakiwa kulipa faini ya R30,000 (Sh4.8 milioni), akawa huru.