Sunday, January 18, 2015

MWIGULU ANUSURIKA KIFO, APOTEA ANGANI SAA SITA NA HELIKOPTA

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amenusurika kifo, baada ya kupotea angani kwa saa sita akiwa ndani ya helikopta iliyokuwa inazunguka sehemu mbalimbali mkoani  Tanga.

Ndege hiyo iliyopoteza mawasiliano na waongoza ndege, inayotumika katika mikutano yake kwa vile  pamoja na uwaziri ni Naibu Katibu Mkuu CCM Bara.

Tukio hilo lilitokea jana  wakati anatoka Kilindi kwenda wilayani  Muheza, kwa ajili ya mkutano wa hadhara uliokuwa ufanyike kwenye uwanja wa Orofea.

Kiongozi huyo kabla ya kupata mkasa huo, alihutubia mkutano wa hadhara na alipomaliza alianza safari kuelekea wilaya za Pangani, Mkinga na  Muheza kwa ajili ya mikutano.

Nchemba alisema kuwa wakati anatoka Kilindi alipoteza mawasiliano na kulazimika kuzunguka angani zaidi ya saa sita.

Baadaye rubani  alipofika wilayani Muheza, alipata mawasiliano japo walikuwa wamechelewa.  Nchemba akiwa ndani ya ndege hiyo alitua salama katika uwanja wa mpira wa Jitegemee wilayani Muheza ambapo alipokelewa na mwenyeji wake mbunge wa jimbo la Muheza Herbert Mntangi (CCM) na Mkuu wa Wilaya ya  Subira Mgalu.

Akiwa katika mkutano, alisema kuwa watahakikisha tatizo la maji katika mji wa Muheza linamalizika na kwamba katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/17 watatenga fedha za ndani bila kujali wahisani.