Monday, April 27, 2015

Majambazi Wavunja Kaburi....Wamvua Marehemu Nguo Na Viatu, Watimka Na Mabegi Aliyozikwa Nayo


Watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamebomoa kaburi la Napegwa Kishaluli (75) mkazi wa Mailimoja Kibaha mkoani Pwani aliyezikwa Aprili 20 mwaka huu na kumvua nguo zote pamoja na kuchukua mikoba aliyokuwa amezikwa nayo.
 
Tukio hilo lilitokea Aprili 24 mwaka huu katika Kata ya Tangini jirani na soko la Loliondo ambako baada ya mazishi kaburi hilo liliwekewa mlinzi kwa muda wa wiki moja.
 
Mkataba wa mlinzi huyo ulipomalizika aliondoka na siku iliyofuata kaburi hilo lilivunjwa.
 
Watu wa karibu na familia ya marehemu wamesema kuwa baada ya mazishi ulikuwapo uvumi kwamba marehemu alizikwa na vitu vya thamani zikiwamo fedha, simu, pete na mikufu ya dhahabu pamoja na nguo zenye thamani kubwa.
 
Hata hivyo, taarifa zinasema marehemu Kishaluli alizikwa na mikoba miwili ya nguo na vitu vyake vingine na kwamba kabla ya kifo chake aliagiza azikwe na vitu vyake.
 
Akizungumza na Mwandishi wetu jana,ndugu wa marehemu,Bartholomew Mwanjile alisema baada kuzika walilazimika kuajiri mtu wa kulinda kaburi hilo la ndugu yao kwa wiki moja lakini siku moja baada ya mkataba kumalizika kaburi hilo lilivunjwa.
 
“Tuliweka mlinzi alinde kaburi hilo kwa wiki moja tukiamini litakuwa limekauka kwa sababu lilitengenezwa kwa zege.
 
“Tuliamini watu wenye nia mbaya watashindwa kulivunja jambo ambalo limekuwa kinyume kwa vile baada ya muda huo kumalizika kaburi lilibomolewa na watu wasiojulikana ambao waliamini ndani ya mikoba hiyo kulikuwa na fedha,” alisema Mwanjile.
 
Mwanjile alisema baada ya kuvunja kaburi hilo majambazi walifungua jeneza na kupekua ndani kwa kuligeuza na kuliweka tofauti na lilivyokuwa awali, baada ya kumvua marehemu nguo zote na viatu alivyokua amevalishwa na hata soksi nazo walichukua.
 
Alisema tukio la kuvunjwa kwa kaburi hilo limetokea baada ya uvumi kuwa ndugu yao alizikwa na nguo na vitu vingine zikiwamo fedha, kiasi cha Sh milioni 8, cheni ya dhahabu,simu za gharama na kompyuta mpakato(laptop),jambo ambalo si la kweli.
 
“Tulimzika ndugu yetu na mikoba ya nguo zake ambazo aliagiza kabla ya mauti kumkuta na kaburi tulijenga kwa zege lakini tukashauriana tuweke mlinzi, hapo ndipo watu wakaanza kutia shaka wakadhani kuna vitu vya gharama jambo ambalo si kweli,” alisema Mwanjile.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jafari Mohamedi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea na watakaobainika watachukuliwa hatua za sheria