Thursday, October 22, 2015

Madai ya kumuua Kanumba…Lulu kizimbani tena

lulu mungu (3)Nyota wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’.
Stori: Na Brighton Masalu
MAMBO yameiva! Nyota wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’ (20) yu mbioni kupanda tena Kizimba cha Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kwa ishu yake ile ya madai ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa msanii wa filamu nchini, marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’, Amani lina ripoti mkononi.
Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka ndani ya mahakama hiyo jijini Dar, kesi hiyo ilisimama kwa muda wa mwaka mmoja na zaidi kutokana na matatizo yaliyo nje ya uwezo wa mahakama, lakini sasa matatizo hayo yameisha hivyo kesi hiyo itaanza kurindima siku yoyote kuanzia sasa.
StevenKanumba.jpgAliyekuwa Staa wa filamu nchini, marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’
NI BAADA YA MWAKA MMOJA NA MIEZI NANE
Tangu kusimama kwa kesi hiyo, mwaka 2013, ilitarajiwa kuanza tena kusikilizwa Februari 17, 2014 lakini ikakwama kutokana na matatizo mbalimbali ya kimahakama.
ITAANZA UPYA
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, mwendesha mashtaka wa serikali atamsomea mashtaka upya Lulu lakini neno la msingi kwenye mashtaka hayo ni; mnamo Aprili 7, 2012 anadaiwa kumuua bila kukusudia, Steven Kanumba.
“Baada ya kuulizwa, Lulu akiwa kama Elizabeth Michael atajibu anachotaka kutoka moyoni kulingana na ukweli anaoujua kisha jaji atampangia tarehe ya kurudi tena,” alisema mtoa habari huyo.
MAHAKAMA ITATUMIA MWONGOZO WA JAJI MKUU
Tofauti na madai ya awali kwamba, kesi hiyo ingeendeshwa kwa siku 730, habari za uhakika zinasema kuwa, kesi itakapoanza safari hii haitasimamishwa mpaka siku ya hukumu. Kwa hiyo itategemea na kasi ya hakimu husika.
“Lakini pia, kauli ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman anayoitoa kila Siku ya Sheria Duniani (Februari 3) kwamba kesi zote za jinai zisipitishe miaka miwili, itazingatiwa,” kilisema chanzo.
Kikaongeza: “Lakini nadhani ikianza safari mwaka huu, naamini mpaka mwaka 2017 itakuwa imemalizika kama sheria ya miaka miwili itazingatiwa.”
lulu na cheniCHENI BADO MDHAMINI
Chanzo hicho kilisema kuwa, bado mcheza sinema maarufu Bongo, Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ anaendelea kutambulika na mahakama kama mdhamini wa Lulu. Kwa hiyo, anatakiwa kuendelea na jukumu la kumlinda Lulu ili asiruke dhamana (asitoroke, asikiuke masharti ya dhamana).
MASHAHIDI WAJIPANGE
Chanzo kilisema baadhi ya mashahidi muhimu nao watapewa taarifa ya kimaandishi ili tarahe ya kesi wafike mahakamani.
Mashahidi hao ni Dokta Kidume ambaye alikuwa akimtibu Kanumba pia ndiye alikuwa mtu wa pili kufika kwenye chumba cha marehemu mara baada ya kuanguka na kupoteza maisha.
Seth Bosco naye anatakiwa kujiandaa kupokea wito huo kwani yeye siku ya tukio alikuwa nyumba moja na marehemu (vyumba tofauti). Yeye alimshuhudia Kanumba akiwa katika hali mbaya baada ya kutoelewana na Lulu na kukimbia kwenda kumwita Dokta Kidume.
WAKILI WA LULU AZUNGUMZA
Peter Kibatala ni wakili maarufu jijini Dar. Yeye ndiye mwanasheria katika kesi ya Lulu. Amanililimtafuta ili kujua hatima ya kesi hiyo na madai kwamba iko njiani kuanza upya. Alisema:
“Aaa! Sijajua. Lakini kwa kawaida mahakama itakapoona mambo yameanza, kesi inatakiwa kuanza kusikilizwa itatakiwa kutoa taarifa siku sita kabla.”
AMZUNGUMZIA LULU
Wakili Kibatala alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, mteja wake (Lulu) amekuwa akimpigia simu mara kwa mara akitaka kujua tarehe ya kesi yake kuanza tena.
“Hata Lulu mwenyewe amekuwa akinipigia simu kuulizia ni tarehe ngapi kesi yake itaanza tena. Nitapewa taarifa siku sita kabla,” alisema mwanasheria huyo.
LULU PRESHA INAPANDA
Naye rafiki wa karibu wa Lulu, akizungumza na gazeti hili huku akiomba hifadhi ya jina lake, alisema:
“Ninyi mnaandika Lulu siku hizi anakunywa sana pombe. Mnajua hayuko sawasawa. Ile kesi yake ya kumuua (bila kukusudia) Kanumba inamtesa sana kichwani.
“Ukimya wa kesi unamfanya ashindwe kujua hatima yake. Kila akikumbuka anampigia simu wakili wake. Mbaya zaidi kuna watu wanamwambia kesi inaweza kukaa kimya kwa muda mrefu halafu siku moja ikalipuka na kuwa nzito. Kwa hiyo wakati mwingine mjue hilo.”
WASOMAJI WETU
Baadhi ya wasomaji wa Magazeti Pendwa ya Global Publishers  wamekuwa wakipiga simu chumba cha habari na kuulizia kama kesi ile ilifutwa kinyemela au kihalali.
“Jamani Global, mimi shida yangu ni kuulizia kuhusu ile kesi ya Lulu na Kanumba. Hivi bado ipo au ilishafutwa kinyemela. Maana si mnajua watu maarufu tena huenda kuna kubebana,” aliwahi kuuliza msomaji mmoja.
LULU ASAKWAJumatatu na Jumanne iliyopita, simu ya Lulu ilipopigwa iliita muda mrefu bila kupokelewa. Hata hivyo, baadhi ya watu wake wa karibu walisema Lulu huwa hapokei simu ambayo jina halipo kwenye simu yake.