Uongozi wa Yanga umesema Mwenyekiti wa Kamati ya ujezi wa jengo la Mafia, Ridhiwani Kikwete siyo mwanachama wa klabu hiyo kwa kuwa hajalipa ada yake kwa miezi sita mfululizo.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto ilieleza kitendo cha Ridhiwani kupinga hatua ya Wajumbe wa Bodi ya Udhamini na wanachama wa Yanga kwa pamoja kumuongezea muda wa mwaka mmoja, mwenyekiti wao, Yusuf Manji hayana uzito kwa kuwa siyo mwanachama.
“Ridhwani Kikwete hajalipa ada zake za uanachama kwa miezi zaidi ya 6 mfululizo na kwa mujibu wa Katiba ya Yanga ibara ya 13 kipengele cha pili ambacho kinasema kuwa endapo mwanachama hajalipa ada yake kwa muda wa zaidi ya miezi sita mfululizo atakuwa amekoma kuwa mwanachama wa Yanga.”
Taarifa hiyo ya Yanga imekuja ikiwa ni siku moja baadaya Ridhiwani kukaririwa na gazeti hili akisema haridhishwi na mambo ya migogoro ya kikatiba yanayoendelea ndani ya Yanga.