Wednesday, April 15, 2015

MKE AANGUA KILIO KANISANI MUMEWE AKIFUNGA NDOA YA PILI


DHAMBI? Neema Pangani, mkazi wa jijini Dar alijikuta akiangua kilio kanisani wakati mumewe Daniel Mhina alipokuwa anamuoa mke wa pili, Irene Lema, Risasi Mchanganyiko lina stori kamili.
Neema Pangani, akilia baada ya mumewe kuoa mke wa pili.
Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita katika Kanisa la Evangelistic Assemblies of God (EAGT) Bonde la Baraka lililopo maeneo ya Alimaua Kijitonyama jijini Dar, ambapo Mchungaji Kiongozi  Asheri Mwaisunga ndiye aliyebariki ndoa hiyo.
Wakati ndoa inafungwa katika kanisa hilo, mke halali wa Daniel, Neema ambaye naye ni muumini wa kanisa hilo, aliamua kutoka nje na kuangua kilio. “Ndoa yangu na Daniel tulifunga Desemba 15, mwaka 1991 katika Kanisa la Evangelistic Assembies of God Tanzania (EAGT), Uzuri Manzese jijini Dar ambapo mchungaji Asheri Mwaisunga (huyohuyo aliyefungisha ya pili) ndiye aliyefungisha ndoa hiyo.
Mume akisaini hati ya ndoa.
“Wakati naposwa na mume wangu Daniel nilikuwa tayari nina mtoto ambaye nilikuwa nimezaa na mwanaume mwingine lakini nikasikia kuna mama alikuwa anataka Daniel amuoe ndugu yake, nikamuuliza mume wangu akasema hapendi kupangiwa mtu wa kumuoa kwa sababu ndoa ni ya watu wawili na mimi ndiye nilikuwa chaguo lake,” alisema Neema na kuzidi  kumwaga maelezo kuwa, mchungaji huyo aliposikia matatizo yao, alimshauri Daniel atafute mwanamke mwingine akidai yeye hana kizazi.
Kwa upande wake Daniel, alijitetea kuwa yeye amefunga ndoa ya bomani Ijumaa iliyopita na pale kanisani alikuwa akibariki na amefanya hivyo baada ya kugundua mke wake ana matatizo.
Mke akisaini hati ya ndoa.
“Ni kweli nimefunga ndoa lakini ni ya bomani na nilitoa tangazo siku 21 kabla, hakukuwa na kipingamizi chochote na pale kanisani juzi nilikuwa ninabariki ili nipate baraka kutoka kwa mchungaji wangu ambaye nilimuomba baada ya kuona kwamba mimi ni muumini mzuri,” alisema na kusisitiza mkewe huyo wa zamani alikuwa na matatizo.
Cheti cha ndoa ya kwanza.
Mchungaji Asheri Mwaisunga alipotafutwa kwa njia ya simu alijitetea na kudai kuwa yeye hakufungisha ndoa hiyo ila alikuwa akiibariki baada ya kufungwa bomani: “Mimi sikufungisha hiyo ndoa kwani tayari walishafungishwa na Mkuu wa Wilaya na baada ya pale ndiyo wakaja kanisani kwa ajili ya kubarikiwa, mkitaka vielelezo kamili kuhusu hilo nendeni kule mtapata.”
Hata hivyo gazeti hili lilinasa picha za Daniel akionekana kusaini cheti cha ndoa kanisani hapo licha ya mchungaji na Daniel kudai pale walikwenda kubariki.