Tanzania imepoteza asilimia 60 ya tembo wake katika miaka sita iliyopita zaidi kutokana na ujangili kwa ajili ya pembe za ndovu. Wanaonufaika zaidi na pembe za ndovu ni baadhi ya wafanyabiashara haramu wa nchini China na katika nchi nyingine zenye watumiaji wa bidhaa zitokanazo na pembe za ndovu huku Tanzania ikibaki kuwa muathirika wa tatizo hili.
Msanii Ali Kiba amepata dili ya kuwa Balozi wa WildAid |
Muimbaji maarufu wa Afrika Mashariki Alikiba ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa kampeni hii alisema. “Ninafurahi kupewa heshima hii na nitatumia nafasi hii kutoa kila mchango ninaoweza kutoa katika jitihada hizi za kulinda wanyama pori wetu”, alisema Ali Kiba. “Tembo wetu wazuri lazima waachwe waweze kuishi katika mazingira yao ya asili badala ya kuishia kuwa pambo kwenye meza ya mtu”, aliongeza Ali Kiba.
Katika utafiti wa hivi karibuni uliohusisha zaidi ya Watanzania 2,000 waishio vijijini na mijini, zaidi ya asilimia 79 walioshiriki walisema kuwa watasikitika endapo tembo watatoweka Tanzania na zaidi ya asilimia 73 walisema wanaamini kuwa tembo ni utambulisho na urithi wa taifa.
“Watanzania wote bila kujali wanapoishi, ni wadau wa rasilimali hii ya wanyama pori”, alisema Peter Knights, Mkurugenzi Mtendaji wa WildAid. Kauli mbiu ya kampeni hii ‘Ujangili Unatuumiza Sote’ inatukumbusha kuwa wale wote wanaojihusisha na ujangili wa kuua tembo na kusafirisha pembe za tembo hao kimagendo kwenda Asia ya Mashariki wanatuumiza Watanzania sote”.
Dk. Patrick Bergin, Afisa Mtendaji Mkuu wa African Wildlife Foundation, alisisitiza kwamba ujangili unachafua jina la Tanzania nchi ambayo ina sifa ya kuwa na hifadhi kubwa ya tembo.
“Tanzania imekuwa ikijulikana kwa kuwa na makundi makubwa ya tembo ambapo ukijumlisha na Botswana na Zimbabwe utaona kuwa nchi hizi kwa pamoja zina nusu ya tembo wote waliopo barani Afrika,” alisema Bergin. “Hata hivyo, kiwango cha sasa cha ujangili kinatishia kufuta sifa hii ya kipekee. Wakati Watanzania wanazidi kujifunza zaidi kuhusu janga hili kupitia hii kampeni, tunaamini kuwa watashirikiana na sisi kuilinda mali hii adimu.”
Kampeni hii itatumia redio na televisheni, mitandao ya kijamii, magazeti, mabango na filamu zitakazoonyeshwa maeneo ya wazi ili kuwafikia wananchi wengi iwezekanavyo wakiwemo wakazi wa vijiji vilivyoko ndani ndani.
Video mpya inayomhusisha Ali Kiba na Jacqueline Mengi tayari imetengenezwa na imeonyeshwa kwa mara ya kwanza katika uzinduzi wa kampeni hiyo.