Chama cha ACT wazelendo jana kimenza mafunzo ya siku mbili mfululizo kwa wagombea wake wa nafasi za ubunge nchini mafunzo ambayo yamelenga kuwajengea uwezo na kujiamini zaidi kuelekea kufanya kampeni na kutafuta nafasi za uwakilishi wa katika majimbo mbalimbali kikiwa ni chama pekee nchini Tanzania kulichoendesha mafunzo kama hayo kwa sasa.
Kiongozi mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe akizungumza na wanahabari wakati wa mafunzo hayo alisema kuwa chama hicho ni chama pekee nchini Tanzania kilichodiriki kuwapa mafunzo ya kuelekea katika uchaguzi ili kuwaweka katika mstaari mmoja wa kuhakikisha kuwa wanakwenda na lugha moja kwa watanzania kueleza mipango na ilani ya chama hicho.
Zitto alisema kuwa chama cha ACT wazalendo ndio chama pekee nchini Tanzania ambacho kina agenda maalum kwa watanzania tofauti na vyama vingine ambavyo alisema kuwa vinatumia mbwembwe na ulaghai kwa watanzania bila kuweka wazi nini wanataka kuwafanyia watanzania.
Alisema kuwa mambo ambayo chama hicho kimekuwa kikiyapigania na kitaendelea kuyapigania ni pamoja na mambo ya hifadhi ya jamii kuhakikisha kuwa watanzania wote wanafaidika nayo,pamoja na miiko ya uongozi na kukemea ufisadi kwa nguvu moja ambapo alisema kuwa kwa sasa hakuna chama hata kimoja kinachothubutu kusimama na kukemea ufisadi kwani nao wamekuwa sehemu ya ufisadi huo.
Historia Zilizowekwa na ACT
Akizungumzia historia iliyowekwa na chama hicho,Zitto alisema kuwa ACT kimeweza kusimamisha wagombea ubunge katika majimbo 219 kati ya majimbo 265 jambo ambalo linakifanya chama hicho kuwa ni chama cha pili kwa wagombea ubunge wengi huku cha kwanza kikiwa ni chama cha mapinduzi CCM.
Historia nyingine ambayo chama hicho kimeiweka ni kuweza kusimamisha wagombea ubunge wanawake wengi kuliko vyama vingine vyote nchini Tanzania ambapo chama hicho kimesimamisha wanawake 25% sawa na wabunge 55 katika majimbo toifauti tofauti nchini Tanzania huku kubwa ni kusimamisha mgombea urais mwanamke.
Zitto alitaja historia nyingine kuwa ACT wazalendo ndio chama pekee kilichosimamisha wagombea wenye umri mdogo kuliko vyama vyote nchini ambapo mgombea mwenye umri mdogo ana miaka 21 na mwingine akiwa na miaka 23 ambapo alisema kuwa ni ishara kuwa chama hicho kinawajali vijana.
Changamoto wanazokabiliana nazo
Akizungumzia changamoto ambazo chama hicho kinakumbana nazo,Zitto alisema ni hujuma mbalimbali kutoka kwa wapinzani wao ikiwemo kukatwa kwa majina kadhaa ya wagombea wao bila sababu za msingi.
Chama hicho kitazindua kampeni zake siku ya jumapili katika viwanja vya zakiem mbagala Jijini Dar es salaam ambapo wanatarajia kuweka wazi mipango na ilani ya chama hicho.