Saturday, July 4, 2015

MAAJABU YA MOROGORO! WAAMKA KULA DAKU, WAMKUTA NYOKA MWENYE HIRIZI!

Nyoka huo baada ya kuuawa.

Dustan Shekidele, Morogoro
Inatisha! Ndani ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, familia ya mwanaume aliyetambuliwa kwa jina la Hamis Juma, imekumbwa na mauzauza baada ya kuamka ili kula daku na kukutana na nyoka mwenye hirizi mlangoni.
Mama mwenye nyumba hiyo, Mama Nurdin akitaharuki baada ya kutokea hali hiyo.
Tukio hilo lililozua taharuki lilijiri mapema wiki hii kwenye nyumba ya familia hiyo inayoishi Mtaa wa Mkota Kata ya Kiwanja cha Ndege mjini hapa.
Majirani wakishangaa hali hiyo.
Baada ya kutonywa juu ya tukio hilo, Ijumaa lilifika kwenye familia hiyo alfajiri na kushuhudia nyoka huyo aliyekuwa na hirizi na kitambaa cheusi shingoni akiwa mlangoni.
Akisimulia kisa hicho baba wa familia hiyo, Hamis alisema kuwa waliamka saa 7:00 usiku ili kupata daku kama kawaida kwani walianza kufanya hivyo tangu walipofunga.
“Wakati tukiwa sebuleni tunakula, tulianza kuona damu nzito ikisambaa kutokea mlangoni.
“Ukweli tulishtuka sana. Tulipofungua mlango tulishtuka kuona nyoka mkubwa mlangoni akiwa na hirizi huku damu zikiendelea kusambaa kutoka pale alipokuwa yule nyoka.
“Ilibidi tufunge mlango hadi alfajiri tuliamua kuwaita watu waje kushuhudia na kusaidia kumuondoa,” alisema Hamis.
Diwani wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Mohamed Matikula akimpa pole Mama Nurdin.
Katika kutafuta msaada wa kumuondoa nyoka huyo na kusafisha damu zilizozagaa, alitokea mjomba wa familia hiyo ambaye jina halikupatikana akaanza kumtoa kwa kutumia mti, jambo lililosababisha taharuki kwa watu waliokuwepo wakaanza kukimbia.
Baada ya kumtoa nyoka huyo, watu walianza kumpiga wakitaka kumchoma moto lakini alitokea mwanaume asiyefahamika akamkwapua na kuanza kukimbia naye mitaani.
Wakati akikimbia, kundi la watu lilikuwa likimkimbiza ndipo alimtupa na kutokomea kusikojulika.
Katika hali ya kushtua zaidi, nyoka huyo alibadilika, akawa hana hirizi huku akionekana ‘kadogo’ jambo lililoibua madai ya ushirikina hivyo watu wakamuua.

Baba mwenye nyumba hiyo, Hamis Juma.
Kwa upande wake mke wa Hamis, Mama Nurdin ambaye ni mjumbe wa mtaa huo, alishtushwa na tukio hilo na kusema familia yake imekumbwa na hofu kubwa.
Uongozi wa Kata ya Kiwanja cha Ndege ukiongozwa na Diwani, Mohamed Matikula na Afisia Mtendaji, Diha Zongo walifika eneo la tukio na kuwachukua baba na mama wa familia hiyo hadi ofisi ya kata kwa mahojiano zaidi.