Monday, May 18, 2015

TOTO LA PELE LABEBA TUZO YA MWANASOKA BORA MWAFRIKA LIGUE 1 UFARANSA…NA NDIYO LINAHAMA TIMU

KIUNGO wa kimataifa wa Ghana, Andre Ayew(pichani kulia) amesherehekea siku zake za mwisho na klabu ya Marseille, baada ya kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Mwafrika wa Ligi Kuu ya Ufaransa, maarufu kama Ligue 1 leo.
Ayew, mwenye umri wa miaka 25, amewapiku Max-Alain Gradel wa Ivory Coast na Saint-Etienne Mtunisia Aymen Abdennour wa Monaco.
Winga huyo kijana – aliyekuwamo kwenye kikosi cha Ghana kilichofungwa na Ivory Coast kwa penalti 9-8 katika Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka huu – ameteuliwa na jopo la Waandishi wa Habari na atakabidhiwa tuzo ya Marc-Vivien na kituo cha Redio Ufaransa, RFI na chaneli ya Televisheni France 24 baadaye leo.
Ayew, ambaye mdogo wake Jordan pia alikuwa Marseille kabla ya kuhamia Lorient mwanzoni mwa msimu, anazivutia klabu kadhaa za England zikiwemo Newcastle, Tottenham, Arsenal na klabu aliyokuwa akiishabikia utotoni, Liverpool.
Mtoto huyo wa gwiji wa zamani wa soka Ghana na Marseille, Abedi Pele ameonyesha dalili za kuhamia Ligi Kuu ya England, baada ya kutangaza atahitimisha miaka yake 10 ya kuwa na vigogo hao wa Ufaransa, mwishoni mwa msimu huu.