Saturday, January 3, 2015

WABUNGE WENGI WANAENDEKEZA WAGANGA WA KIENYEJI

Hirizi ya ajabu
Imeelezwa kuwa wabunge wengi  wamekosa hofu ya mungu kutokana na kuendekeza waganga wa jadi hivyo kutawaliwa na roho za kishetani na kuendekeza pesa matokeo yake hawako karibu na wananchi wao.

Hayo yamesemwa na Askofu wa Kanisa la Tanzania Field Evangelism(TFE)maarufu kanisa la Emmanuel mjini Shinyanga Edson Mwombeki wakati wa kongamano la siku 5 la wachungaji na maaskofu 200 kutoka makanisa ya kipentekoste nchini la kufunga mwaka 2014 na kukaribisha mwaka 2015.

Askofu huyo alisema hivi sasa wabunge wanapotoka bungeni wanaanza kugawa pesa kama andazi na kwamba hakuna mbunge anayetoka bungeni na kwenda kwa wachungaji kuombewa na badala yake wabunge wamekuwa na waganga wa kienyeji wakiamini kuwa ndiyo watawasaidia katika uongozi wao na maisha yao kwa ujumla.

“Tumewafanyia uchunguzi,ni wabunge wachache hawana waganga wa kienyeji,sasa hivi kila mmoja ana waganga wake,wanategemea waganga wa kienyeji kila saa,sisi ndiyo waangalizi wa watu,tukikujua una ndumba tunakusalimisha kwa Yesu unaokoka”,alisema Mwombeki.

“Wabunge wanaendekeza uganga wa kienyeji,ndiyo wanaowazunguka, ndiyo maana maaskofu tumechukia, na sisi biblia inatukaza kuongozwa na mtu anategemea miungu sasa sisi tunamuuliza katibu mkuu wa CCM taifa Abdulrahman Kinana,Je CCM ni ya uganga wa kienyeji?”,alihoji Mwombeki.
 Aidha alisema Chama cha Mapinduzi kimeanguka katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 kwa sababu mbalimbali ikiwemo wakuu wa wilaya na mikoa kutokuwa karibu na wananchi na wabunge kutumia  pesa zao kuhonga wananchi na sasa wengine wanadiriki hata kununua hadi viwanja vya makanisa ili wajenge gereji zao.

“Leo nataka nimwambie ndugu yangu Kinana anayefanya kazi kubwa kuimarisha chama kuwa mchawi wa CCM ni baadhi ya watendaji wake,asiposahihisha ategemee anguko kubwa katika uchaguzi mkuu 2015,na hawa wabunge wasimdanganye”,alisema askofu huyo.

 “Tunampa tahadhari tu Katibu mkuu wa CCM Kinana na hii siyo siasa kwa sababu hii ishara ya kuanguka kwenye vijiji inatosha,afanye jitihada aite wachungaji kama anaweza kuwasikiliza,na akumbuke kuwa hawa wabunge, aliowaweka kuwaongoza wananchi hawasikilizi watu watamdanganya tu”,aliongeza Mwombeki.

Askofu Mwombeki alimshauri Kinana kurekebisha changamoto zinazotokana na viongozi wake wabovu ili kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi ujao huku akimtaka kuacha kukaa ofisini na kupokea taarifa kwa sababu atadanganywa bali atembelee wananchi.

Aidha alimshauri Kinana kushughulika na watenda kazi wake badala ya kung’ang’ana na wala rushwa pekee huku akimtaka kufuatilia katika mikoa waliyoanguka tatizo siyo sakata la Tegeta Escrow bali uongozi mbovu wa wakuu wa wilaya,wakuu wa mikoa na wabunge wasiopenda kuwajibika na kutokuwa karibu na wananchi.

Alisema katika uchaguzi mkuu ujao wachungaji na maaskofu hawataki wabunge wafanyabiashara wanaolangua wananchi na badala yake wanajipanga kupeleka wabunge wenye hofu ya mungu ili waweze kumsaidia rais ajaye.

“Tunataka viongozi wenye hofu ya mungu,wenye nia ya kusaidia nchi na kusaidia kupumua kwa rais ajaye,kwani rais wetu wa sasa Jakaya Kikwete ametumia nguvu nyingi kwa watu wabovu,Tunampongeza kwa kazi nzuri,rais huyu kila mara matatizo,huwezi kuongoza nchi kwenye matatizo unamaliza hili linakuja jingine”,alisema.

Aidha alisema alishangaa kuona wagombea wa CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa waliokuwa wakifanya kampeni kwa kutumia magari na wengine wakiwa wamevaa suti wakishindwa na wagombea wa vyama vya upinzani wenye hali duni ya kimaisha ambao vazi lao kuu ni kandambili hali inayoonesha kuwa wananchi hawaridhishwi na utenda kazi wa viongozi waliowachagua.

Aliongeza kuwa viongozi wengi wa vyama vya upinzani walioshinda katika uchaguzi walianzia makanisani kuombewa ndiyo maana wameshinda bila kutumia pesa na nguvu nyingi.