ZOEZI la utafutaji miili ya watu 150 waliopoteza maisha katika ajali ya ndege ya Ujerumani aina ya Airbus A320 yenye namba za usafiri 4U 9525 iliyoanguka jana katika Milima ya Alps, Ufaransa limeendelea leo huku kifaa cha kunasia sauti kikipatikana huku kikiwa kimeharibika.
Vikosi vya uokoaji vikiwa eneo la tukio.
Waziri wa maswala ya ndani nchini Ufaransa, Bernard Cazeneuve, amesema kuwa kifaa hicho cha kunasa sauti kwenye ndege kilipatikana jana Jumanne baada ya kuanguka kwa ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Ujerumani ikitokea Hispania.
Mbali na kuharibika, Waziri Cazeneuve amesema kuwa kifaa hicho bado kitatoa taarifa kwa wataalam wanaojaribu kubaini kilichosababisha kuanguka kwa ndege hiyo, ambayo iliwauwa abiria na wahudumu waliokuwemo kwenye ndege hiyo.
Helikopta zimeonekana zikipaa katika eneo la tukio huku maofisa wa polisi wakiendelea kuchunguza mabaki ya ndege hiyo.
Maofisa wakuu wanaonya kuwa kupata mabaki ya miili ya abiria itachukua muda mrefu kutokana na hali mbaya ya anga katika eneo hilo.
Kansela wa Ujerumani pamoja na Rais wa Hispania na waziri wake mkuu, wanatarajiwa kuzuru eneo la ajali hiyo leo Jumatano.