Shilole si mgeni katika kuota vitu vikubwa. Kutoka kwenye ndoto yake ya kufanya kolabo na Jennifer Lopez, awamu hii ameenda mbali zaidi. Muimbaji huyo amechoka ‘Kuchuna Mabuzi’ na sasa anataka kuingia mjengoni. Mrembo huyo ambaye jina lake halisi ni Zuwena Mohamed, amepanga kugombea ubunge kwenye jimbo analotokea la Igunga mkoani Tabora katika uchaguzi wa mwaka 2015!
Akizungumza kwenye kipindi na Sizi Kitaa cha Clouds TV, Shilole amesema yupo serious na nia hiyo na kama Mungu akipenda atakuwa mbunge wa jimbo hilo.
“Baada ya Dokta Dalali Kafumu anayefuata ni mimi,” amesema Shilole. “Mimi nadhani napenda jimbo langu na napenda wakazi wangu wa Igunga wananiona toka nakua mpaka sasa hivi, kwahiyo wanafurahi. Sasa wananiambia ‘sisi hatutaki kumpa mtu mwingine kiti hiki sasa wananipa changamoto. Vitu viwili vya kwanza ambavyo nitavifanya nikiingia kwenye lile bunge nikiwa kama msanii, kwanza nitatetea haki za wasanii, cha pili Igunga yangu wapo wakazi wa Igunga vijana wapate kazi, yaani akina mama, wale mama lishe na wengine lazima wawe na kazi zao. Kwahiyo nitawatafutia kazi, nitajenga chuo cha muziki,” alijinadi muimbaji huyo.
“Mimi jimbo langu nalijua na nimekua pale mpaka nimekuwa mkubwa lazima nilitimize sitaki wananchi wangu wapate tabu. Mimi nadhani wanaoenda kugombea majimbo yasiyo ya kwao wanaweza fanya chochote, lakini kama ni wa hapo lazima itakuuma. Lakini unakuta mtu wa Dar es salaam anakwenda kugombea Mtwara huko nani anamjua? Mimi nitaenda kugombea kwangu lazima nitapata kura lazima watanipa! Kwahiyo kaeni tayari Shilole ni mbunge mtarajiwa Igunga,” alitamba.