Kashfa ya aliyekuwa Miss Tanzania, Sitti Mtemvu imechukua sura mpya baada ya Wakala wa Uzazi, Vifo na Ufilisi (Rita) kusema kuwa wamekamilisha upekuzi wa taarifa alizotumia kuombea cheti cha kuzaliwa na vielelezo hivyo vimelekwa polisi vikafanyiwe kazi.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, Ofisa mtendaji mkuu wa Rita, Phillip Saliboko na Meneja masoko na mawasiliano, Josephat Kimaro walisema upekuzi wa nyaraka zilizotumiwa na Sitti uliofanywa na wanasheria wao, tayari umekamilika.
“Kazi yetu (Rita) tumeimaliza na upekuzi wa taarifa za Sitti umekamilika na kinachofuata sasa ni kupeleka nyaraka hizo kwenye mamlaka inayohusika ambayo ni polisi, wao ndio wataamua nini cha kufanya,” alisema Kimaro.
Alisema Rita haiwezi kumhukumu moja kwa moja mrembo huyo kuwa alighushi nyaraka na kudanganya ili apate cheti hicho cha kuzaliwa kilichotolewa na Rita Septemba na badala yake wanapeleka vielelezo walivyonavyo polisi ili nao wavifanyie kazi.
“Sisi (Rita) jukumu letu lilikuwa ni upekuzi wa nyaraka, kazi ambayo imefanywa kwa ustadi mkubwa na jopo la wanasheria wetu na hadi sasa imekamilika na kinachofuata ni kuzipeleka nyaraka hizo polisi ambao wao ndiyo wenye jukumu la uchunguzi na kumchukulia hatua Sitti au la,” alisema.
Wakati huohuo, Saliboko akieleza kuwa bado wana changamoto ya baadhi ya watu kudanganya taarifa zao ili wapate vyeti vya kuzaliwa na kusisitiza kuwa wanaandaa mfumo maalumu ili kukomesha udanganyifu huo.
“Tukibaini mtu ametumia udanganyifu ili kupata cheti, kwanza huwa tunamfutia cheti chake na taratibu nyingine za kisheria zinafuata. Tunafanya hivyo kwa watu wote wanaokuja kuomba vyeti kwetu na siyo kwa Miss Tanzania peke yake japo hili la Sitti tunaiachia mamlaka husika ifanye kazi yake,” alisema.
Sitti Mtemvu aliingia kwenye kashfa ya kudanganya umri wake na nyaraka zake mbalimbali zilionyesha alizaliwa 1989, umri ambao umepitiliza ule unaotakiwa kwa mshiriki wa mashindano ya Miss Tanzania, huku cheti chake kikionyesha alizaliwa 1991, hivyo kulazimika kuvua taji hilo.
Wakati huohuo, mrembo aliyevikwa taji la Miss Tanzania nambari mbili, Lilian Kamazima anatarajiwa kuwasili leo mjini Arusha na kupokewa kwa shangwe akiwa na taji lake.
Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa Kampuni ya Mwandago Entertainment Ltd, Faustine Mwandago iliyosimamia ushindi wake ngazi ya kanda ilisema kuwa mrembo huyo atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) saa 6:00 mchana.
Mwandago alisema kuwa mrembo huyo atapokelewa na wenyeji wake, wakiwamo wazazi wake na kisha kupanda gari la wazi ili kuwapa fursa wakazi wa Arusha kumshuhudia.
Alisema kuwa mara baada ya kuwasili Arusha atapelekwa moja kwa moja nyumbani kwao, Sakina ili kushiriki hafla aliyoandaliwa na wazazi wake pamoja na ndugu, jamaa na marafiki.
Wakazi wa Arusha wametakiwa kujitokeza kwa wingi kumpokea mrembo huyo kwa lengo la kumpa moyo na kulikaribisha taji hilo mara baada ya ukame wa muda mrefu wa kupata taji la Miss Tanzania.