Wednesday, January 14, 2015

TANESCO: KUNA TATIZO LA UPATIKANAJI UMEME WA LUKU


 “Tumewasiliana nao na wametuhakikishia kuwa baada ya muda mfupi watarekebisha kasoro zilizojitokeza ili huduma ziendelee kama kawaida,” alisema Mramba. 
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema kuna tatizo la upatikanaji wa Luku katika baadhi ya maeneo, lakini jitihada zinaendelea ili kurekebisha hali hiyo.
Kauli hiyo imekuja baada ya jana na juzi baadhi ya wateja kukosa huduma hiyo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Felichesmi Mramba alisema jana kuwa: “Tunajua kuna tatizo hilo hasa kwa wale wanaonunua kwa wakala wetu wa Selcom na Multicom, lakini kampuni husika ya Itron inalifanyia kazi suala hilo.
“Tumewasiliana nao na wametuhakikishia kuwa baada ya muda mfupi watarekebisha kasoro zilizojitokeza ili huduma ziendelee kama kawaida,” alisema Mramba.
Tulipata malalamiko hayo kutoka kwa wananchi tofauti waliotaka kujua chanzo cha kutokuwapo kwa huduma hiyo.
Mkazi wa Ubungo Riverside, Winnie Mnganga alisema juzi alilazimika kulala gizani baada ya miamala yote aliyoifanya ya kununua umeme kutokamilika.
“Nilinunua umeme mara kadhaa lakini sijafanikiwa kupata units...Nilifanya hivyo tangu saa kumi na moja jioni lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote. Sijui Tanesco wanashida gani, wasipokata umeme basi tatizo jingine jipya linaibuka,” alisema Mnganga.
Mkazi mwingine wa Tabata Bima, Kelvin Julius alisema alipatwa na tatizo hilo licha ya kujaribu kununua Luku kwa kutumia njia mbalimbali, ikiwamo ya simu ya mkononi.
“Hata nilipojaribu kwenda katika kituo cha uuzaji wa Luku hali iliendelea kuwa hivyo, japokuwa leo (jana) asubuhi nilifanikiwa kukamilisha muamala na sasa hivi umeme upo,” alisema Julius.
Kuhusu maeneo ya Tegeta, Changanyikeni, Mbezi na Makongo kukosa umeme, Mramba alisema hali hiyo ilitokana na mvua zilizonyesha juzi kuathiri miundombinu. “Nguzo tano za umeme zilianguka Goba pamoja na nyaya kukatika, hali ilisababisha maeneo hayo kukosa umeme,” alisema.