Baraza la Uslaama la Umoja wa Matiafa leo limeitisha kikao cha dharura kujadili hali ya mambo Burundi baada ya jenerali mwandamizi wa jeshi la nchi hiyo kutangaa kuipindua serikali ya Rais Pierre Nkurunziza.
Kikao hicho cha dharura kimeitishwa na Ufaransa huku katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akitoa wito wa utulivu na ustahamilivu nchini Burundi.
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa unafuatilia kwa karibu kinachoendelea nchini Burundi na kusisitiza kauli ya Katibu Mkuu Ban Ki-moon aliyotoa wakati wa mkutano wa viongozi wa umoja wa Afrika huko Addis Ababa, Ethiopia kuhusu awamu za uongozi.
Hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric aliyezungumza mjini New York, wakati wa mkutano na waandishi wa habari waliotaka kufahamu msimamo wa chombo hicho kuhusu hali iliyoripotiwa Burundi.
Jana baada ya kuenea habari kuwa Jenerali Godefroid Niyombare amempindua Rais Pierre Nkurunziza, rais huyo alijaribu kurundi nchini kwake kutokea jijini Dar es Salamu, Tanzania alikokuwa amekwenda kushiriki kikao cha marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.
Hata hivyo ndege yake ilishindwa kutua baada ya askari watiifu kwa Niyombare, kuzingira uwanja wa ndege wa Bujumbura.
Kuna madai kwamba kundi la vijana linalounga mkono serikali limeshambulia kituo kimoja cha habari cha binafsi mjini Bujumbura. Kundi hilo linalojulikana kama Imbonerakure, baadhi ya watu wanaamini kwamba vijana hao wanatumiwa kama wapiganaji na kwamba huenda wamepewa silaha ili kuwatishia raia kabla ya uchaguzi.
Hali bado ni tete nchini Burundi, barabara nyingi nchini huo hazina watu kwa kipindi kirefu cha alfajiri huku wengi wakisalia majumbani mwao kuhofia usalama.
Huku hali hiyo ikiendelea, risasi zimesikika zikilindima wakati ambapo jeshi la serikali limekuwa likikabiliana na wafuasi wa Jenerali Niyombare katikati mwa mji mkuu wa Burundi, Bunjumbura, mahala ambapo tangazo lilitolewa jana Jumatano kuwa Rais Pierre Nkurunziza, amepinduliwa.
CHANZO: IRAN SWAHILI