WAZIRI na Naibu Waziri wake katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wameshindwa kufanikiwa kwenye juhudi zao za kushawishi wapate uwaziri katika Serikali ya Rais, Dk. John Magufuli, huku mmoja kati yao akitapeliwa shilingi milioni 40.
Viongozi hao wote walikuwamo katika wizara moja, kufuatia mabadiliko ya mwisho ya baraza la mawaziri yaliyofanywa na Kikwete huku Raia Mwema likielezwa kwamba walitaraji nguvu ya ushawishi kupitia kwa “madalali” itafua dafu kwenye serikali ya Magufuli.
“Naibu Waziri wakati wa Kikwete ndiye aliyetapeliwa shilingi milioni 40. Huyu aliingia katika Baraza la Kikwete baada ya kushawishi kupitia kwa mmoja wa wake za kigogo mwandamizi serikalini. Mama huyo ndiye aliyemshawishi mumewe ambaye naye bila shaka alimshawishi Kikwete kwa sababu ni lazima washauriane katika uundaji wa baraza kutokana na nafasi zao za juu za uongozi nchini.
“Sasa alidhani awamu hii mambo yatakuwa hivyo hivyo, akakutana na ‘madalali’ ambao ni kweli wapo wengi na ninyi (gazeti la Raia Mwema) mlikwishawahi kuandika namna udalali ulivyokuwa ukifanywa na baadhi ya maofisa wa Ikulu hata katika kuweka miadi ya kumwona Rais.
“Jamaa (anamtaja jina) aliamini amekwishaweka mambo sawa, Magufuli alipotaja awamu ya kwanza ya Baraza lake hakuwamo na wala bosi wake wa zamani hakuwamo, wakajijengea matumaini kwamba akimalizia vile viporo vya wizara nne watakuwamo.
“Desemba 22, Naibu Waziri huyo wa zamani alipewa taarifa na madalali wake kwamba yumo kwenye orodha na kwa hiyo afike Dar es Salaam kwa kuwa siku inayofuata (Desemba 23) mawaziri watatajwa. Alisafiri usiku hadi Dar. Rais alipotoa taarifa ya mawaziri wake jioni ya Desemba 23 hakuwamo.
“Mwenzake (aliyekuwa waziri utawala wa Kikwete) alipanga kwenda kufanyiwa maombi Nigeria kwa Nabii T.B Joshua, sidhani kama atakwenda tena maana ilikuwa asafiri siku chake kabla ya Desemba 23, sijui nini kilimchelewesha hadi habari mbaya ikamkuta nchini kabla hajasafiri,” alieleza mtoa taarifa wetu na kusisitiza kwamba, Magufuli amepania kufuta udalali wa kusaka vyeo, na hata wahusika katika udalali huo wanajulikana kwake.
Waziri huyo anatokea mikoa ya Kanda ya Kati wakati Naibu wake akitokea mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Raia Mwema linashindwa kutaja majina ya mawaziri hao kwa kuwa juhudi za kuwapata kuzungumzia sakata hilo ziligonga mwamba, hata simu zao za mkononi hazikuweza kupatikana.
Viongozi hao wamewahi kuongoza wizara nyeti (jina linahifadhiwa) ambayo hata hivyo, katika utawala wa miaka 10 ba Kikwete ‘ilitema’ mawaziri kadhaa kutokana na kashfa mbalimbali, baadhi zikiwa ni zile zilizowahi kuibuliwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais Magufuli, kwa mara ya kwanza alitangaza sehemu ya baraza lake la mawaziri Desemba 10, mwaka huu, baada ya kukaa kimya kwa takriban zaidi ya mwezi mmoja tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika baraza hilo, aliweka viporo vya mawaziri katika wizara nne, akitangaza mawaziri 14 tu kati ya Wizara 18 alizounda.
Wizara ambazo ziliwekwa viporo kwa maana ya kutopata mawaziri kutokana na kile Magufuli alichosema anaendelea kuwatafuta mawaziri husika, ni pamoja na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ambayo Naibu wake alimtangaza kuwa ni Edwin Ngonyani; Wizara ya Fedha na Mipango ambayo licha ya kuwa na waziri kiporo, Naibu wa Wizara hiyo alitajwa kuwa ni Dk. Ashantu Kijaji; Wizara ya Maliasili na Utalii haikupewa waziri kwa wakati huo ingawa Naibu wake alitajwa kuwa Mhandisi Ramo Makani.
Wizara nyingine iliyowekwa kiporo kwa wakati huo ni Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ambayo Naibu wake alitangazwa kuwa Mhandisi Stella Manyanya.
Baadaye, Desemba 23, Rais Magufuli alimalizia viporo hivyo ambapo alimteua Dk. Philip Mpango kuwa Mbunge na Waziri wa Fedha; Profesa Makame Mbarawa kuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano; Profesa Jumanne Maghembe kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na Dk. Joyce Ndalichako ambaye alimteua Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi baada ya kumteua kwanza kuwa mbunge. Katika orodha hiyo, vigogo hao wawili wa enzi za utawala wa Kikwete hawakuwapo.
chanzo:RaiaMwema