Friday, January 2, 2015

NITAMUUNGA MKONO MBOWE KUHUSU UFISADI WA BOMBA LA GESI GHARAMA KUZIDISHWA MARA MBILI

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe amesema atamuunga mkono Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe pale atakapowasilisha hoja yake bungeni kuhusu ufisadi wa zaidi ya Sh1 trilioni katika mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Zitto aliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa mkoani hapa uliandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF) kuwashukuru wakazi wa mkoa huo kwa kuwachagua viongozi wa chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Najua bado mnalia kuhusu bomba la kupeleka gesi Dar es Salaam, machozi yenu yatafutika kwani tayari habari za ufisadi mkubwa katika ujenzi wa bomba hili zimeanza kuchomoza.

“Kiongozi wa Upinzani Bungeni (Mbowe) ametamka mara kadhaa kuwa atatoa hoja kuhusu ufisadi katika ujenzi wa bomba la gesi. Pale atakapohitaji msaada wetu tutamsaidia, tunaamini gharama za mradi huu zimezidishwa mara mbili na inawezekana kabisa kuwa zaidi ya Dola ya Marekani 600 milioni (zaidi ya Sh1 trilioni) zimegawanywa kwa watu kama rushwa kuanzia China mpaka hapa Tanzania. Machozi yenu wana Mtwara yatafutwa kwa uwezo wa Mola,” alisema Zitto.