Tuesday, June 9, 2015

MTOTO: NIMEUNGUZWA NA BIBI KWA KUPOTEZA KALAMU YA SH. 200

MTOTO Jackson Hosea (10) wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kiseke iliyoko Ilemela, Mwanza  ameunguzwa mwilini kwa kisu na imedaiwa kuwa aliyefanya kitendo hicho cha kinyama ni bibi yake aitwaye Laurencia Athanas.
Mtoto Jackson Hosea akiwa na majeraha tumboni baada ya kuunguzwa kwa kisu na bibi yake.
Taarifa zaidi kutoka chanzo chetu ndani ya jeshi la polisi, kimesema kwa njia ya simu kwamba mtoto huyo alifanyiwa unyama huo Mei 23, mwaka huu siku ya Ijumaa jioni.
“Wakati akitoa maelezo polisi, mtoto huyo alikuwa akitokwa na machozi kufuatia maumivu makali aliyoyapata kwa sababu ya kupoteza kalamu ya shilingi 200,” kilisema chanzo.
KALAMU YA SH 200
Imedaiwa kwamba mwanafunzi huyo mara baada ya kutoka shule alijikuta hana kalamu aliyonunuliwa na bibi yake huyo mzaa mama ambaye wanaishi naye ndipo alipoadhibiwa na kubaki na majeraha makubwa mgongoni na kwa sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Bugando, Mwanza.
MIKONONI MWA POLISI
Polisi mkoani Mwanza walipata habari hizo kutoka kwa walimu na majirani wa mama huyo ndipo walikwenda kumkamata.
“Hivi sasa jeshi la polisi linamshikilia  bibi huyo mkazi wa Kiseke, Ilemela kwa tuhuma za kumchoma kwa kisu cha moto mjukuu wake na  kumsababishia majereha mbalimbali  mwilini,” kilisema chanzo.
Picha tofauti zikionyesha jinsi mtoto huyo alivyojeruhiwa kwa kisu na bibi yake.
Habari zinasema kuwa mtoto huyo akiwa kituo cha polisi, alisimulia kila kitu kuhusiana na unyama huo na alipoulizwa alipo mama yake mzazi alisema anaishi Nzega.
AFISA MTENDAJI
Afisa mtendaji wa eneo hilo, Bi. Hellen  Mcharo amelithibitishia gazeti hili kutokea kwa tukio hilo.
Mcharo alisema: “Tukio hilo liliibuliwa kwa mara ya kwanza Mei 25, 2015 na  mwalimu mmoja ninayemfahamu kwa jina moja la Midali.
“Alimuona mtoto akiwa na majeraha ya kuchomwa moto na alipomuuliza alisema aliunguzwa na bibi yake, Mei 23, mwaka huu,” alisema kiongozi huyo.
POLISI WANASEMAJE?
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, SACP Charles Mkumbo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Kwa kweli ni tukio la kusikitisha sana na huyo bibi Laurencia  Athanas tunamshikilia na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema. kamanda huyo.