Tuesday, September 23, 2014

BI. MOZA ATAMANI MWISHO WA DUNIA UFIKE HARAKA

Kikongwe mmoja aliyefahamika kwa jina la Moza Nyanongwa (anakadiria ana miaka zaidi 100), mkazi wa Tandale, Kwatumbo jijini Dar amefunguka kuwa anatamani mwisho wa dunia ufike mapema kwa kudai kuchoshwa na mmomonyoko wa maadili unaoendelea nchini na dunia nzima kwa jumla.
Kikongwe anayefahamika kwa jina la Moza Nyanongwa.
UZINZI, KATA ‘K’, NGUO FUPI ZAMCHEFUA
Akizungumza na mwandishi wetu, nyumbani kwake, Bi. Nyanongwa alisema kuwa amefikia hatua hiyo kwa kuwa mambo mengi maovu yanayoendelea nchini hivi sasa yanamchefua kwa kiasi kikubwa na kuongeza kuwa hayakuwepo enzi zake kwa kuwa kila mtu alikuwa akijiheshimu kimavazi na lugha tofauti na siku hizi ambapo wasichana hukaa nusu uchi huku vijana wa kiume wakibobea kwenye uhuni na kuvaa suruali na kaptura kwa mlegezo ‘kata K’ na kuonesha nguo za ndani na kuendekeza uzinzi na ulevi.
“Enzi zetu hakukuwa na mambo kama haya, tulikuwa tukivaa vizuri, wanaume walikuwa wakivaa suruali na kaptura kiunoni siyo chini ya makalio, wakati wanawake walivaa magauni na kanga au vitenge,” alisema Bi. Nyanongwa.
Nyanongwa ambaye asili yake ni Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani, aliongeza: “Enzi zetu tulikuwa tunacheza ngoma za asili kama vile Mkwaju Ngoma lakini vijana wa siku hizi wamebadilika ghafla na kucheza nusu uchi usiku mzima kwenye ngoma zao wanazoziita Vigodoro na Rusharoho, wakati wanacheza watu wanakusanyika kushangilia upuuzi huo.”
WANAOKAA PAMOJA BILA NDOA NI MAHAWARA
Kwa upande wa uhusiano wa kimapenzi, Nyanongwa hakuficha kushangazwa na watu ambao hukaa pamoja kama mume na mke pasipo ndoa au bila kutambulishana kwa wazazi.
“Kitendo hicho ni uchafu mkubwa ambao unachochea kuharibika kwa maadili pia ni utovu wa nidhamu kwa wazazi wa pande zote mbili, unaishije na mwanamke hujajitambulisha kwao? Siyo kwamba ni utovu wa maadili tu lakini akipatwa na janga utafanyaje?
“Enzi zetu hata kama huna hela ya mahari ulikuwa unaweza ukakopa kwa wakwe, wao wanakuozesha, ukipata unapeleka, na watu walikuwa wakifanya hivyo kwa sababu walikuwa waaminifu, ndoa hiyo ilikuwa ikiitwa ndoa ya ‘Mwajala’.

Bibi Moza Nyanongwa akiwa nyumbani kwake.
“Hivyo hakukuwa na sababu ya kuishi mwanaume na mwanamke pamoja bila kuoana, jamii ilijua kabisa kuwa hivyo ni vitendo vya uhawara jambo ambalo lilikuwa likiepukwa kwa sababu watu walikuwa wanaona haya,” alisema.
Akizungumza kwa masikitiko huku akiwasha sigara yake, Bi Nyanongwa alisema kuwa hivi sasa hali ni mbaya kufikia hatua hadi mzazi anaweza akamtukana mwanaye wa kumzaa matusi ya nguoni au kumuita mbwa, utashangaa, hajui kuwa kama mtoto wake ni mbwa maana yake hata yeye ni mbwa!
WATOTO KUTUKANA WAZAZI
“Siku hizi utakuta watu wazima wanapigana kisha wanavuana nguo hadharani watoto wakiwa wanaona kila kitu, kama siyo laana ni nini hicho?
“Ajabu ni kwamba hata watoto nao siku hizi haishangazi kuona wakiwatukana wazazi wao! Hawajui kabisa kuwa mama na baba yao ni Mungu wa hapa duniani,” alisema bibi huyo huku akiwa amekunja sura.
Akielezea jinsi maisha yalivyokuwa enzi zao, Bi Nyanongwa alisema kuwa ili kuwa ni nadra sana kwa mtu kupelekwa polisi kwa makosa mbalimbali tofauti na siku hizi.
Alijitolea mfano yeye mwenyewe kuwa mpaka anafika umri wake huo, hajawahi kufikishwa kituo cha polisi au kutuhumiwa kwa kosa lolote.
“Sijawahi kufikishwa polisi kwa kosa lolote na jirani au chombo cha dola kwa sababu moja tu kwamba nilikuwa nafuata maadili. “Usipofuata maadili utaiba, utakula rushwa na utawaona wenzako siyo sawa na wewe na ndiyo maana viongozi wengi wa siku hizi wanalaumiwa kwa rushwa na wizi, hawafuati maadili,” alisema.
“Kwanza kituo chenyewe cha polisi sikijui hata kidogo, sijawahi kufikishwa kwa kosa lolote. Enzi zetu ukimuona polisi unakimbia na kujificha, siku hizi mtu mmoja ana kesi kibao polisi,” alisema Bi. Nyanongwa.
KWA NINI ANATAKA MWISHO WA DUNIA UJE?
“Kutokana na kuongezeka uovu huo na mengine mengi kama vile ushoga, usagaji, utumiaji wa madawa ya kulevya, kutomcha Mungu na uzinzi vyote vinanifanya niombe mwisho wa dunia uje mapema ili tusiendelee kuona uchafu huu,” alisema. Alifafanua kuwa enzi zake hakuwa ‘anarukaruka’ kwa wanaume ndiyo maana aliolewa na mume mmoja ambaye ameshafariki na alizaa naye watoto watano na sasa ana wajukuu wanne na kitukuu kimoja.