Monday, November 10, 2014

RAIS KIKWETE AFANYIWA UPASUAJI WA TEZI DUME MAREKANI, HALI YAKE INAENDELEA VYEMA

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na  Dkt.Edward Shaeffer wa  hospitali ya Johns Hopkins (kushoto) na Daktari wa Rais Profesa Mohamed Janabi  (kulia) muda mfupi baada ya kuwasili ili kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyopo  Baltimore Maryland Marekani Jumamosi asubuhi.Upasuaji huo uliochukua muda wa saa moja na nusu  ulifanyika salama.Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na daktari Bingwa Mpasuaji Edward Shaeffer muda mfupi kabla ya kuingia kwenye chumba cha upasuaji uliofanyika katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyopo Baltimore  Maryland nchini Marekani Jumamosi asubuhi(picha na Freddy Maro).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alfajiri ya jana, Jumamosi, Novemba 8, 2014, alifanyiwa upasuaji wa tezi dume (prostrate) katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani.  
Rais Kikwete amefanyiwa upasuaji huo baada ya madaktari waliomfanyia uchunguzi wa afya yake  kujiridhisha kuwa Rais alikuwa anahitaji matibabu ya aina hiyo. Upasuaji huo uliofanyika alfajiri na kuchukua kiasi cha saa moja unusu, umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa.  Hali ya Mheshimiwa Rais Kikwete inaendelea vizuri, bado yuko wodini akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari na kupatiwa tiba. 
Wananchi wataendelea kupewa taarifa sahihi kuhusu hali ya Rais Kikwete kwa kadri zitakavyokuwa  zinapatikana.  
Imetolewa na KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU
DAR ES SALAAM,
NOVEMBA 9, 2014