Monday, June 30, 2014

SERIKALI:SIMU ZA MKONONI ZINA MADHARA MAKUBWA SANA...SOMA ZAIDI

SERIKALI imewataka Watanzania kununua simu zenye viwango kwa kuwa utafiti uliofanywa na taasisi mbalimbali za afya duniani, umebaini kuwa mtumiaji akizungumza kwa simu kwa muda mrefu, anapata madhara.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga, alisema hayo jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chonga, Haroub Mohamed Shamis (CUF).
Chonga katika swali lake alisema kwa kuwa imebaini kuwa utumiaji wa simu za mkononi kwa zaidi ya dakika sita una madhara kwa afya za watumiaji hasa wanapoongea na simu kwa zaidi ya dakika sita, Serikali ieleze inawalinda vipi watumiaji hao.
Akijibu swali hilo, Kitwanga alisema mawasiliano ya simu za mkononi husafirishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa kupitia mawimbi ya redio ambayo yanazalishwa na umeme.
Alisema mawaimbi hayo katika hali ya kawaida yamethibitishwa kitaalamu kuwa yako katika kiwango cha chini na hivyo kutokuwa na madhara na binadamu.
phones
Alifafanua kuwa pamoja na kuthibitisha huko, taasisi mbalimbali za kiafya duniani zimebaini kuwa mawimbi hayo ya simu yana madhara pale mtumiaji anapoongea kwa muda mrefu na hasa kwa kutumia zenye ubora ulio chini ya viwango.
Ili kulinda afya za watumiaji, Kitwanga alisema Serikali kupitia mamlaka zake mbalimbali za udhibiti wa mawasiliano na viwango, inaendelea na jitihada za kuelimisha wananchi kuhusu madhara hayo yanayoweza kujitokeza kutokana na kuongea muda mrefu.
Pia alisema Serikali inaendelea kuhakikisha bidhaa za simu zinazoingizwa nchini zinakuwa na ubora unaotakkiwa pamoja na uwezo wa kumkinga mtumiaji na madhara yanayoweza kujitokeza.
Aliwataka wananchi kutumia simu za mkononi zenye ubora unaokubalika pamoja na kushirikiana na Serikali katika kupambana na wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa za simu za mkononi zilizo chini ya ubora.