Sasa leo habari mpya ni
kwamba Rais Magufuli ameahirisha shamrashamra za maadhimisho ya siku ya
Muungano kwa mwaka huu ambayo huadhimishwa kila tarehe 26 ya Mwezi Aprili na
badala yake ameelekeza kuwa siku hiyo itakuwa ya mapumziko kama kawaida na
watanzania waiadhimishe wakiwa majumbani kwao ama katika shughuli zao binafsi.
Kufuatia kuahirishwa kwa
shamrashamra hizo, Rais Magufuli ameelekeza kuwa fedha zilizopangwa kutumika
kwa ajili ya kugharamia vinywaji, vyakula, gwaride, halaiki, burudani
mbalimbali na hafla ya usiku ambazo ni zaidi ya shilingi Bilioni 2, zitumike
kuanzisha upanuzi wa barabara ya “Mwanza – Airport” katika
eneo linaloanzia Ghana Quaters hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Barabara hiyo inafanyiwa upanuzi
ili kukabiliana na kero ya msongamano mkubwa wa magari ambao unaathiri shughuli
za kila siku za wananchi.