SIMANZI! Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Abdu Jumaa iliyopo Kitunda, jijini Dar es Salaam, Enock Mseti (20) alitekwa na watu wasiojulikana kisha kuuawa kikatili na maiti yake kutupwa kando ya reli hivi karibuni.
Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Kitunda, baba mzazi wa marehemu, Reuben Mseti alisema kijana wake ambaye hakuwa na tabia ya kushiriki katika makundi maovu, aliondoka jioni baada ya kufanya kazi zake za nyumbani kama ilivyokuwa kawaida yake.“Mwanangu alikuwa afanye mtihani wa kidato cha nne mwaka huu, ingawa kutokana na hali yangu kiuchumi kuwa mbaya, alikuwa amesimama kwenda shuleni, lakini nilikuwa katika jitihada za kuhakikisha anafanya mtihani huo,” alisema mzee Mseti kwa huzuni.
“Hili ni pigo kubwa sana kwangu na familia yangu ndugu mwandishi, maana kijana huyu ndiye alikuwa kila kitu hapa nyumbani, ukizingatia mimi na mke wangu umri umeshatuacha. “Kwa jinsi mwili wake ulivyokutwa, inaonekana aliuawa mbali na pale alipotupwa kwa sababu katika paji la uso wake, kulionekana alama ya kupigwa na kitu kizito, mikono na miguu yake ilikuwa imevunjwa, lakini nguo alizovaa hazikuwa na damu kuonyesha kama kulikuwa na purukushani.“Sehemu aliyokutwa marehemu ni mita chache tu kutoka nyumbani katika eneo ambalo lina kipori kidogo karibu na ilipopita reli,” alisema mzee Mseti.
Kijana ambaye ni msaidizi wa kazi za nyumbani kwa mzee huyo aliyejitambulisha kwa jina la Seleman Abdallah alisema siku ya tukio marehemu aliondoka na kurudi nyumbani majira ya saa nne kuulizia chakula, akidai kuwa awekewe kidogo tu kwani asingekula sana, kisha akaondoka.
“Marehemua aliondoka na akarudi kama saa 5 hivi usiku na kuondoka tena, lakini safari hii hakurudi hadi tulipopata taarifa za kufa kwake jambo ambalo lilitushangaza,” alisema Abdallah. Marehemu alizikwa katika Makaburi ya Kinyamkera yaliyopo Kitunda jijini Dar es Salaam.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, Amina.
IMESOMWAAAA