Tuesday, July 22, 2014

FUNGA HUIMARISHA KINGA YA MWILI......SOMA ZAIDI HAPA UJUE FAIDA YAKE


Kuna funga za aina nyingi, lakini kubwa ni ya kiroho ambayo waumini hufunga kwa ajili ya kutii maamrisho ya Mungu, ingawa ufungaji wake unatofautiana kutoka dini moja hadi nyingine.
Wakati Waislamu wanafunga kwa kutokula kitu chochote kuanzia asubuhi hadi jua linapozama, Wakristo wao wakati wa funga huruhusiwa kula, lakini kwa kiasi na utaratibu maalum.
Tunaposikia neno kufunga, wengi tunaliangalia tendo hilo kwa upande wa kiroho kuwa ni amri ya Mungu ambayo tunapoifuata tunapata thawabu. Funga pia huchukuliwa kama njia mojawapo ya kufanya maombi maalum kwa Muumba ili kujibiwa maombi yetu kwa namna ya kipekee.
Katika ulimwengu wa sasa, funga imegundulika kuwa njia bora ya kupambana na maradhi mbalimbali na hatari mwilini, ambayo katika hali ya kawaida yameshindikana kutibika kwa kutumia tiba za kisasa.
Ingawa funga inaonekana kama ni ibada fulani ngumu kwa baadhi ya watu, lakini Mungu bila shaka alikuwa na siri kubwa na aliamrisha tufunge kwa faida ya miili yetu na pengine kama watu wote wangekuwa wanafunga kama inavyotakiwa, bila shaka maradhi mengi yangepungua.
NINI FAIDA ZA FUNGA KIAFYA?
Faida za kufunga kimwili ziko nyingi, zikiwemo kuponya mwili. Unapofunga unaupa nafasi mwili wako kupumzika na kujitengeneza upya wenyewe. Funga inaupa nafasi mwili kuondoa sumu sehemu mbalimbali ambazo zilijijenga kwa muda wa mwaka mzima.
Halikadhalika funga hufufua upya chembechembe hai za mwili, huboresha mfumo wa hewa. Tofauti na imani kuwa mtu mwenye njaa hukosa nguvu, funga huongeza nguvu za mwili na uchangamfu wa akili pia.
Baada ya wataalamu mbalimbali wa sayansi kugundua kuwepo kwa faida kubwa ya kufunga, wamebuni funga zingine zenye lengo la kuboresha afya tu na siyo kwa mambo ya kiroho. Kuna aina nyingi za funga, kama vile kufunga kula vyakula vyote isipokuwa juisi ya matunda tu kwa siku kadhaa.
Aina nyingine ya funga-tiba ni ile ya kufunga kula vyakula vyote, isipokuwa kunywa maji peke yake kwa muda maalum. Funga za aina hii huwa ni za muda maalum zikiwa na lengo maalum, ama kupunguza uzito, kutibu shinikizo la damu, kisukari  ama magonjwa mengine. Hata hivyo, inashauriwa mtu kujijua hali yake ya kiafya kwanza kabla ya kufunga.
Faida za funga kwa ufupi ni kama zifuatazo:
-Funga huondoa sumu mwilini
-Funga hupumzisha mwili na kazi ya kusaga chakula
-Funga hupunguza hatari ya kupatwa na magonjwa ya uvimbe
-Funga huwapa ahueni wagonjwa wa kisukari ya kupanda
-Funga huharakisha uyayushaji wa mafuta mwilini
-Funga hudhibiti kiwango cha presha
-Funga huweza kupunguza uzito wa mwili
-Funga humfanya mtu kuzingatia lishe bora
-Funga huimarisha kinga ya mwili
-Funga huweza kumuondolea mtu uteja wa sigara au kilevi (addiction).
Hivyo, ni ukweli ulio wazi kuwa Waislamu au Wakristo wanapofunga ili kutekeleza amri ya Mungu, wanapata faida nyingine ya kiafya bila wao kujijua.
Hata utafiti wa kawaida nchini unaonesha kuwa watu wanaofunga hali zao kiafya huimarika sana katika kipindi chote cha Mwezi wa Ramadhani na hata idadi ya wagonjwa huripotiwa kupungua hospitalini.