Monday, July 28, 2014

SHULE SEKONDARI SHINYANGA KUWATIMUA WAVAA MINI-SKIRTS WATUMIA VIPODOZI NA WAVAA MILEGEZO.


Shule ya Sekondari Mwadui iliyopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, imetangaza kufukuza wanafunzi wote wanaotumia vipodozi, wanaovaa sketi fupi, milegezo na wanaotumia simu za mkononi shuleni.
 
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, Mchungaji Yohana Nzelu, alisema hayo jana katika kikao cha Bodi ya Shule na Wazazi.
 
Mwalimu Nzelu alisema moja ya chachu ya mafanikio ya wanafunzi shuleni, ni nidhamu ya kutosha na maadili mema na kuongeza kuwa Bodi hiyo ilikaa na kujadili namna ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wake na kuweka mikakati, ikiwemo hatua hizo.
 
Akisoma taarifa kwa wazazi na walezi wa wanafunzi walio katika shule hiyo, Mwalimu Nzelu alisema hatua hizo zinalenga kuzuia wanafunzi kujiingiza katika makundi mabaya na kuboresha taaluma.
 
‘’Shule hii katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012, wanafunzi 61 waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu na mwanafunzi mmoja alichaguliwa kwenda kidato cha tano.”
 
‘’Mwaka jana (2013) wanafunzi 76 walifanya mtihani wa kidato cha nne, waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu 33, waliochaguliwa na Serikali kujiunga kidato cha tano wanafunzi 24, na waliokwenda shule binafsi walikuwa saba.
 
 “Tumepiga hatua hivyo mikakati iliyopo ni kusisitiza maadili na kuondoa changamoto zilizokuwepo za wanafunzi kukosa nidhamu,“ alieleza Mwalimu Nzelu.
 
Akizungumza kwenye kikao hicho, Askofu Mkuu wa KKKT  Dayosisi hiyo, Emmanuel Makala, ambaye ndiye msimamizi wa shule hiyo, alisema suala hilo si la kupuuzwa na hawatakuwa na msamaha kwa mwanafuzi atakayekiuka sheria hizo huku akitoa mwito kwa wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja.
 
Askofu Makala alisema wazazi na walezi wakishirikiana ipasavyo na walimu kwa kufuatilia taarifa za watoto wao shuleni, itasaidia kwa kiwango kikubwa kuongeza taaluma ya wanafunzi na kupata ufaulu mzuri