TAASISI ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu(NIMR),imesema vijana wenye umri wa kuanzia miaka 30 na kuendelea, wanaongoza kwa kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,Mkurugenzi wa NIMR,Dk.Mwele Malecela alisema kwa sasa tatizo hilo ni kubwa ambalo linawakumba vijana wengi hususan barani Afrika.
Alisema hali hiyo,imesababisha vijana hao kutafuta dawa za kuongeza nguvu za kiume aina ya Mundex,ili waweze kupunguza ukubwa wa tatizo hilo.
“Vijana wengi wenye umri wa kuanzia miaka 30 na kuendelea wana matatizo ya upungufu wa nguvu za kiume, jambo ambalo limewafanya kutafuta dawa za kuongeza nguvu ili waweze kuzitumia na kupunguza ukubwa wa tatizo.
“Tangu tugundue dawa hii, idadi kubwa ya wanaokuja kununua ni vijana hasa wenye umri wa miaka 30,hali ambayo inaonesha wazi kuwa tatizo hili linakua kwa kasi,”alisema Dk Mwele.
Alisema kipindi kilichopita, matatizo hayo yalikuwa yanawapata wanaume wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea, lakini sasa hivi ni tofauti kabisa ambapo vijana wenye umri huo ndiyo wenye matatizo hayo.
“Miaka iliyopita tatizo hili lilionekana ni la watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea,sasa hivi ni tofauti kabisa ambapo matatizo hayo yameshamiri kwa vijana, jambo ambalo limewafanya kutafuta dawa ndani na nje ya nchi ili waweze kujitibia,”alisema.
Alibainisha kuwa taasisi hiyo kwa kushirikiana na tiba mbadala walifanya utafiti na kubaini kuwa dawa ya Mundex inaweza kuwasaidia kupunguza ukubwa wa tatizo.
Taasisi hiyo,pia imebaini idadi kubwa ya wanawake wakiwamo watoto, wana matatizo ya uvimbe tumboni(Fibrous) hasa kwa waafrika.
Alisema dawa hiyo imethibitishwa kisheria na kwamba inaweza kutumika mahali popote kwa sababu haina madhara kwa binadamu.
Alisema kutokana na hali hiyo,wanaweza kuitafuta katika ofisi zao za kanda ili waweze kuinunua na kuitumia, jambo ambalo linaweza kuwasaidia.
“Tulifanya utafiti na kubaini kuwa dawa ya Mundex ina uwezo wa kupunguza tatizo la upungufu wa ngufu za kiume.
“Kwa sababu imethibitishwa kisheria, kila mmoja mwenye matatizo anaweza kuitumia ili iweze kumsaidia,”alisema.
Alisema kwa sasa inaonekana tatizo hilo ni kubwa ambalo linaongezeka siku hadi siku, hali hiyo inaweza kuwaathiri wanaume wengine kupata matatizo hayo.
Alisema kutokana na hali hiyo, wameiomba Serikali kuwaongezea fedha ili waweze kufanya utafiti ambao utaweza kubaini chanzo cha tatizo hilo na tiba zaidi inayowafaa ili kuwatibia wataopata matatizo.
Akizungumzia kuhusu uvimbe, Dk.Malecela alisema tatizo hilo ni kubwa linalowafanya wagonjwa kufanyiwa upasuaji.
“Sasa hivi hadi watoto wanafanyiwa upasuaji kwa ajili ya uvimbe,hali ambayo inaonyesha wazi kuwa tatizo hilo ni kubwa linahitaji nguvu ya ziada,ikiwamo kufanya utafiti ili kupata ufumbuzi,”alisema.
Alisema taasisi yake,ina watalaamu na wasomi wa kutosha ambao wanaweza kufanya utafiti wa kiwango cha juu na cha kimataifa ambacho kinaweza kuwajengea imani kwa jamii na watanzania kwa ujumla.
Alisema mpaka sasa, wameweza kujenga uhusiano na vyuo vikuu mbalimbali ndani na nje ya nchi ambavyo vimeweza kuwatuma wanafunzi kwenda kupata mafunzo kwa njia ya vitendo.
Alisema miongoni mwa tafiti ambazo ziliwafanya wafanikiwe ni pamoja na utafiti wa majaribio ya chanjo ya ukimwi na malaria nchini.
Alisema katika utafiti wa chanjo ya ugonjwa wa Ukimwi, taasisi hiyo ilishiriki katika tathmini ya upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya na majaribio ya tiba ya virusi vya HSV-2(Herpes Simplex Virus2) katika kupunguza maambukizi ya Ukimwi.
“Pia tulifanikiwa kupata dawa ya usugu ya kurefusha maisha kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi(VVU).
“Tulifanikiwa kufanya uchunguzi wa vimelea vya Ukimwi katika maziwa ya mama anayenyonyesha,”alisema.
Alisema, licha ya kufanya tafiti hizo wana changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na ukosefu wa rasilimali fedha, hali ambayo inafanya washindwe kufanya tafiti za mara kwa mara.
Alisema mpaka sasa wana miundombinu mibovu pamoja na uhaba wa ofisi katika kituo cha Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH) na Tanga ambapo wanatumia majengo ya kupangisha ambayo gharama zake ni kubwa.
Alisema mkakati uliopo ni kuhakikisha wanafanya tafiti mbalimbali zenye tija ambazo zitaweza kuisaidia Serikali kutatua matatizo yaliyopo nchini.