Tuesday, November 10, 2015

Bibi Harusi Amkimbia Bwana Harusi Saa Chache Kabla Ya Ndoa Kufungwa


Mwanamke aliyejulikana kwa jina la Doroth Msuya, mkazi wa Monduli mkoani Arusha, ametoweka muda mfupi kabla ya kufunga ndoa na Joseph Machange, mkazi wa Mwika, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
 
Ndoa ya wawili hao ilitarajiwa kufungwa Jumamosi ya Novemba 7 katika Kanisa la Kinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Usharika wa Lole, Mwika.
Mchungaji mwenza wa usharika huo, Elikeseni Shao, alisema majira ya saa sita na nusu mchana wakati maandalizi ya ibada ya ndoa yakiwa yamekamilika, walipokea taarifa za kutoweka kwa bibi harusi huyo akiwa saluni.
 
“Sisi kama viongozi wa kanisa tulipokea kwa masikitiko taarifa za kutoweka kwa aliyekuwa bibi harusi mtarajiwa wakati akiwa saluni, na kwamba liliwashtua sana ikizingatiwa kuwa maandalizi yote ya ndoa yalikwisha kamilika na kumuacha bwana harusi solemba,” alisema.
 
 Alisema uongozi wa kanisa hilo baada ya kupewa taarifa hizo iliwalazimu kuitisha kikao cha familia zote mbili na kuzungumza nao juu ya tukio hilo ambapo pia walichukua hatua ya kuzifanyia maombi familia hizo ili zisiingie katika mawazo ya imani za kishirikina.
 
Akielezea mazingira ya tukio hilo, mmiliki wa saluni aliyokuwa akipambiwa bibi harusi, Stella Mringo, alisema awali alimpokea mteja huyo saa nne asubuhi na ilipofika saa sita na nusu mchana alimuomba amruhusu atoke kwenda kujisaidia.
 
Alisema bibi harusi huyo alitoka nje akiwa na mpambe wa watoto aliyefahamika kwa jina moja la Esther.
 
“Lakini mpambe huyo alirudi na kuchukua khanga ya bibi harusi na alipotoka tena hakumkuta,” alisema.
 
Kwa upande wake, mshereheshaji wa sherehe hiyo, William Ngalo, alisema akiwa kwenye ukumbi  wa sherehe uitwao Mamba Complex, alipokea taarifa kuwa asiendelee na kazi ya kufunga muziki kwa kuwa kuna matatizo yamejitokeza, na alipofuatilia alijulishwa kuwa bibi harusi alitoweka katika mazingira ya kutatanisha.
 
Alisema  bibi harusi huyo alitafutwa eneo lote la Mwika bila kupatikana jambo lililolazimu chakula kilichoandaliwa katika sherehe hiyo kuliwa nyumbani kwa wazazi wa bwana harusi majira ya saa tatu usiku.
 
Kwa upande wake, baba wa bwana harusi mtarajiwa, Eliringia Machange, alisema wao kama familia wamepokea kwa masikitiko tukio hilo na kwa sasa hawawezi kusema chochote.
 
Bwana harusi mtarajiwa, Joseph Machange, alisema jambo lililomtokea haliamini kwani limemuumiza, hasa baada ya kutumia fedha zaidi ya milioni saba kwa ajili ya maandalizi ya harusi hiyo.
 
Alisema kwa sasa suala hilo limeripotiwa katika kituo kidogo cha polisi Himo, na kwamba wanasubiri uchunguzi uendelee.