Tuesday, October 7, 2014

WAINGIA KWENYE KABURI KUZUIA MAZISHI YA BIBI YAO...SOMA ZAIDI

WAJUKUU wa marehemu Sabina Ngalu (77) wameibua kituko makaburini kufuatia kuzama ndani ya kaburi la marehemu huyo na kugoma kutoka wakidai kwamba mpaka walipwe shilingi laki moja (100,000), Uwazi lina mkanda mzima.
Wajukuu wa bibi huyo wakiwa kaburini.
Tukio hilo la aina yake lilijiri mwishoni mwa wiki iliyopita katika Kitongoji cha Nyamwanza Kata ya Sima wilayani Sengerema mkoani Mwanza muda mfupi baada ya mwili wa marehemu kuwasili eneo la mazishi kwenye shamba lake ukitokea Kanisa la Roman Katoliki Parokia ya Yesu Kristo Mfalme la mjini Sengerema.
Sababu za wajukuu hao kung’ang’ania ndani ya kaburi hilo walitaka wapewe ng’ombe mmoja au pesa hizo taslimu kwa mjibu wa mila na desturi za kabila la Kisukuma jambo ambalo lilipingwa na baadhi ya wanandugu waliodai mila hizo zilipitwa na wakati.
Kufuatia wajukuu hao kuendelea kugomea ndani ya kaburi, kaka wa marehemu, Enosi Ngalu alikwenda  kukata fimbo na kuwashukia kisha kuwacharaza viboko wote huku nao wakisisitiza hawatoki mpamka ‘kieleweke’.
Padri na wananchi wakiwa makaburini.
Baadhi ya wajukuu walioonja joto la jiwe ya kuchapwa viboko ni Andrea Mabula, Sabina Bukuru, Johari Bukuru, Asha Bukuru, Faida Bukuru, Yuves Petro, Semeni na kiongozi wao, Enos Ntilaga.
Kitendo cha wajukuu hao  kuendelea kugoma kutoka kaburini kilimchefua Padri Nicodemus Mayalla ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Yesu Kristo Mfalme, Sengerema ambaye aliamua kuondoka eneo la maziko huku akiwataarifu polisi kuhusiana na vurugu hizo.
Kufuatia hali hiyo, mmoja wa waombolezaji alizama mfukoni na kutoa kiasi hicho cha pesa na kuwapa ndipo walipokubali kutoka dani ya kaburi hilo ili mazishi yaendelee.
Ili kuonesha alikerwa na kitendo hicho, Padri Mayalla ambaye kwa wakati huo alikuwa amewekwa chini na baadhi ya ndugu wakimsihi kutosusia mazishi hayo, aligoma kurejea kaburini kuongoza ibada ya mazishi.
Jeneza lenye mwili wa bibi huyo likishushwa kaburini.
Baada ya vuta nikuvute, hatimaye Padri Mayalla alikubali kuendelea na ibada lakini aliwataka wajukuu hao kurudisha pesa waliyochukua na kuwaomba radhi wana mtaa huo na ndipo yeye aweze kurudi kaburini.
Wajukuu hao waliitwa mbele ya padri huyo  na mbele ya wana mtaa, wakaomba samahani ikiwa ni pamoja na kurudisha kitita hicho cha pesa paroko huyo naye akarejea kaburini na kuongoza ibada ya mazishi.
Hata hivyo, wakati ibada ikiendelea  polisi zaidi ya wanne kutoka Kituo cha Polisi Sengerema wakiwa na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) na mabomu ya machozi walifika eneo la tukio  ili kuhakikisha amani na utulivu vinatawala.
Polisi akiwa eneo la tukio.
Cha kushangaza, saa baada ya kutoka makaburini, wajukuu hao waliwahi nyumbani kwa marehemu, Mtaa wa Mlimani, Kata ya Nyatukala wilayani Sengerema na kuanzisha timbwili jingine kwa kuficha chakula na vyombo vya kupakulia wakidai warudishiwe pesa yao waliyoirejesha makaburini kwa shinikizo la baba paroko.
Baada ya timbwili hilo kukolea, mmoja wa wafiwa alizama mfukoni na kutoa shilingi laki moja na kuwakabidhi wajukuu hao ambao walirudisha chakula jikoni na taratibu za waombolezaji kupata chakula ziliendelea.