Hakatizi mtu: Mshambuliaji wa Uholanzi, Arjen Robben akifanyiwa madhambi na beki wa Argentina, Martin Demichelis.
TIMU ya Argentina imetinga fainali ya michuano ya Kombe la Dunia 2014 baada ya kuiondoa Uholanzi kwa penalti 4-2 kwenye mchezo wa nusu fainali uliopigwa Sao Paulo, Brazil usiku huu.
Kipa wa Argentina, Sergio Romero, alifanikiwa kuokoa mikwaju miwili ya penalti iliyopigwa na Ron Vlaar na Wesley Sneijder wa Uholanzi baada ya dakika 120 kumalizika timu hizo zikiwa suluhu.
Lionel Messi, Ezequiel Garay, Sergio Aguero na Maxi Rodriguez waliifungia Argentina kwa penalti huku Waholanzi Arjen Robben, Dirk Kuyt wakifunga penalti za Uholanzi.
Kwa matokeo ya leo, Argentina watamenyana na Ujerumani katika fainali itakayopigwa Julai 13 mwaka huu huku Uholanzi na Brazil wakipepetana kuwania nafasi ya mshindi wa tatu.