Ludewa ni moja kati ya wilaya tano zinazounda mkoa mpya wa Njombe. Upande wa Kaskazini, Ludewa inapakana na Wilaya ya Njombe Vijijini na Wilaya ya Makete. Kusini Mashariki kuna Mkoa wa Ruvuma na Kusini Magharibi inapakana na Nchi ya Malawi na Ziwa Nyasa.
Pia Ludewa ni jimbo la uchaguzi linaloongozwa na Mheshimiwa Deogratius Haule Filikunjombe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Wiki iliyopita, Uwazi lilichanja mbuga mpaka kwenye jimbo hilo na kuzungumza na wananchi mbalimbali kisha kuhitimisha kwa kuzungumza na mheshimiwa mbunge.
MATATIZO YA WANANCHI
Wakizungumza na Uwazi kwa nyakati tofauti, wananchi wa Kata za Madope, Luponde na Lusitu walizitaja kero zinazowasumbua kuwa ni ukosefu wa maji safi na salama, huduma duni za afya katika zahanati, vituo vya afya (kwa mfano Mlangali) na Hospitali ya Wilaya ya Ludewa ambayo haina umeme wa uhakika na uchache wa wataalamu na watumishi wa afya.

Kero nyingine ni ukosefu wa magari ya kubebea wagonjwa ‘Ambulance’, hali iliyomlazimu mbunge wa jimbo hilo, wakati mwingine kujitolea mwenyewe kununua magari hayo, kwa mfano alinunua gari la kubebea wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Mlangali, ubovu wa miundombinu na uhaba wa walimu, madarasa na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
Matatizo mengine ni kukosekana kwa umeme maeneo mengi ya jimbo hilo, kukosekana kwa mawasiliano ya simu na ushuru mkubwa wanaotozwa wananchi wakati na kabla ya kuuza mazao yao.Pascal Msigwa, mkazi wa Kijiji cha Mkiu jimboni humo, alimsifu mbunge wao kwamba anajitahidi kushirikiana nao katika shida na raha lakini akaongeza kwamba kasi yake ya kuwatetea bungeni, hairidhishi kwani anazungumza mara chache sana, hali ambayo inawafanya wavunjike moyo katika kufikia ndoto ya maisha bora kwa kila Mtanzania.
Amon Mtega, ni mkazi wa Kata ya Mlangali ambaye yeye alisema: “Kwa kweli mbunge wetu hajafanya makubwa kama alivyoahidi wakati akiomba kura kwani kero za maji, umeme na huduma za afya katika Kituo cha Afya cha Rugalawa na Hospitali ya Wilaya ya Ludewa zipo palepale.”
Uwazi lilifanikiwa kufika katika Kituo cha Afya cha Rugalawa na kubaini kuwa kinakabiliwa na matatizo ya upungufu mkubwa wa wahudumu, vitanda, dawa, vifaa vya tiba huku huduma ya umeme wa jua ikiwa si ya uhakika kutokana na ubovu wa miundombinu yake.
Wananchi kutozwa michango mingi ni kero nyingine iliyobainishwa na wananchi wa jimbo hilo ambapo Casto Mtitu, mkazi wa Kata ya Kitewele alisema wamekuwa wakitozwa michango mingi wasiyokuwa na uwezo nayo kama vile gharama za huduma ya afya (matibabu) na ujenzi wa shule za sekondari za kata.
“Hata hivyo, shule ambazo tunachangia ujenzi wake bado zina upungufu mkubwa wa walimu, vifaa vya kujifunzia vikiwemo vitabu vya kiada na ziada ,vyumba vya maabara ikiwa ni sambamba na vifaa vyake, tunauliza hiyo michango tunayotoa inaenda wapi?” alihoji Mtitu.
Kwa upande wa miundombinu ya barabara, wananchi wengi waliozungumza na Uwazi, walimpongeza mbunge wao wakisema amejitahidi kuboresha barabara katika maeneo mengi ambapo zinapitika katika kipindi chote cha mwaka.
MAELEZO YA MBUNGE
Baada ya kusikia kero za wapiga kura, Uwazi lilimtafuta mbunge wa jimbo hilo lakini hakuweza kupatikana ofisini kwake kwa maelezo kwamba alikuwa bungeni mjini Dodoma. Uwazi halikuishia hapo, lilimtafuta kwa njia ya simu ambapo alipopatikana, alisema kuwa kwa kipindi cha miaka kumi ya ubunge wake amejitahidi kutekeleza ahadi zake muhimu alizowaahidi ambazo zilikuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo na kero kubwa kwa wakazi wa jimbo hilo.

Kwa upande wa nishati ya umeme, mawasiliano ya simu na upatikanaji wa maji safi na salama, Filikunjombe alisema kuwa hizo ni changamoto kubwa zinazomkosesha usingizi na kueleza kwamba tayari baadhi ya changamoto hizo zipo kwenye mchakato wa utekelezaji na nyingine ameshazitatua kabisa.
Akizungumzia sekta ya afya, mbunge huyo alisema kwamba kwa sasa kuna unafuu mkubwa wa huduma katika baadhi ya zahanati na vituo vya afya ukilinganisha na kipindi cha nyuma. Hata hivyo, alikiri kwamba bado kuna changamoto za hapa na pale lakini akaahidi kuongeza jitihada zaidi za kuboresha huduma katika sekta hiyo ya afya kwa muda uliobakia.
Filikunjombe alihitimisha kwa kuwaomba ushirikiano wapiga kura wake na kuwataka wavute subira kwani matatizo yote anayatambua na mengine yapo kwenye mchakato wa utekelezaji.