Friday, January 29, 2016

Samatta ajiunga na KRC Genk ya Ubelgiji

Samatta
Mbwana Samatta akiwa kwenye ndege kuelekea nchini Ubelgiji kujiunga na KRC Genk.
Sakata ya usajili wa nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars, Mbwana Samatta inaonekana kukamilika baada ya mshambuliaji huyo kukubali kujiunga na klabu ya ubelgiji ya KRC Genk.
Samatta maarufu kama Samagoal, ameanza safari ya kuelekea Ubelgiji ambapo anatarajiwa kusaini mkataba na klabu hiyo.
Ajenti wa nyota huyo, Jamal Kisongo ametetea hatua ya Samatta kujiunga na Genk licha ya Nantes kutoa donge nono Zaidi ya Genk huku akisema kuwa uamuzi huo ni kwa minajili ya ufanisi wa Samatta.
“Wachezaji wengi wa Tanzania wanaazimio la kucheza soka Ulaya na naamini fursa hiyo itafika kwani hali ya sasa itafungua milango kupitia Genk”.
Angalia umahiri wa Mbwana Samatta hapa chini:

Kisongo ameongeza kuwa mkataba huu mpya na Genk utawanufaisha pia wachezaji wa Tanzania kwani makubaliano hayo yataiwezesha klabu hiyo kusaka vipaji zaidi nchini Tanzania.

Samatta ambaye pia ni mchezaji bora wa wachezaji wa ndani barani Afrika anatarajiwa kupigania nafasi yake ya kikosi cha kwanza cha Genk.
“Ni muhimu kwa Samatta kuingia na kucheza katika kikosi cha kwanza cha Genk na inatarajiwa hali hiyo itamwezesha kutimiza ndoto hiyo,” alisema Kisongo.
Samatta-Waziri-Mkuu-15
Uhamisho wa Samatta unadaiwa kuzua utata baina yake na mmiliki wa klabu ya TP Mazembe, Moise Katumbi kwani Katumbi alichagua Nantes ambayo ilitoa kitita bora zaidi.
-Samatta aliichezea Simba kabla ya kujiunga na TP Mazembe mnamo mwaka wa 2011 na aliisaidia TP Mazembe kutwaa taji la vilabu bingwa barani Afrika huku majuzi akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa ndani ya Afrika.