Wednesday, January 7, 2015

MWILI WA MSIERRA LEONE ALIYEUAWA AKITOROKA WASOTA MUHIMBILI



WAKATI mwili wa mtuhumiwa wa dawa za kulevya, Abdul Koroma (33) aliyeuawa wakati akijaribu kutoroka ukiendelea kuhifadhiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala limesema linasubiri kujitokeza kwa ndugu wa marehemu wakati wowote kwa ajili ya kuja kuuchukua mwili huo. 

Akizungumza na paparazi jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Mary Nzuki alisema mbali ya kusubiri ndugu hao, pia wanasubiri utaratibu wa ubalozi wa Sierra Leone, anapotokea marehemu huyo ili kujua nini hatua zipi zichukuliwe na kwamba suala hilo lipo mikononi mwa polisi wa kimataifa (Interpol).

Koroma aliuawa Desemba 31, mwaka jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alikopelekwa kusomewa mashitaka ya kukutwa na gramu 1,229 za dawa za kulevya, zinazokadiriwa kuwa na thamani ya Sh milioni 61 alizokamatwa nazo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Koroma aliuawa baada ya kupigwa risasi na askari wakati akijaribu kuruka uzio kwa nia ya kutoroka baada ya kuomba kwenda ‘kujisaidia’, tukio lililothibitishwa na jeshi la polisi.

“Hadi ninavyozungumza hivi sasa, mwili wa marehemu bado unaendelea kuhifadhiwa katika hospitali za Muhimbili, tukisubiri ndugu yeyote wa marehemu kujitokeza au uamuzi wowote kutoka katika ubalozi wa nchi yake kama wataamua asafirishwe au azikwe hapa hapa nchini,” alisema Nzuki.

Alisema kikubwa wanachosubiri kwa sasa ni taarifa za Interpol ili kujua nini kifanyike kuhusu mwili huo kwa kuwa suala hilo hawawezi kulimaliza hivi hivi kwa kuwa marehemu alikuwa raia wa nchi nyingine tofauti na Tanzania.

Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema kimsingi, kesi ya mtuhumiwa huyo kwa sasa imefutwa, kwani mhusika hayupo tena duniani.