HABARI ya Mwenyekiti wa Klabu ya Bongo Movie Unity, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ kujiuzulu wadhifa wake siyo mpya lakini Ijumaa Wikienda linakudadavulia sababu zilizochochea bosi huyo abwage manyanga.
Kwa mujibu wa chanzo makini, bosi huyo alitakiwa ajiuzulu mwenyewe katika mkutano wa wanachama uliofanyika Ijumaa iliyopita katika Viwanja vya Leaders Club, kutokana na tuhuma mbalimbali huku wanaodaiwa kutangaza nia ya kugombea urais 2015, Edward Lowassa na Bernard Membe wakitajwa.
Mapaparazi wetu waliokuwepo eneo la tukio, walishuhudia wasanii mbalimbali wakiendesha ajenda ya kumng’oa Steve Nyerere.
Mapaparazi wetu waliokuwepo eneo la tukio, walishuhudia wasanii mbalimbali wakiendesha ajenda ya kumng’oa Steve Nyerere.
Wanachama hao walidai kwenye uongozi wa Steve kumekuwepo na ufisadi, kutumia madaraka vibaya na ubadhirifu mkubwa hivyo bora ajiengue. Steve alionesha kukasirishwa na tuhuma hizo ambazo alidai hazikuwa na ukweli wowote lakini hadi mwisho wa kikao, wanachama waliendelea kushikilia msimamo wao kwamba ajiuzulu.
Punde tu baada ya kikao hicho kilichokosa muafaka kumalizika, Steve Nyerere alitangaza kupitia mtandao wa Instagram kwamba amejiuzulu wadhifa wake.Mapaparazi wetu walipomtafuta Steve alifunguka kuwa aliamua kujiachia ngazi ili kulinda heshima yake.
Hata hivyo, madai ya Steve Nyerere kujiuzulu yalipingwa vikali na wanachama wenzake wa Bongo Muvi waliodai kuwa amejikosha lakini ukweli ni kwamba wamemng’oa.Uongozi wa Steve Nyerere ulioteuliwa mwaka jana, umekuwa ukikumbwa na kashfa kibao za uchakuchuaji wa fedha zikiwemo za rambirambi na mambo mengine yahusuyo klabu.
Hata hivyo, kuna tetesi kwamba wanasiasa wanaotajwa kuwania urais 2015, Lowassa na Membe ndiyo waliosababisha mtafaruku huo kwa kuwagawa wasanii hao, kila mmoja akimshabikia mwanasiasa anayemtaka.