Monday, May 18, 2015

HUU NDIO MTAMBO MAALUMU UTAKAONASA WAHARIFU WA MTANDAO!

Dar es Salaam. Siku chache baada ya kupitishwa kwa sheria ya makosa ya uhalifu wa mtandao, mtambo wa kutambua makosa hayo wa TZ-CERT umezinduliwa.

Mtambo huo unaoendeshwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), utakuwa ukikusanya taarifa hasi za wahalifu zitakazotumika ushahidi kwenye vyombo vya dola.

Akizindua mtambo huo, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa alisema lengo la kutengenezwa mtambo huo ni kuhakikisha kunakuwapo na usalama katika mitandao ya kijamii.

Alisema mtambo huo umekuja wakati mwafaka kuungana na sheria ya mtandao iliyosainiwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete.
Profesa Mbarawa alisema Sh800 milioni zimetumika kutengeneza mtambo huo.

“Katika kipindi cha miaka 10 makosa ya uhalifu kwenye mtandao yameongezeka maradufu, hivyo mtambo huu utakuwa mwarobaini wa kukabiliana na changamoto hiyo,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema mtambo huo utaunganishwa kwenye taasisi zote muhimu likiwamo jeshi, polisi na benki ili kuhakikisha Taifa linakuwa salama wakati wote.

Profesa Mbarawa alisema utafanya kazi ya kuratibu usalama wa mitandaoni kwa kuwashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi.

Wakati huohuo, Mbarawa alizindua mtambo maalumu wa TCRA utaofanya kazi ya kuangalia mihamala ya fedha zinazopitia katika simu za mikononi (Mobile Money Monitoring).

Kaimu Mkurugenzi wa TCRA, Dk Joseph Kilongola alisema uangalizi huo umekuja baada ya kubainika kuwa kuna fedha nyingi ‘zinatembea’ kwenye mitandao ya simu, hivyo ni vyema Serikali ikawa na takwimu sahihi za mapato yanayotokana na huduma za mawasiliano.

“Mitambo hii yote ni muhimu ili kupunguza na kudhibiti wizi wa mtandaoni,” alisema na kuongeza kuwa pia utaleta imani ya wananchiwanaotumia huduma hiyo ya fedha kwenye simu hali itakayokuza uchumi wa nchi.”
-MWANANCHI