Thursday, March 24, 2016

Madee Amedai Angekuwa Ameathirika na Matumizi ya Madawa ya Kulevya, Angewataja Wanaomuuzia


Msanii wa muziki kutoka Tip Top Connection Madee Ali amesema kama angekuwa anatumia Madawa ya kulevya na tayari ameshaathirika basi angewataja wale wanaomuuzia ili kuisaidia serikali kutokomeza matumizi ya madawa ya kulevya.
Madee2

Akizungumza katika kipindi cha Enewz cha East Africa Television, Madee amesema serikali inaweza kutokomeza biashara ya Madawa ya kulevya kama ikiwatumia wale walioathirika.

“Ningekuwa mimi natumia Madawa ya kulevya na tayari yameshaanza kuniathiri si utaulizwa imekuwaje kuwaje, nani amekufundisha hizi mambo, umeanza wapi umenunua kwa nani, ina maana nitaanza kumtaja yule ambaye ameniuzia, na ambaye ameniuzia mimi kikete, yeye atamtaja bosi wake, bosi wake atamtaja yule bosi wake mkubwa kwa hiyo ile cheni yote itakuja mpaka itamfikia yule kigogo anayeingiza kutoka nje”, alisema Madee

Pia Madee alisema ingawa wasanii wana nafasi yao katika kupambana na biashara ya Madawa ya kulevya, lakini serikali ndio chombo ambacho kinaweza kupambana na biashara hiyo na inatokomeza kabisa.